Tanzania, ASFU wasaini makubaliano ya ushirikiano kuwezesha, kukuza uwekezaji, biashara na utalii nchini

NA MWANDISHI MAALUM

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Geoffrey Mwambe Pamoja na Rais wa Jumuiya ya Muungano Kimataifa chini ya kundi la Afrika na Asia (Afro- Asian union (AFASU),Dkt. Hossam Darwish wametia saini hati ya makubaliano ya Ushirikiano kuwezesha kukuza na kuunda ushirikiano katika sekta ya uwekezaji , wenye lengo la kuwezesha na kukuza uwekezaji, biashara na utalii nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Jijini Dar es salaam, Mhe. Mwambe ameainisha maeneo ambayo Tanzania na ASAFU watashirikiana katika kuvutia maeneo ya uwekezaji kuwa ni pamoja na uwekezaji katika Afya,kilimo, Viwanda, Biashara Mtandao, Utalii, Elimu pamoja na Uwekezaji katika TEHAMA.

Mhe. Mwambe ameeleza kuwa kusainiwa kwa hati ya makubaliano kunaonyesha dhamira kubwa ya serikali ya awamu ya sita ya kushirikiana na wadau wote duniani na kuwaalika katika uwekezaji lakini pia kutumia fursa ya kuaminika kama serikali ya Tanzania kuweza kuwaomba Taasisi na sekta binafsi waweze kutusemea ili kushawishiana kuja kuwekeza Tanzania kwasababu ya mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa nchini.

“Serikali ya awamu ya sita inaaminika na mazingira ya uwekezaji Tanzania yameendelea kuboreshwa na pia sisi kwenye Nyanja za kimataifa tafsiri yake ni kuwa tanzania inaendelea kusifika kwenye ubora wake wa mazingira ya uwekezaji,”amesema Mhe. Mwambe

Aidha, Mwambe amewashukuru wawekezaji hao na kuwahakikishia kuwa ofisi yake iko tayari kushirikiana nao kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha wanafanikiwa, na kuwataka watanzania na Taasisi nyingine za serikali kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kufanikiwa kuwekeza nchini.

“Nawashukuru sana AFASU, nawakaribisha sana na ninawaomba watanzania tuendelee kuwapa ushirikiano wote pale ambapo wataitaji vibali, ardhi, na idhini mbalimbali za serikali ili waweze kutekeleza mradi wao tutahakikisha kwamba tunasimamia hilo kwahiyo tusingependa kuwakwamisha kwa sababu hii inatupa sifa sisi na inampa pia amani Mhe. Rais na kuendelea kujenga imani kubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,"amesema.

Kwa upande wake Rais wa Jumuiya hiyo, Dkt. Hossam Darwish amesema Jumuiya ya AFASU wako tayari kutekeleza vipengele vyote ambavyo vimo ndani ya makubaliano hayo na watatekeleza kwa nguvu kubwa na haswa kwa kuanza na sekta ya kilimo ambapo ndani ya Jumuiya wanao wajumbe ambao ni wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya kilimo, ambapo wameona maeneo ya kilimo na wamevutiwa sana na fursa hiyo ya kilimo hapa nchini na hivyo wanatoa ishara njema kwamba wao watakuwa ni sehemu ya uwekezaji katika sekta hii ya kilimo pamoja na sekta nyingine ambazo zitakuwa zimeainishwa katika makubaliano.

Dkt. Hossam ameongeza kuwa, kwa hatua ya kwanza na kwa haraka wataanza na mradi wa chuo cha Kimataifa cha Kitanzania cha mifumo ya kielektroniki ambacho kitakuwa na vitivo vitivo 14 vya kimasomo ya kielimu na wanaimani kwamba vitivo hivyo vinaweza kwenda sambamba na kile walichokiona kinahitajika ndani ya nchi yetu ambapo shahada mbalimbali zitatolewa kupitia chuo hicho na kitaweza kuchukua wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika na kusisitiza kuwa, mfumo wa masomo utaweza kutoa wataalamu wa kutosha. 

Amesema, hatua nyingine itakayofuata ni mradi wa maonyesho ya biashara ambayo yatafanyika hapa nchini Tanzania ili kuweza kuchochea uwekezaji na pia jumuiya hiyo itajikita katika uwekezaji wa masuala ya utalii hususan katika ujenzi wa hoteli zenye hadhi kubwa na katika sekta ya afya watajikita katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha Dawa na vifaa Tiba .

Kwa upande mwingine, Dkt. Hossam amemshukuru Waziri wa Uwekezaji kwa kuonesha uzalendo mkubwa kwa nchi yake ambapo amekuwa na juhudi kubwa sana na kwa upande wake anamatumaini makubwa kuwa Tanzania itapiga hatua katika sekta hii ya uwekezaji kwa juhudi kubwa ambazo anazifanya Waziri wa Uwekezaji. 

Hafla hiyo ya utiaji Saini wa hati ya makubaliano ya Ushirikiano ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji Tanzania, Dkt. Maduhu Kazi, na Mkurugenzi Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis, pamoja na maafisa wa serikali kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, Wizara ya mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news