Miaka 60 ya Uhuru: Mifugo na Uvuvi yajivunia mafanikio lukuki

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imetaja mafanikio ambayo imeyapata katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara huku ikiendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Uvuvi kwa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya kuboresha sera, sheria, kanuni na taratibu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mashimba Ndaki ameyasema hayo leo Novemba 25, 2021 wakati akizungumzia mafanikio ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara jijini Dodoma.

Amesema kuwa, wizara hiyo imeanzisha Dawati la Sekta Binafsi kwa ajili ya kutoa elimu, kuwaunganisha wadau wa uvuvi na taasisi za kifedha ili kuwawezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu.

“Mazingira hayo yamehamasisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya uvuvi, ikiwemo uvuvi wa kibiashara, viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi na kutengeneza zana za uvuvi,"amesema Waziri Ndaki.

Pia Mheshimiwa Ndaki amesema, wizara yake itahakikisha kuwa, Sekta ya Mifugo inaendeshwa kibiashara ili kuleta tija kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla hapa nchini.

Waziri amesema, Sekta ya Uvuvi ni miongoni mwa sekta za uzalishaji mali ambayo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo ya usimamizi na uratibu wa uendeshaji wa shughuli za uvuvi nchini.

“Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara wizara yangu itaendelea kuhakikisha kuwa, sekta ya mifugo inaendeshwa kibiashara ili kuleta tija kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla,”amesema Mheshimiwa Waziri.
Pia amesema, wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi ili kukuza na kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi kwa kasi zaidi, chini ya uongozi mahiri wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Kuhusu nyama na maziwa

Waziri Ndaki amesema, Watanzania wamekuwa na changamoto ya kula nyama na kunywa maziwa ambapo amedai kwa mwaka mtu mmoja anatakiwa kula nyama kilo 50 na maziwa lita 200.

Aidha, kiwango cha ulaji wa samaki kwa sasa ni kilo 8.5 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na kiwango kinachopendekezwa na Shirika na Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) cha kilo 20.3 kwa mtu kwa mwaka.

Kuhusu malisho kwa wafugaji

Mheshimiwa Waziri Ndaki amesema, Serikali imetenga maeneo kwa ajili ya walisho ya wafugaji hasa katika kipindi cha kiangazi lengo likiwa ni kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.

Ubora wa nyama

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Ndaki amesema, nyama ya Tanzania ina ubora na ndio maana imekuwa ikinunuliwa na nchi nyingi kutokana na ubora huo huku akizitaja nchi ambazo zimekuwa zikinunua nyama ya Tanzania kuwa ni Oman,Kuwait,Qatar,Vietnam na nyingine.

Kuhusu rasilimali za uvuvi

Waziri Ndaki amesema, Tanzania ilianza juhudi za kulinda na kudhibiti rasilimali za uvuvi tangu ilipotunga sheria ya kwanza ya uvuvi iliyoitwa ‘Fisheries Ordinance and Trout Protection Ordinance CAP 368’.

Amesema, tangu nchi yetu ipate Uhuru, juhudi mbalimbali zimefanyika ili kuwezesha usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi zikiwemo kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali, kuanzisha kanda nne na vituo 35 vya doria.

Bandari ya Uvuvi

Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki amesema, wizara inaendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kupitia Mtaalam Mwelekezi ambaye ni Kampuni ya M/S Sering Ingegneria ya nchini Italia kwa gharama ya shilingi bilioni 1.421.

Pia amesema, Serikali tayari imechagua eneo la Kilwa Masoko kwa ajili ya kujenga bandari ya uvuvi ambayo kukamilika kwake italeta matokeo makubwa katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Waziri amesema, katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bandari hiyo mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.

Aidha, jitahada za kutafuta wawekezaji wa kujenga miundombinu mingine ya uvuvi katika eneo hilo zinaendelea vizuri.

Changamoto

Mheshimiwa Waziri Ndaki amesema, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) imefanya tathmini ya mahitaji ya samaki nchini ambapo makadirio ni tani 750,000 kwa mwaka ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 496,390, sawa na upungufu wa tani 253,615.

Juhudi zinazoendelea za kuongeza uzalishaji wa samaki nchini zitaongeza ulaji wa samaki kwa watanzania kufikia kilo 10.5 ifikapo mwaka 2026.

Aidha, ili kukidhi mahitaji ya samaki nchini na kuongeza kiwango cha ulaji wa samaki, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina matarajio ya baadaye kuimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kujenga na kukarabati mialo, masoko na kuboresha teknolojia za uhifadhi ili kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 baada ya kuvunwa.

Sambamba na kuhamasisha teknolojia sahihi za uvuvi na matumizi ya zana bora kwa wavuvi wadogo kutoka vyombo 13,593 vinavyotumia injini hadi vyombo 25,000 kwa ajili ya shughuli hiyo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news