Dkt.Tulia Ackson akabidhi mabati 500 ujenzi wa mabweni CBE Kampasi ya Mbeya

NA MWANDISHI MAALUM

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson amekabidhi mabati 500 yenye thamani ya shilingi milioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya watoto wa kike kwa Chuo cha Biashara CBE Kampasi ya Mbeya.
Mabati hayo ambayo ni sehemu ya mchango wa kuunga juhudi za Mheshimiwa Dkt.Tulia ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimetoka Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu.

Mheshimiwa Dkt.Tulia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anaendelea kuboresha na kuinua viwango vya miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo mabati hayo yametolewa ili kusaidia kupunguza adha kwa watoto wa kike kukaa mbali na mazingira ya chuo ikiwa ni mkakati wake wa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali ili kuwajengea mazingira bora.
Dkt.Tulia ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na mlezi wa Chuo cha Elimu ya Biashara CBE jijini Mbeya akizungumza wakati akikabidhi mabati hayo kwa uongozi wa chuo alitumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo na kuzitaka taasisi zingine ziige mfano wa benki hiyo.
Amesema kuwa,mchango huo utaongeza ari na hamasa kwa watoto wa kike kusoma kwa bidii huku wakiishi katika mazingira rafiki ya chuo badala ya kupanga jambo ambalo litawapunguzia vishawishi nje ya masomo yao.


"Msaada huu ni mkubwa utasaidia kukamilisha kuezeka hosteli zote,tunawaomba wadau walioahidi waendelee kutoa msaada tunapokea kitu chochote kinachohusu ujenzi,’’amesema Mheshimiwa Tulia.

Dkt. Tulia amesisitiza wadau waendelee kuchangia kutokana umuhimu wake kwa watoto wa kike hususan kutokana na mtazamo tofauti kwa kupigiwa mfano Rais aliyeko madarakani ambaye ni mwanamke na kuwa mtoto wa kike akiendelea kulindwa anaweza kuwa kiongozi mkubwa.
‘’Nimelipa umuhimu mkubwa tukio hili kwa kuja mwenyewe huku Bunge likiendelea mjini Dodoma,mimi ni mlezi wa chuo hiki,tuendeleze juhudi hizi yeyote mwenye mchango wake nitamfuata aliko ili aendelee kutusapoti kwenye jambo hili,’’amesema.

Awali Meneja wa NMB Kanda Nyanda za Juu, Straton Chilongola amesema, benki hiyo imeshiriki kuchangia ikiwa ni sehemu ya mchango unaotokana na faida yake kuchangia huduma za kijamii kwenye sekta ya elimu.
Naye Mkurugenzi wa CBE Kampasi ya Mbeya, Tumaini Jeremiah amemshukuru Dkt.Tulia kutokana na ushawishi na hamasa yake kubwa ambayo imesababisha Benki ya NMB kutoa sapoti hiyo ambapo amezitaka taasisi zingine kuiga mfano huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news