WAZIRI MHAGAMA:MAFURIKO YANAONGOZA KWA MADHARA NCHINI

Na Robert Kalokola, Geita

Ikiwa leo Dunia inaadhimisha siku ya maafa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema mafuriko ndiyo yanaongeza hapa nchini kusababisha madhara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Ajira,Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Maafa wilayani Chato,kushoto ni Kanali Jimmy Said ambaye ni Mkurugenzi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).

Amesema kuwa, mafuriko yanasababishwa na baadhi ya wananchi kujenga kiholela na kuzuia mikondo ya maji,wananchi kuishi mabondeni hivyo mvua ikinyesha athari yake inakuwa kubwa.

Jenista Mhagama ameeleza kuwa, ili kupunguza madhara yanayotokana na janga hilo la mafuriko , serikali imeboresha vifaa vya kufuatilia hali ya hewa vinavyotumiwa na mamlaka ya hali ya hewa nchini.

Amesema kuwa, kwa sasa taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) zina uhakika kwa kiwango cha asilimia 87.

Ameongeza kuwa, mradi wa kuboresha vifaa vya mamlaka ya hali ya hewa ulitokana na ushirikiano na taasisi na jumuiya mbalimbali za kimataifa.

Mhagama amefafanua kuwa, serikali inashirikiana na nchi jirani, taasisi za kikanda na kimataifa katika mapambano ya kupunguza madhara yatokanayo na maafa.

Ametaja baadhi ya majanga kuwa ni pamoja na mafuriko,ukame,milipuko ya magonjwa na tetemeko.

Amesema kuwa, serikali imedhamiria kushirikiana na jumuiya za kimataifa, Umoja wa Mataifa katika mapambano ya madhara yanayo tokana na majanga.

Ametaja sera ya taifa 2004 imetambua umuhimu wa mtashirikiana ya kikanda na kimataifa katika usimamizi wa kupunguza madhara ya maafa.

Amesema kuwa, baadhi ya shughuli zimetekelezwa na serikali kwa mashirikiano na mashirika ya kimataifa ikiwa ni kuanzisha maghala katika kanda sita ya kuhifadhi vifaa vya kutumia wakati ambao maaafa yanapotokea.

Mengine ni kuweka mipango ya kukabiliana na maafa katika halmashauri ishirini hapa nchini ambazo zinaongoza kwa maafa mbalimbali kama vile ukame.

Mkurugenzi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Jimmy Said amesema kuwa, mamlaka yake inakutana na changamoto ya wananchi kuwa na uelewa mdogo wa majanga katika maeneo yao.

Ameeleza kuwa, halmashauri hapa nchini zinasaidiwa kujengewa uwezo wa kuweka mipango ya kukabiliana na majanga na madhara katika maeneo yao.
Jenista Mhagama ambaye ni Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu akizungumza. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).

Post a Comment

0 Comments