Wanufaika wa Mfuko wa Elimu wa Taifa wampa faraja Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania

Na Eliafile Solla- TEA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlala ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye ameonesha kufurahishwa na Jumuiya ya Shule ya Wasichana ya Makete iliyopo Mkoani Njombe pamoja na uongozi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete kwa jitihada zake za kuboresha miundombinu ya shule hiyo ambayo ilipata ufadhili kutoka Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) mwaka 2018.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzani (TEA) Bi. Bahati Geuzye (kulia) akitoa elimu kuhusu Mfuko wa Elimu wa Taifa na jinsi unavyofanya kazi kwa Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu, alipotembelea banda la TEA kwenye moja ya maonesho hivi karibuni.

Kauli hii imetolewa mkoani Njombe, Wilayani Makete katika sherehe za mahafali ya kidato cha nne shule ya Wasichana Makete ambapo Bi. Bahati Geuzye alikuwa mgeni rasmi wa sherehe hizo.

‘‘Kwanza kabisa naishukuru Jumuiya ya Shule kwa kunipa heshima kubwa ya kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali haya, lakini pia naupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete na Uongozi wa Shule kwa jitihada za kuboresha miundombinu na mazingira ya shule ambayo kwa hakika yanavutia, alisema Bi. Bahati’’.

Aliweka bayana kwamba, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inaona fahari kuwa sehemu ya mafanikio ya shule hiyo ya Wasichana ya Makete kwa kuzingatia kuwa TEA ilifadhili ujenzi wa nyumba sita (06) za walimu mwaka 2018 kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, ambazo zimezaa mtaa unaoitwa TEA.

Kwa upande wa vigezo vya ufadhili Bi. Bahati alieleza kuwa, miongoni mwa vigezo vinavyotumika kutoa ufadhili kupitia Mfuko wa Elimu nchini ni pamoja na shule kuwa na usajili rasmi na idadi kubwa ya wanafunzi kuliko miundombinu iliyopo, hivyo ufadhili hutolewa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa na kwenye matumizi ya matundu ya vyoo.

Aidha, kigezo kingine kinachotumika katika utoaji wa ufadhili wa ujenzi wa Mabweni na Nyumba za walimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ni shule kuwa kwenye maeneo ama mazingira yasiyofikika kirahisi.

‘‘Kutokana na vigezo nilivyotaja hapo juu, mwaka 2018 Shule ya Sekondari ya Wasichana Makete ilipatiwa ufadhili kutoka Mfuko wa Elimu wa Taifa kiasi cha Shilingi Milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba sita za walimu ambapo TEA ilitoa ufadhili huo kuboresha mazingira ya kufundishia kwa kuwapa Walimu makazi bora," alisema Bi. Bahati.

Aliendelea kusisitiza kwamba, mradi huo wa ujenzi wa nyumba sita (06) za Walimu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Makete, ni miongoni mwa miradi iliyotekelezwa kwa kiwango cha hali ya juu na amefarijika kuona shule hiyo imekuwa mabalozi wazuri wa TEA, ambapo wameanzisha mtaa unaoitwa TEA.

Bi. Bahati alidokeza kuwa, kutokana na mafanikio makubwa aliyoyaona katika shule hiyo ya Wasichana ya Makete ambayo imeanzishwa mwaka 2014, ni dhahiri kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya miundombinu ya elimu baada ya kuanza kutoa elimu ya Kidato cha Tano na Sita hivyo TEA itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.

Mbali na hilo, alitoa rai kwa wadau wengine wa elimu ikiwa ni pamoja na wananchi, Halmashauri na Taasisi nyingine za Umma na binafsi kuwa tayari kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika shule hiyo na nyinginezo zenye uhitaji hapa nchini ili kupunguza changamoto za elimu na kuhakikisha elimu inatolewa kwa usawa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news