Miaka 60 ya Uhuru: Wizara ya Elimu yarekodi mafanikio ya kihistoria, Serikali yatoa fursa kwa wanafunzi wanaopata mimba kuendelea na masomo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha mtoto wa kike anamaliza elimu ya msingi, hivyo imetoa fursa ya kuendelea na masomo kwa wasichana ambao wanapata ujauzito wakiwa katika shule za msingi au sekondari.

Pia wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu baada ya kujifungua.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 baada ya Uhuru wa Tanzania Bara katika sekta ya elimu nchini.

Profesa Ndalichako amesema,Serikali itatoa nafasi kwa wanafunzi hao kuendelea na masomo kutokana na takwimu kuonyesha kuwa watoto wanaacha shule kwa sababu mbalimbali.

“Takwimu za elimu zinaonyesha kwamba wanafunzi wanaacha shule kutokana na sababu mbalimbali ukiwemo utoro, ujauzito, utovu wa nidhamu,lakini sababu kubwa ni utoro ambapo wanafunzi wa shule za msingi ni takribani 108 ambapo asilimia takriban 93 ni watoro na asilimia 5 wanaacha shule.

“Lakini tumesema hata hawa asilimia tano wanaocha shule kwa sababu ya utoro pengine wanaweza kuwa na sababu ya msingi ya utoro wao,inawezekana kuna changamoto za kifamilia zikiwemo za kiuchumi,kuuguliwa,kuhama maeneo.

“Lakini Serikali imesema yule atakayekamilisha kutatua changamoto zilizokuwa zikimkabili anaweza kurudi shule ndani ya miaka miwili tangu alipoacha shule,”amesema.

Akizungumzia kuhusu wanafunzi wa darasa la saba wanaoshindwa mtihani kwa sababu mbalimbali alisema,wanafunzi hao sasa wanapewa nafasi ya kurudia mitihani yao kwani huenda waliacha shule kwa sababu za msingi.

“Kwa waliomaliza darasa la saba na kushindwa mtihani kwa namna yoyote ile ikiwemo kufutiwa matokeo wataruhusiwa kufanya mtihani wa marudio,"amesema.

Profesa Ndalichako amesema, utaratibu wa wananfunzi hao kurudia mtihani utawekwa na Baraza la Mitihani huku akisema, wanafunzi watakaorudia mtihani ambao watafaulu mtihani huo watapata fursa ya kuchaguliwa katika shule mbalimbali hapa nchini kujiunga na shule za sekondari.

Hatua hiyo ni kuzingatia kwamba wanafunzi wa kidato cha nne na sita wanapata fursa, kwa hiyo serikali imeona iwapatie fursa na wanafunzi wa darasa la saba ambao bado ni wadogo.

Ametoa wito kwa wasimamizi wa mitihani wazingatie sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa kwani Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaojihusisha na wizi wa mitihani kwa namna moja ama nyingine.

Aidha, Profesa Ndalichako amesema,mwelekeo wa Sekta ya Elimu baada ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara ni kuendelea kutoa elimu bora itakayoipatia jamii maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

“Serikali itachukua hatua zifuatazo ili kuimarisha elimu na kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa elimu ikiwemo kuhakikisha kwamba inaboresha mitaala ya elimu katika ngazi zote na kuweka msisitizo zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sayansi, Ujasiliamali, Stadi za kazi na masuala mtambuka,"amesema.

“Fani za kimkakati kama vile uhandisi, kilimo, udaktari zitendelea kupewa kipaumbele,Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuendelea kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume ambapo kazi hii inafanyika kwa kasi zaidi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo sambamba na ujenzi wa madarasa 15,000 unaoendelea nchini Serikali inatarajia kujenga shule 1,000 za sekondari za kutwa na shule za sekondari 26 za wasichana katika kipindi cha miaka mitano ijayo,"amesema.

Amesema,tayari utekelezaji umeanza kwa shule 274 za kutwa na shule 10 za wasichana ambapo Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 1,405 mwezi huu.

Pia amesema, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi itaendelea kuimarishwa ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika wilaya 29 nchini.

Amesema, lengo ni kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa ambapo kwa msingi huo, mafunzo kwa vitendo yatapewa uzito stahiki sambamba na kuimarisha ushirikiano na viwanda ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.

Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako, Serikali itaendelea kuimarisha elimu maalum kwa kuhakikisha miundombinu inayojengwa ni rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

“Pia Serikali itaendelea kununua vifaa visaidizi ili kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kujifunza kwa ufanisi zaidi, Serikali itaendelea kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa fursa za elimu,"amesema.

Kuhusu mafanikio ya sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 baada ya Uhuru wa Tanzania Bara amesema,mafanikio haya yametokana na kazi iliyotukuka iliyofanywa na serikali kwa awamu zote sita pamoja na wadau mbalimbali wenye nia njema na elimu ya Tanzania.

Kuhusu elimu ya msingi na sekondari

Amesema,katika elimu ya msingi na sekondari, baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule za msingi zilizosajiliwa kutoka shule 3,270 mwaka 1961 hadi shule 18,546 mwaka 2021.

“Kati ya shule 18,546, shule 16,656 ni za Serikali na 1,890 za binafsi,shule za sekondari zimeongezeka kutoka 41 mwaka 1961 ambapo shule 2 zilikuwa za binafsi, hadi kufikia 5,460 mwaka 2021 ambapo shule 3,983 ni za Serikali na shule 1,287 ni za binafsi.

“Takwimu hizi zinaonesha wazi namna ambavyo baada ya kupata Uhuru, Serikali imetoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi kushiriki katika elimu ambapo hali hii imewezesha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya sekondari kuongezeka kutoka wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 4,432 mwaka 1961 hadi wanafunzi 803,085 mwaka 2021.

“Ongezeko hilo limechangiwa na mikakati mbalimbali ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila Malipo ulioanza kutekelezwa 2016 chini ya Serikali ya Awamu ya Tano na unaendelea kutekelezwa,“amesema.

Pia amesema,ujenzi wa shule za sekondari za kata uliofanyika kuanzia mwaka 2005 na unaendelea kufanyika hadi sasa umewezesha elimu ya sekondari kutolewa karibu na wanaposhi wanafunzi.

Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako,Serikali ya Awamu Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendeleza kwa vitendo upatikanaji wa fursa za elimu ya sekondari kwa wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

“Katika kipindi cha miezi 14 nane tu tangu aliposhika hatamu ya uongozi wa nchi yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya sekondari 12,000 na kazi hiyo inaendelea,”amesema.

Pia amesema, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuchukua hatua mahususi za kuongeza idadi ya shule za kidato cha tano na sita ili kuongeza fursa zaidi kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Elimu Maalum

Amesema, elimu ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania bila kujali mazingira yake ambapo Sera za Elimu zimekuwa zikisisitiza juu ya umuhimu wa elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo baadhi ya mafanikio yalipatikana ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule za msingi zinazochukua wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka shule nne za Wamisionari (Tabora, Buigiri, Irente na Uhuru Mchanganyiko) mwaka 1961 hadi kufikia shule 776 mwaka 2021.

“Shule za sekondari zimeongezeka kutoka shule moja (Mpwapwa sekondari) mwaka 1960 hadi kufikia shule 74 mwaka 2021,kuongezeka kwa vyuo vikuu vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka Chuo Kikuu kimoja cha Dar es Salaam mwaka 1961 hadi vyuo vikuu 11 mwaka 2021,"amesema.

Amesema, ongezeko hilo limetoa fursa kwa wanafunzi kuchagua vyuo na fani wanazotaka kusomea,kuanzishwa kwa Mafunzo ya Elimu Maalum mwaka 1976 ambapo Wizara ya Elimu ilianza kuandaa walimu kwa wanafunzi Wasioona na Viziwi katika Chuo cha Ualimu Tabora.

Aidha amesema,mwaka 1983 Chuo cha Ualimu Tabora kilianza kuandaa walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili.

Waziri Ndalichako amesema,mwaka 1996 Chuo cha Ualimu wa Elimu Maalumu Patandi kilianza kutoa kozi mbalimbali za elimu maalumu.

Katika hatua nyingine amesema ufundishaji wa lugha ya alama umeimarishwa ili kuwawezesha watoto viziwi kujifunza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news