Aliyoyasema Rais Samia wakati akihutubia Mkutano wa COP 26

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Novemba 2, 2021 amehutubia mkutano wa wakuu wa nchi wanaoshiriki mkutano wa 26 kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kutoa wito kwa mataifa yote kuwa juhudi za pamoja zinahitajika kwa kuwa athari za mabadiliko hayo hazichagui nchi zilizoendelea au zinazoendelea.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mbalimbali Wanawake katika Mkutano huo maalumu wa COP 26 unaoendelea katika Mji wa Glasgow, Scotland, Novemba 2, 2021. (PICHA NA IKULU).

Mhe. Rais Samia ameeleza namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoiathiri Tanzania katika ardhi ya uzalishaji mali, ongezeko la kina cha bahari, kuyeyuka kwa barafu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, namna ambavyo kisiwa cha Zanzibar kinavyoathirika kwa ongezeko la kiwango cha joto ambalo linaathiri ekolojia inayovutia watalii.

Aidha, ameongeza kuwa athari hizo zinatokea licha ya Serikali ya Tanzania kuendelea na azma yake ya kutenga hekta milioni 48 kwa ajili ya utunzaji wa misitu.

Mhe. Rais Samia ameeleza pia kuwa Serikali ya Tanzania inao mkakati maalum wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambao umeainisha hatua kadhaa za kuchukua ikiwemo kupunguza athari za hewa ukaa kwa asilimia kati ya 30 na 35 ifikapo mwaka 2030.

Mhe. Rais Samia amehimiza nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za kuratibu upatikanaji wa kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 100 kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi hususan kwa nchi zinazoendelea kwa kueleza kuwa athari zikitokea zitawakumba wote, nchi zilizoendelea na zinazoendelea.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia pia ameshiriki na kuzungumza katika mkutano maalum wa viongozi wanawake wanaoshiriki Mkutano wa 26 wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi (COP26) ulioitishwa na Kiongozi wa Serikali ya Scotland, Bi. Nicola Sturgeon.

Mhe. Rais Samia ameelezea namna wanawake duniani na hususan Tanzania wanavyoathirika na mabadiliko ya tabianchi na kutoa wito kwa hatua madhubuti kuchukuliwa ili kuwasaidia wanawake na jamii nzima kwa ujumla. Pia ametoa wito wa kushirikisha wanawake katika utungaji wa sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Mhe. Rais Samia pia ameeleza namna Tanzania ilivyo mstari wa mbele katika kushirikisha wanawake kwenye mapambano ya mabadiliko ya tabianchi na kusema kuwa Tanzania ina mkakati maalumu wa Kitaifa wa Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi tangu mwaka 2013 ambao umekuwa na lengo la kuhakikisha wanawake wameshirikishwa kikamilifu katika eneo la mabadiliko ya tabianchi.

Mara baada ya Mkutano huo, Mhe. Rais Samia pamoja na viongozi wengine Wanawake waliohudhuria mkutano huo wamesaini tamko la pamoja kuhusu kupaza sauti katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news