Jangwani wamwangukia Naibu Waziri wa Ardhi Dkt. Mabula

NA MUNIR SHEMWETA, WANMM

Baadhi ya wakazi wa Jangwani jijini Dar es Salaam wamemuaomba Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi, Dkt.Angeline Mabula kusaidia Mwekezaji kupatiwa eneo la Jangwani ili waweze kulipwa fidia na kupisha eneo hilo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akipita baadhi ya maeneo katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam alipokwenda kusikiliza changamoto za wakazi wa eneo hilo wanaotaka eneo la Jangwani kupatiwa Mwekezaji.

Wakazi hao waliwasilisha ombi hilo kwa Naibu Waziri Dkt.Mabula alipotembelea eneo la Jangwani kujionea mazingira ya eneo hilo kama ni salama kwa uwekezaji sambamba na mipango ya mamlaka husika kuhusiana na eneo hilo.

Kampuni ya Jangwani Holding Ltd imeomba kuwekeza sehemu katika eneo la Jangwani na kukubali kuwalipa fidia wakazi wanaoishi hilo. 
 
Hata hivyo, uamuzi wa kutoa eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji unasubiri ushirikishwaji wa mamlaka husika ambazo ni Ofisi ya Makamu wa Rais idara ya Mazingira, Halmashauri ya Jiji la Ilala pamoja na Mradi wa Uendelezaji jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Wakizungumza katika eneo hilo juzi wakazi hao walisema, wanachohitaji kwa sasa ni Mwekezaji kupatiwa sehemu ya eneo la Bonde la Jangwani ili nao waweze kuwalipwa fidia na kwenda kutafuta maeneo mengine ya kuishi.
Salehe Selemani Cheyo ambaye ni Mjumbe wa Mtaa wa Msimbazi Bondeni, akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula wakati Naibu Waziri alipokwenda kusikiliza changamoto za wakazi wa Jangwani jijini Dar es Salaam wanaotaka eneo hilo apatiwe Mwekezaji ili awalipe fidia.

Kwa mujibu wa wakazi hao, eneo hilo limekuwa na changamoto ya mafuriko kwa muda mrefu na juhudi za awali za serikali kuwapatia maeneo wananchi Mabwepande wilaya ya Kinondoni halikudhi wakazi wote kwa kuwa walipatiwa viwanja walikuwa 43 kati ya 1,200.

‘’Imekuja kampuni inataka kutuhamisha hapa na itulipe fidia, lakini mamlaka husika hazijaridhia huku halmashauri ya jiji ikishindwa hata kuweka vibao kuonesha kuwa eneo hili ni eneo hatarishi na maeneo yamewekwa vifusi na kuendelea na shughuli kama kawaida,’’amesema mwananchi mmoja.

Walisema kwa sasa wako hoi bila kujua hatma yao na kuomba Mwekezaji kupewa eneo ili waondoke kwenda kutafuta sehemu nyingine za kuishi kwa kuwa baadhi ya nyumba zao zimeharibika.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akisisitiza jambo wakati wa kikao na watendaji wa sekta ya ardhi, Mradi wa Uendelezaji jiji la Dar es Salaam (DMDP) na wawakilishi wa Kampuni ya Jangwani Holding Ltd baada ya kumaliza ziara ya kutembelea eneo la Jangwani Dar es Salaam alipokwenda kusikiliza changamoto za wakazi wa eneo hilo wanaotaka eneo la Jangwani kupatiwa Mwekezaji.

Salehe Selemani Cheyo aliyejitambulisha kama Mjumbe wa Mtaa wa Msimbazi Bondeni alisema, kiu kubwa ya wakazi wa eneo la Jangwani ni kuona mwekezaji anapatiwa eneo hilo ili waweze kulipwa fidia na kudai kuwa kinachowashangaza ni kuelezwa eneo hilo ni atarishi wakati limekuwa likipatiwa huduma mbalimbali kama vile maji na umeme na wananchi wamekuwa wakilipia huduma hizo.

‘’Tunaambiwa eneo hili ni hatariishi wakati watu tuna leseni za makazi na tumekuwa tukilipa kodi za majengo na nyumba zipo mpaka Sambusa, kwanini hatarishi wakati pesa za wananchi wanachukua? Alihoji Cheyo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula aliwaomba wakazi wa eneo hilo kuwa na subira wakati serikali ikilifanyia kazi suala hilo kwa kuwa kuna mamlaka na mipango tofauti kuhusiana na eneo hilo ambapo serikali lazima zijiridhishe kama uwekezaji hautakuwa na madhara sambamba mipango ya uendelezaji.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kabla ya uamuzi kufanyika lazima baadhi ya mamlaka zishirikishwe ili maamuzi yatakayotolewa yawe na tija na mamlaka hizo ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais idara ya Mazingira, Halmashauri ya Jiji la Ilala pamoja na kujua Mradi wa Uendelezaji jiji la Dar es Salaam (DMDP) unasemaje kuhusiana na eneo hilo.

‘’Mambo yakienda vizuri watawekeza lazima mvute subira na kilichonileta hapa ni kujiridhisha eneo ni salama, je liko katika mpango ganoi na wahusika wamejiridhisa? Maana hatuwezi kupitisha leo halafu kesho kunatokea maafa, naomba muwe na subira,’’ alisema Naibu Waziri Dkt.Mabula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news