Kampuni ya CNOOC yasaini Mkataba wa Wanahisa wa EACOP

*Hatua hii itawezesha Kampuni ya Mradi kuundwa

NA MWANDISHI MAALUM

Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya China (CNOOC) ambayo ni mmoja kati ya wanahisa wanne wanaotekeleza mradi wa EACOP, ametia saini mkataba wa wanahisa (Shareholders Agreement) leo Novemba 4, 2021 hatua inayofungua ukurasa mpya wa kuanzisha Kampuni maalumu ya Mradi (EACOP Company) ambayo ndio itatekeleza na kuendesha mradi wa EACOP. 

Wanahisa wengine wa mradi wa EACOP ni pamoja na TPDC (15%), Kampuni ya Taifa ya Mafuta Uganda (UNOC-15%), Total Energies (62%) na CNOOC (8%).
Rais wa Kampuni ya CNOOC, Ndg. Chen Zhubiao (wapili kutoka kulia waliokaa) akitia saini Mkataba wa Wanahisa wa mradi wa EACOP huku wanahisa wengine wakishuhudia, kutoka kulia waliokaa ni Mkurugenzi kutoka UNOC Ndg. Francis Nagimesi, Mkurugenzi Mtendaji wa TOTAL EACOP, Ndg. Martin Tiffen, na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio. Wengine waliosimama ni watumishi kutoka TPDC, UNOC na CNOOC.

Akizungumza mara baada ya tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. James Mataragio amesema leo hii tumeshuhudia hatua nyingine kubwa katika mradi wa EACOP ambapo mmoja ya mwanahisa mwenzetu, "CNOOC amesaini mkataba wa wanahisa na hivyo kuwezesha uanzishwaji wa kampuni ya mradi ambayo ndio itakuwa na jukumu la kutekeleza, kusimamia na kuendesha mradi wa EACOP,"amesema. 

Dkt. Mataragio ameeleza kuwa wanahisa wengine wa mradi waliweka sahihi mikataba yote ikiwemo wa wanahisa mnamo Aprili 11, 2021 lakini kampuni ya CNOOC ilihitaji muda zaidi kukamilisha taratibu za kupata idhini kutoka katika Serikali yao kabla ya kusaini mkataba wa wanahisa.

Mkataba huo umetiwa saini na Rais wa Kampuni ya CNOOC, Ndg. Chen Zhuobiao na kushuhudiwa na Wakurugenzi Watendaji kutoka kampuni wanahisa wengine pamoja na wawakilishi wao. 

Akizungumza baada ya kutia sahihi mkataba huo, Ndg. Chen amesema, "tunaelewa ni kwa kiasi gani hatua hii ilikuwa ikisubiriwa na tunayofuraha kwamba Serikali yetu imetoa idhini kwa CNOOC kuwa mwanahisa katika mradi wa EACOP na hivyo kuwahakikishia wanahisa wengine juu ya utayari wa CNOOC kuendelea kama timu moja katika kufikia malengo makubwa ya mradi wa EACOP kwa manufaa ya watu wa nchi zetu,"amesema.
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Azizi P. Mlima ( wa kwanza kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wanahisa wa EACOP baada ya kampuni ya CNOOC kutia saini mkataba wa wanahisa. Wengine pichani waliokaa baada ya Balozi ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa TOTAL EACOP, Ndg. Martin Tiffen, Rais wa CNOOC, Ndg. Chen Zhubiao na Mkurugenzi kutoka UNOC, Ndg. Francis Nagimesi. Waliosimama kuanzia kushoto ni Mratibu wa Mradi wa EACOP Tanzania, Ndg. Asiad Mrutu, Kaimu Meneja Uthamini na Ufuatiliaji TPDC, Ndg. Safiel Msovu, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria TPDC, Dkt. Elias Mwashiuya, Mkaguzi wa Ndani TPDC, Ndg. Msaada E. Athumani na Afisa Rasilimali watu TPDC, Ndg. Danford Luambano

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP, Ndg. Martin Tiffen alieleza furaha aliyonayo kufuatia kampuni ya CNOOC kusaini mkataba wa wanahisa. 

Ndg. Tiffen amesema, "tumekuwa tukiweka malengo kila mwaka ya kufikia maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investment Decision) na kwa kampuni ya CNOOC kusaini mkataba huu leo ni wazi sasa kuwa mradi wa EACOP umekamilisha hatua ya kuwa na wanahisa na hivyo kuanzisha kampuni ya EACOP ambayo sasa itachukua majukumu ya kutekeleza mradi ambayo yamekuwa yakitekelezwa na TOTAL Energies kwa niaba ya wanahisa wengine,"amesema.

Kwa upande wa Tanzania, mradi huu umepiga hatua mbalimbali zikiwemo ulipaji wa fidia kwa watu 351 katika maeneo ya awali, kukamilika kwa uthamini na uhakiki wa watu 9,122 katika mkuza wa mradi ambapo malipo yanatarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa, kukamilika kwa tathmini ya athari za mazingira na stadi za kijiolojia, kijiofizikia na kijiotekniki katika maeneo ya bahari pamoja na kusainiwa kwa mikataba yote muhimu ya mradi.

Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa kilomita 1,443 (kati ya hizo kilomita 1,147 ziko nchini Tanzania) za bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda kupitia Tanzania hadi Bandari ya Tanga kwa lengo la kuuza mafuta hayo katika soko la Kimataifa. 

Kwa upande wa Tanzania bomba hili litapita katika mikoa nane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. 

Vile vile mradi wa EACOP utahusisha ujenzi wa miundombinu mingine nchini Tanzania ambayo ni pamoja na; vituo vinne (4) vyenye pampu kwa ajili kusukuma mafuta; vituo viwili (2) vya kupunguza kasi ya msukumo wa mafuta;kituo cha kuhifadhia mafuta takribani mapipa milioni 2; Gati lenye urefu wa kilomita 2 kutoka kwenye kituo cha kuhifadhi mafuta kuelekea kituo cha kupakia Mafuta; Valvu 53 kwenye maeneo muhimu kwa ajili ya kuzuia au kuruhusu utiririkaji wa Mafuta; Vituo vidogo 15 vya umeme kwa ajili ya kupasha joto bomba; Kilomita 107 za barabara mpya na zilizoboreshwa na kambi kumi na mbili (12) za ujenzi wa Mradi. 

Kazi zote hizi zitatoa fursa za ajira kwa watanzania ambapo inatarajiwa ajira 10,000 hadi 16,000 zitazalishwa katika kipindi cha hadi miaka minne ya utekelezaji wa mradi, mapato kwa serikali, fursa za Watanzania kutoa huduma kwa zile huduma zilizotengwa mahususi kwa ajili ya Watanzania na faida nyingine nyingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news