Mfumo, waajiri watajwa kuwa kikwazo mafao ya wastaafu nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI imetaja mabadiliko ya mfumo wa kiutendaji na baadhi ya waajiri kuchelewa kulipa fedha za wanachama wao kuwa sababu za kuchelewa kulipwa kwa mafao ya wastaafu.
Sarafu na noti za fedha halali za Tanzania. (Picha na BoT).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama ameyasema hayo Novemba 23, 2021 wakati akielezea mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara jijini Dodoma.

Mheshimiwa Waziri Mhagama amesema, mabadiliko ya kimfumo kwenye utendaji yamepepekea baadhi ya wastaafu kuchelewa kulipwa mafao na stahiki zao kwani Serikali imekuwa ikifanya mapitio kwa ajili ya kujiridhisha.

Amesema, mfumo uliopo umetengenezwa kumaliza changamoto hizo, lakini kwa kuwa zilishakuwepo awali ndiyo maana baadhi wanacheleweshwa.

“Ni kweli kwamba bado kuna changamoto katika malipo ya wastaafu, lakini tatizo ni mfumo na kwa baadhi ya halmashauri wanachelewesha kulipa fedha za wanachama wao,”amesema.

Kuhusu madeni amekiri kuwa mifuko bado inaidai Serikali ambapo PSSF pekee wanaidai Serikali shilingi trilioni 4.6 ambapo baadhi ya madeni yametokana na mfumo wa zamani ambapo wafanyakazi hawakuwa wakikatwa fedha zao lakini walipostaafu ilibidi walipwe tu.

Mheshimiwa Waziri amesema, deni hilo kwa ujumla wake limetokana na malipo ya wastaafu ambao hawakuwa wakichangia katika mifuko, fedha ambazo amedai Rais Samia Suluhu Hassan ameshaagiza zaidi ya shilingi trilioni mbili zilipwe kwa mtindo wa hati fungani.

Post a Comment

0 Comments