WAZIRI MKUU AONYA MATUMIZI MABAYA YA TEHAMA

Na Robert Kalokola, Geita

Waziri Mkuu Kassim Majalliwa amewataka vijana nchini kujiepusha na matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuingia katika vitendo vya wizi,utapeli na uchochezi kwa njia ya mitandao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokelewa katika viwanja vya Mazaina wilayani Chato katika MAONESHO ya Wiki ya Vijana. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).

Amesema kuwa,Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mtu atakayejihusisha na vitendo vya uhalifu kwa njia ya TEHAMA na kuwataka vijana nchini kutojiingiza katika mtego huo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongeza kuwa, idadi ya vijana nchini imeongezeka na kufikia asilimia 36 ya watanzania wote na kuwa tegemeo kubwa katika uchumi wa taifa.

Amesema kuwa, Serikali inategemea kundi hilo la vijana katika ubunifu,kuzalisha na kama injini ya uchumi wa taifa kwa kutumia matumizi sahihi ya TEHAMA.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati kushoto) akikagua banda la vijana ofisi ya Waziri Mkuu katika MAONESHO ya Wiki ya Vijana wilayani Chato, mwingine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).

Waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa vijana nchini na kuwataka kutumia TEHAMA kwa matumizi sahihi ya kutengeneza ajira na kuongeza kipato.

Amefafanua kuwa, ili kuakikisha TEHAMA inatumika kwa usahihi serikali imeboresha mifumo ya usimamizi wake kwa kuweka sera,sheria na kanuni mbalimbali za kusimamia matumizi vya sahihi ya TEHAMA kama vile Sheria ya Mitandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Miamala.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa maonesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa vijana.

Amesema kuwa, vijana wamepata fursa ya kutafakari uzalendo,uadilifu na uwajibikaji kama njia ya kuwaenzi waasisi wa taifa letu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Japhet Simeo (kulia) akitoa ufafanuzi wa shughuli za ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (mwenye kipaza sauti kushoto) mwingine ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).

Manufaa mengine amesema kuwa, ni vijana kubadilishana uzoefu,ujuzi,kuongeza fursa za kiuchumi na kupata elimu mbalimbali kama za uzazi wa mpango,mapambano dhidi ya Ukimwi,madawa ya kulevya na ugonjwa wa UVIKO-19.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema kuwa,vijana katika mkoa huo wameshanufaika na asilimia 4 za mikopo ya mapato ya halmashauri na jumla ya milioni 857.3 zimeshatolewa kwa vikundi 132 vyenye wanachama 998.

Ameongeza kuwa, vijana ambao wamenufaika na mikopo hiyo wameshaanza kurejesha mikopo ili iwanufaishe na vijana wengine ambao hawajapata mikopo hiyo.

Maonesho ya Wiki ya Vijana kitaifa yanafanyika wilayani Chato yamefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Oktoba 12,mwaka na yatahitimishwa Oktoba 14, mwaka huu siku ambayo ni kuzima Mwenge wa Uhuru na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news