Wanawake: Rais Samia tusaidie kunusuru ndoa zetu, ubaba wa maji unatukosesha usingizi

Na Hadija Bagasha, Muheza

Wanawake wa kijiji cha Kwakibuyu Kata ya Songa wilayani Muheza mkoani Tanga wametoa kilio chao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutokana na tatizo la uhaba wa maji linalowakabili kwa muda mrefu kijijini hapo.

Hali inayopelekea kuhatarisha ndoa zao kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji.
Kina mama hao wametoa kilio hicho mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo wakati alipofika kijijini hapo kwa lengo la kujionea na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao.

Awali kina mama hao wamesema tatizo la ukosefu wa maji limekuwa likiwanyima usingizi kila kukicha na hivyo kumuomba mkuu huyo wa wilaya kuwasaidia kufikisha kilio chao kwa Rais Samia ili kunusuru ndoa zao.

Akizungumza na DIRAMAKINI Blog mmoja ya kinamama hao alisema kuwa, maji wanayotumia kwa sasa hayafai kwa matumizi ya binadamu, kwani sehemu wanayochota ni chafu, lakini pia hata mifugo imekuwa ikifanya uchafuzi wakati wakienda kutafuta maji ya kunywa.

"Mheshimiwa mkuu wetu wa wilaya tumekuwa hatuishiwi maradhi ya tumbo kila kukicha tunaumwa kutokana na maji tunayokunywa hayafai kwa matumizi ya binadamu, lakini hakuna namna tunalazimika tu kunywa, kipikia na hata kufulia, lakini pia tunatembea umbali mrefu sana kufuata maji haya haya yasiyofaa kutokana na hatuna njia nyingine ya kupata maji,"alisema mmoja wa akina mama hao.

Mama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Saumu Ally alisema kuwa kina mama wengi wamekuwa wakikosa muda wa kukaa na waume zao kutokana na muda mwingi kuutumia kutafuta huduma ya maji kitendo ambacho kimekuwa kikihatarisha ndoa zao kwa kuwa wanakosa muda wa kujenga familia zao.

Walisema mbali na changamoto hiyo ya uhaba wa maji, lakini pia wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa kijijini hapo kutokana na kuwepo kwa madarasa manne pekee ambayo yamekuwa yakitumika kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba.

Awali akizungumza na wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo amesema serikali ipo kwenye mpango wa kufikisha huduma ya maji wilayani humo kutokana na kuanza kwa miradi mikubwa ya maji ambayo serikali imeanza kutekeleza.

"Niwatoe tu hofu wananchi wetu na niwaombe kuwa wavumilivu wakati kipindi hiki serikali inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa maji utakaosaidia kuondoa tatizo la uhaba wa maji wilayani kwetu ni kweli tokea nimefika nimepita katika maeneo mbalimbali katika ziara zangu na nimejionea mwenyewe namna hali ilivyo, hivyo nitahakikisha naliwekea msukumo suala hili," amesisitiza Bulembo.

Aidha DC Bulembo amewataka wananchi wilayani humo kushiriki na kutoa ushirikiano katika zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mapema mwakani na kuwataka kuachana na dhana potofu ya kulihusisha zoezi hilo na imani za kishirikina.

"Niwasihi ndugu wananchi muondokane na dhana hii potofu ambayo nimekuwa nikiisikia, nataka niwaambie tu kuwa serikali inatoa huduma mbalimbali kwa wananchi kulingana na idadi ya waliopo, hivyo kama serikali itashindwa kujua idadi sahihi ya watu waliopo maendeleo hayatakidhi watu kwa kuwa watakaohesabiwa ni wachache ambao hawalingani na idadi iliyopo eneo husika, "amebainisha DC Bulembo.

Sambamba na hayo akizungumzia suala la vyumba vya madarasa Mkuu huyo wa wilaya amewatoa hofu wananchi hao na kusema kuwa serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.140 kwajili ya kujenga vyumba vya madarasa katika maeneo mbalimbili wilayani humo.

Hata hivyo DC Bulembo aliwasisitiza wananchi kuendelea kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19 kwani hivi sasa chanjo hizo zinapatikana katika maeneo yote wanayoishi.

Mkuu huyo wa wilaya anaendelea na ziara yake ya kujitambulisha na kusikiliza kero za wananchi katika kila kata na kijiji kwa kijiji ambapo mpaka sasa ameshafika katika kata 14 kati ya 37 zilizopo na amefika vijiji 59.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news