Spika Ndugai afanya mabadiliko Wajumbe Kamati za Kudumu za Bunge

NA GODFREY NNKO

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Yusto Ndugai amefanya mabadiliko madogo ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge.

Mabadiliko hayo ameyafanya kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 135 (3)-(5) ya Kanuni za Bunge , Toleo la Juni 2020.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 9, 2021 mabadiliko hayo ni pamoja na Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi amehamishwa kutoka Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Pia Spika wa Bunge, Mheshimiwa Ndugai amemhamisha Mheshimiwa Humphrey Hesron Polepole kutoka Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Kamati ya Sheria Ndogo.

Naye Mheshimiwa Asia Abdulkarim Halamga ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika Ndugai, amemteua Mheshimiwa Dkt.Faustine Engelbert Ndungulile kuwa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo na Kamati ya Masuala ya Ukimwi.

Pia Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Kalemani ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo.

Aidha, Mheshimiwa Spika Ndugai, amemteua Mheshimiwa Mhandisi Dkt. Leonard Madaraka Chamuriho kuwa Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo huku Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa akiteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi.

Post a Comment

0 Comments