Madini ya Tanzania yaivutia Iran, Prof.Masanjila abainisha walivyojipanga masoko ya Kimataifa

ASTERIA MUHOZYA NA ABUBAKARI KAFUMBA, UAE

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amesema Serikali ya Tanzania imejipanga vizuri kutafuta masoko na kuuza mazao yake kwa nchi nyingine zinazoshiriki na kutembelea Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Expo 2020 Dubai ambapo inawakilishwa na Sekta mbalimbali ikiwemo ya Madini.
Prof. Msanjila ameongeza kuwa, katika maonesho hayo, Tanzania inalenga kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na kupatikana nchini ambazo zinazotokana na Sekta za Madini, Utalii, Kilimo, Mifugo na sekta nyingine.

‘’Suala la pili tumekuja hapa tukilenga kuuza bidhaa zetu pamoja na kuiuza miradi yetu mikubwa ya maendeleo kwa wawekezaji na kuwahakikishia kuwa wanaweza kuwekeza bila matatizo kwa sababu miundombinu wezeshi ipo,’’amesema Prof. Msanjila.

Ameyasema hayo Novemba 3, 2021 baada ya kutembelea eneo hilo la maonesho ikiwemo banda la nchi ya Irani ili kuona namna nchi hiyo inavyofanya shughuli za uchimbaji madini. Katika ziara hiyo ya kutembelea banda la Irani, Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila aliongozanana na Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai Balozi Mohamed Abdallah Mtonga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dunstan Kitandula, Mkurugenzi wa Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwase, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini Bw. Augustine Olal, na Kaimu Meneja wa Uwekezaji na Mipango kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Bi. Nsalu Nzowa, Kamishana Msaidizi wa Madini Uendelezaji wachimbaji Wadogo Bw. Francis Mihayo na Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Arusha Mhandisi Aidan Mhando.
Akizungumzia namna Taasisi za Madini zilivyojipanga kushiriki ameainisha kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lipo kwa ajili ya kutangaza miradi yake inayotekelezwa na inayopangwa kutekelezwa ikiwemo kutafuta wabia katika uwekezaji kutokana na shirika hilo kuiwakilisha S erikali katika miradi ya madini.

Kuhusu ushiriki wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini inashiriki kwa lengo la kuwawezesha wawekezaji kujua aina za madini zinazopatikana nchini na maeneo ya uwekezaji na kwa upande wa Tume ya Madini ipo katika maonesho hayo kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji kupata taarifa kutoka katika vyanzo sahihi kuhusu namna ya kupata maeneo ya kufanya shughuli za uchimbaji, kuwaunganisha wawekezaji na wachimbaji wadogo wa madini, wawekezaji kupata taarifa zinazohusu biashara ya madini na taratibu zake ikiwemo Sheria na taratibu zinazosimamia uwekezaji katika sekta ya madini.

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali wa banda la Tanzania kwenye maonesho hayo Balozi Mohamed Abdallah Mtonga, ameongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea banda la nchi ya Irani ili kupata uzoefu wa namna nchi hiyo inavyosimamia shughuli za madini.

Akizungumza na ujumbe huo, Meneja wa Biashara wa Kampuni ya Irani Mine House, Sadegk Rokni amesema amefurahishwa na ujumbe wa Tanzania kutembelea banda hilo na kuelezea matamanio ya Iran kuwekeza katika Sekta ya Madini nchini kutokana na utajiri wa ralisimali madini zilizopo Tanzania.

“Tunavutiwa kuwekeza Tanzania kwani ni nchi yenye madini mengi. Sisi tuna takriban aina 70 tu za madini na hakika hatuwezi kulingana na ninyi kwa kwa namna mlivyobarikiwa. Kikubwa tunatamani kujua taratibu za kisheria za uwekezaji,’’ amesema.

Awali, akitoa taarifa za mwenendo wa Tanzania kushiriki katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade amesema jumla ya nchi 192 zinashiriki maonesho hayo ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitano ambapo mataifa yanayoshiriki yanapata fursa ya kujitangaza kujifunza, kupata uzoefu, kutafuta masoko ya bidhaa zao, wawekezaji, wabia na mambo mengine ambayo yanawezesha kukuza sekta muhimu za kiuchumi na maendeleo.

Sekta ya madini Tanzania ni miongoni mwa sekta zinayopewa kipaumbele katika maonesho hayo kutokana kuwa na fursa za kiuwekezaji na biashara ilizonazo kuanzia kwenye masuala ya uongezaji thamani madini, biashara ya madini, uchimbaji madini huku sehemu kubwa ya utajiri huo ikiwa bado haijaguswa.

Kutokana na muktadha huo, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kufanya jitihada za kuhamasisha wawekezaji kupitia njia mbalimbali za kimataifa na kitaifa ikiwemo maonesho hayo ya Expo 2020 Dubai yanayoendelea huku Tanzania ikishiriki kupitia eneo la Mobility lenye kaulimbiu ndogo isemayo‘’ Connectivity, Tanzania Ready for Take Off’’.

Mbali na Taasisi za Serikali kushiriki maonesho hayo, pia Tanzania inawakilishwa na Sekta Binafsi. Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 1 Oktoba, 2021 yanatarajiwa kuhitimishwa mwezi Machi, 2022.

Post a Comment

0 Comments