Shekilindi: Wakulima Makanya kufaidika na ujenzi wa barabara

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi amesema, pamoja na kwamba nusu ya wananchi wa Kata ya Makanya hawakukipigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka jana, lakini Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa sh. bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Mlalo- Ngwelo- Mlola- Makanya- Milingano- Mashewa.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 73 itakuwa ni mkombozi kwa wakulima wa eneo hilo ambao ni maarufu kwa kilimo cha maharage, mbogamboga na matunda, na badala ya kusafirisha mazao yao kwa umbali mrefu hadi kulifikia soko kwa kupita Lukozi- Soni- Mombo- Korogwe hadi Tanga, wataweza kupita Mashewa- Daluni- Maramba hadi Tanga.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Oktoba 7, 2021 uliofanyika Kijiji cha Kulasi, Shekilindi alisema Rais Samia ametoa fedha za barabara jumla ya sh. bilioni tano kwa Jimbo la Lushoto peke yake, na kuwataka wananchi kuacha mihemko wakati wa Uchaguzi Mkuu kwa kupiga kura za chuki kwenda upinzani kisa mgombea mmoja wa udiwani kwenye kura za maoni ndani ya CCM kura zake hazikutosha.

"Nasema wazi, pamoja na kuwa hamkumpa kura Mama Samia kwenye kata hii ya Makanya, lakini Mama ametoa fedha nyingi kwenye Jimbo la Lushoto. Ametoa sh. bilioni tano, kati ya hizo, sh. bilioni 3.5 zinaletwa kwenu kwa ajili ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Mlalo- Ngwelo- Mlola- Makanya- Milingano hadi Mashewa yenye urefu wa kilomita 73, na kazi imeanza ya ujenzi wa madaraja.

"Acheni mihemko kwa kupotezwa na watu walioshindwa kwenye uchaguzi. Ni CCM pekee inayoweza kuwaletea maendeleo. Hebu fikirieni kwa mimi mneninyima kura, lakini hata Mama Samia hamkumpa kura... huko ni kukosa fadhila kwa yale yanayofanywa na Chama Cha Mapinduzi, msije mkarudia tena jambo hilo. Mimi nimewapigania kupata miradi kwa fedha za Serikali, Mfuko wa Jimbo na pesa yangu ya mfukoni, nani anaweza kufanya hivyo. Huyo mliompa kura za ubunge wala hana uwezo huo, kila kitu anategemea kwa baba" alisema Shekilindi maarufu kama Bosnia.

Shekilindi ambaye alikuwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro, alimueleza kuwa Kata ya Makanya ina uhaba mkubwa wa maji, hivyo wakati wanasubiri mradi mkubwa wa maji wa kata 13 ikiwemo hiyo ya Makanya, ameomba Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) waweze kwenda kwenye kata hiyo ili kuweza kubaini vyanzo vya maji ili wananchi waondokane na adha ya maji.

Shekilindi alisema pamoja na jitihada za kujengwa Kituo cha Afya Makanya zikiendelea, ametaka Zahanati ya Kulasi ijengwe jengo la Mama na Mtoto, kwani kwa sasa limeelemewa na wagonjwa pamoja na huduma nyingine, huku Serikali ikianza jitihada za kutafuta watumishi wengine kwa ajili ya zahanati hiyo, kwani kwa sasa ina mganga mmoja, na yupo ukingoni kustaafu.

Mkuu wa Wilaya, Lazaro aliwapa RUWASA siku moja wawe wamefika kuangalia vyanzo vya maji vilivyotajwa na Mbunge kama vitaweza kutosheleza maji, na kuweza kutatua changamoto ya wananchi kwa sasa.

Lazaro aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wao kidato cha kwanza pindi watakapofaulu, badala ya kwenda mijini kufanya kazi za ndani, kwani wakiweza kusoma na kuwa na fani za aina mbalimbali, wataweza kusaidia Taifa lao, wazazi na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla.

"Jana nilikuwa Kata ya Mbwei, nimekuta shule zote za kata hiyo kwenye vijiji vya Mavurui, Mbwei na Mhezi vimeshika nafasi ya mwisho kitaifa kwenye mitihani ya darasa la saba mwaka jana. Hatuwezi kukubali jambo hili liendelee. Tunataka na sisi Lushoto tuweze kupata madaktari, mainjinia na walimu," alisema Lazaro.

Awali, Mkuu wa Wilaya pamoja na Mbunge walipokuwa wanakagua miradi ya maendeleo, Diwani wa Kata ya Makanya Zanuali Mohamed alisema Zahanati ya Mdando imejengwa kwa nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo hadi kupaua kwake, ambapo walisomba mawe gari saba, mchanga gari nane, tofali 7,500, mbao za kupaua 556, michango ya wananchi sh. milioni 7,700, huku Mfuko wa Jimbo ukitoa bati 127, huku Mbunge Shekilindi kwa fedha zake za mfukoni alitoa bati 30. Na sasa hivi wamechoma tofali 5,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi jengo la Mama na Mtoto.

Kwa jitihada hizo zilizooneshwa na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya, aliwahakikishia kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa zahanati hiyo, huku akimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge, ambaye alikuwa ameambatana naye kwenye ziara hiyo, apeleke fedha ili kuunga mkono juhudi za wananchi.

Post a Comment

0 Comments