Yanga SC yazima tambo za KMC FC kwa mabao 2-0

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WANAJANGWANI, Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwalaza wenyeji, wahamiaji mkoani Ruvuma, KMC FC mabao 2-0.
Ni katika mtanange mtamu uliopigwa jioni ya Oktoba 19, 2021 katika dimba la Maji Maji mjini Songea lililopo Mkoa wa Ruvuma.

Awali, Katibu wa Timu ya KMC, Walter Harson alisema, wamejiandaa kushinda katika mchezo huo.

Nyota wa mchezo wa huo ni kiungo wa kimataifa nchini, Feisal Salum Abdallah aliyefunga mabao yote mawili mapema kipindi cha kwanza na kuifanya timu ya kocha, Nasreddine Nabi anayesaidiwa kazi na Mrundi, Cedric Kaze ifikishe pointi tisa baada ya mechi tatu za awali, mbili ikicheza ugenini.

Fei Toto, alifunga bao kwanza dakika ya tano baada ya kufumua shuti kali lililombabatiza mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele kufuatia kudondoshewa mpira na kiungo mwingine, Mkongo Yannick Bangala aliyeuzuia mpira uliookolewa na mchezaji wa KMC.

Mzanzibari huyo akafunga bao la pili dakika ya 12 kwa shuti kali pia la umbali wa mita mita 25 baada ya kutengewa pasi na Mayele.

Post a Comment

0 Comments