Iramba kukabidhi vyumba vya madarasa 61 kabla ya Desemba 5, 2021

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

HALMASHAURI ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida inatarajia kukabidhi jumla ya vyumba vya madarasa 61 ambavyo ni miradi ya elimu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.89 iliyojengwa kwa kutumia fedha za UVIKO-19 ifikapo Desemba 5, 2021.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 30, 2021 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo  Michael Matomora alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Kyengege Kata ya Kyengege.

Aidha, amebainisha kwamba miradi yote imefikia hatua ya kupauliwa na tayari wasafirishaji wapo Dar es Salaam kuchukua mabati.
"Tunatarajia ndani ya siku mbili au tatu yatakuwa yamefika katika maeneo ya kazi, hivyo ni imani yetu kwamba mpaka tarehe tano tutakuwa tumemaliza kupaua kwa sababu tumeshanunua kila kitu,"amesema Matomora.
Mkurungezi huyo amebainisha kwamba katika miradi hiyo 47 ni ya ujenzi wa madarasa katika Shule za Sekondari 19 ambazo zitagharimu kiasi cha sh.Milioni 940.

Aidha, Mkurugenzi huyo ameeleza kwamba miradi 14 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 14 katika shule shikizi saba (7) ambazo ni Ulongo, Magugu, Kagera, Itunda, Masunkune, Kisingu na Ibambasi ambazo zitagharimu kiasi cha sh.milioni 280.

Amesema, kwa ujumla shule ambazo zinatekeleza miradi ya UVIKO-19 katika wilaya ya Iramba ni Lulumba, New Kiomboi, Kinambeu, Shelui, Kyengege, Kizaga, Kidaru, Mbelekese na Mtekente. Nyingine ni Mtoa, Tulya, Ntwike, Urughu, Ushora, Kinampanda, Mukulu, Mgongo, Kaselya na Kisiriri. alifafanua Matomora.

Akijibu baadhi ya changamoto zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo baadhi ya wakuu wa Shule kutotizimiza majukumu yao vizuri Mkuu wa Mkoa, Dkt. Mahenge amesema Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote wa Serikali atakaye sababisha uzembe katika utekelezaji wa miradi hiyo.

"Yeyote atakayefanya uzembe wa makusudi tutamchukulia hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hizo, lengo likiwa sio kumkomoa bali ni kwa ajili ya manufaa ya jamii husika,"amesema Dkt.Mahenge.

Hata hivyo, RC Mahenge amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Iramba kwa jitihada zao katika kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo ambapo mpaka sasa madarasa yote yamefikia hatua ya kupaliwa.

Aidha, RC Mahenge amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba pamoja na viongozi wa CCM kuendelea kusimamia kazi hizo na kuhakikisha kwamba inakamilika kabla au ndani ya Desemba 5, 2021.

Awali Suleiman Mwenda akimkaribisha Mkuu wa mkoa alisema wilaya inatekeleza miradi 47 ya ujenzi wa madarasa katika shule 19 ambapo jumla ya madarasa 18 yamefikia hatua kupauliwa katika shule saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news