Mheshimiwa Silinde amshukuru Rais Samia kwa kuipa uzito Sekta ya Elimu nchini

NA MWANDISHI MAALUM,OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa David Silinde amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 604.75 kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Elimu nchini.

Mheshimiwa Silinde ameyasema hayo leo Novemba 29, 2021 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suhusu Hassan na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika hafla ya makabidhiano ya Shule ya Msingi Museveni iliyopo Chato mkoani Geita.
"Tunashuku kwa kutualikwa kushiriki kwenye makabidhiano ya Shule ya Msingi Museveni ambayo itafundisha kwa mtaala wa Kiingereza na imejengwa na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni. Shule hii ya Museveni itaenda kuleta mabadiliko makubwa katika Mkoa wa Geita na hususani Halmashauri ya Wilaya ya Chato, kwani itaweza kupokea wanafunzi ambao watajifunza masomo yao kwa kutumia lugha ya Kiingereza.

"Pia Mheshimiwa Rais Samia tunakupongeza kwa kutoa fedha Shilingi Bilioni 604.75 katika kipindi cha kutoka Aprili hadi sasa kwa ajili ya kuendelea kuimarisha utekelezaji wa utoaji wa elimu bora kwenye Sekta ya Elimumsingi kama ifuatavyo:

i. Kiasi cha shilingi Bilioni 151 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa Sera ya Elimumsingi bila ada. Aidha, kiasi cha fedha ambacho hutolewa kwa kila mwezi kimeongezeka kutoka Bilioni 21 hadi kufikia Bilioni 26,

ii. Fedha shilingi bilioni 304 kupitia mpango wa mapambano na ustawi wa maendeleo dhidi ya COVID-19 zimepokewa ambapo Shilingi Bilioni 240 zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 12,000 ambavyo vitatumika kwa mapokezi ya Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 2022 na Shilingi Bilioni 60 kwa ajili ya ujenzi vyumba vya madarasa 3,000 kwenye vituo shikizi 907 na Shilingi Bilioni 4 zimeelekezwa kujenga mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mhe Rais tunakuahidi kabla ya tarehe 15 Disemba,2021 tutakua tumekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000 na watoto wote wataanza kidato cha kwanza kwa msimu mmoja.

iii. Kupitia Programu ya GPE – LANES II na EP4R Shilingi Bilioni 113 zimeelekezwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari. Aidha kupitia programu hizo, ujenzi wa shule mpya za msingi 19 na sekondari 15 umefanyika kwa gharama ya shilingi Bilioni 21.25;

iv. Fedha za tozo shilingi bilioni 7 zimepelekwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya madarasa 560 ya Shule za Sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuunga mkono jitihada hizo;

v. Fedha za kuzuia maambukizi na athari za UVIKO-19 Shilingi Bilioni 8.5 zimeelekezwa kwenda kujenga miundombinu ya kunawia mikono,

Matokeo ya juhudi zako hizo katika kuimarisha Elimumsingi, napenda kukujulisha kuwa wanafunzi wote 907,802 waliofaulu Mtihani wa Kuhitimu Darasa la Saba mwaka 2021 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2022.

"Ni imani yangu kwamba Serikali yako ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu nchini kwa kujenga miundiombinu mipya ya elimu kwa maana ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni, mabwalo ya chakula, maabara, maktaba pamoja na matundu ya vyoo.

"Natoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni kwa kutujengea shule hii ambayo inakwenda kufundisha masomo kwa Mtaala wa Kiingereza na kuweka historia katika Mkoa wa Geita hususan Halmashauri ya Wilaya ya Chato. Sisi katika elimu wafadhili kwetu sio wafadhili tu bali ni marafiki na ndugu zetu.

"Ofisi ya Rais-TAMISEMI tayari imetoa maelekezo kwa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita kusimamia utekelezaji wa kazi zilizobaki kwa wakati zikiwemo ununuzi wa samani za majengo yote, uchimbaji kisima cha kuvunia maji, utengenezaji wa mitaro ya maji, njia za miguu (walk ways) na ujenzi wa mabweni mawili. Kiasi cha Shilingi Milioni 705 tayari kimepokewa na Halmashauri ya Wilaya ya Chato.

"Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu na uongozi wote tunapenda kukuhakikishia kuwa tutasimamia uendeshaji wa Shule ya Msingi Museveni kwa kuhakikisha upatikanaji wa watumisi na vifaa vya kutosha kwa wakati ili iweza kuleta mafanikio yaliyokusudiwa,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Silinde.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news