Mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi ulivyorejesha umoja na mshikamano Zanzibar

NA RAJAB MKASABA

SUALA la umoja katika jamii ni jambo lenye umuhimu mkubwa na ambalo limesisitizwa katika vitabu vyote vye dini.

Umoja ni jambo ambalo limekuwa likihimizwa sana katika maisha ya mwanadamu hasa ikizingatiwa kwamba umoja ndio nguzo kubwa ya maendeleo popote pale duniani.

Hatua hiyo ndio inayompelekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake kulipa kipaumbele suala hili na kila anapopata nafasi na kutana na wananchi ama viongozi wenzake wa aina zote wa ndani na nje ya nchi amekuwa akilisisitiza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akila kiapo cha kuiongoza Zanzibar kwa Awamu ya 8 kuanzia mwaka 2020-2025 katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.

Katika kuuendeleza umoja na kuuimarisha zaidi katika jamii hapa Zanzibar, Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kwa kuwaungaisha wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuimarisha udugu wao walionao ambao ulitishia kusambaratika kwa kutokana na itikadi za kisiasa.

Mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha hatua hiyo yameweza kuungwa mkono na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa ndani na nje ya nchi wa dini na serikali pamoja na wananchi kwa ujumla.

Rais Dkt. Hussein Mwinyi amekuwa akiwasisitiza wananchi wa Zanzibar kuimarisha amani na umoja kwa lengo la kuiletea nchi maendeleo jambo ambalo limemjengea sifa kubwa kwani hiyo ndio kiu ya wananchi ya muda mrefu.

Kiongozi huyu anaamini kwamba Wazanzibari wote ni wamoja hivyo, ni vyema wakauendeleza umoja na amani waliyonayo sambamba na kuendelea kuwajibika ili kuiletea nchi maendeleo endelevu.

Amekuwa akisisitiza kuwa Zanzibar wana kila sababu ya kuungana pamoja katika kuendeleza amani na umoja uliopo pamoja na kuchapa kazi kwa azma ya kuiletea nchi maendeleo..

“Leo katika nchi yetu tuna amani na umoja hayo ni mambo makubwa na baada ya hapo maendeleo yatapatikana tu Inshaalllah kwa sababu sote sasa ni wamoja na kilichobaki watu wafanye kazi na kila mtu awajibike, maendeleo yatapatikana tu Inshalla”, kauli hiii aliitoa Rais Dkt. Mwinyi wakati alipokuwa akiwasalimia waaumini wa Kiislamu wa msikiti wa Mfereji wa wima mnamo Machi 3, mwaka huu wa 2021.

Aidha, alisema kuwa hivi sasa Zanzibar imejaa amani na umoja hivyo matumaini makubwa ya kupatikana kwa maendeleo yapo kwani wananchi wote wa Zanzibar ni wamoja na kilichobaki ni kufanya kazi na kuwajibika.

Rais Dk. Hussein Mwinyi ambaye alishinda Urais wa Zanzibar amekuwa akizungumzia maridhiano tangu aapishwe mnamo Novemba 2, mwaka 2020 ambapo katika hotuba yake baada ya kuapishwa alitaja umuhimu wa maridhiano katika kuijenga Zanzibar mpya.

Katika kiapo hicho Rais Dkt. Mwinyi aliapa kwamba atailinda na kuiongoza nchi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Katiba inayoonesha katika Kifungu chake cha 9 (3) ambayo inaelekeza kwamba “Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa umoja wa kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia,” mwisho wa nukuu.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi aliweza kurudia kauli yake hiyo wakati akilihutubia Baraza la Wawakilishi pale aliposema “Ninaheshimu maridhiano na matakwa ya Kikatiba ya kushirikiana na vyama vingine vya siasa katika kuendesha Serikali na niko tayari kuyatekeleza maridhiano kama katiba ya Zanzibar inavyoeleza,”alisema Rais Dkt.Mwinyi.

Mnamo Disemba 8, mwaka 2020 katika hafla ya kumuapisha Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba “Katika kuyaendeleza na kuyastawisha maridhiano, uko wajibu wa viongozi, uko wajibu wa vyama vya siasa na uko wajibu wa wananchi na jamii kwa jumla mimi naahidi, nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuyajenga na kuyadumisha maridhiano kwa maslahi mapana ya nchi yetu, yale yaliyo ndani ya mamlaka kwa uwezo wangu nitayatekeleza bila ya kigugumizi wala ajizi”.

Aliendelea kueleza kwamba, “Sisi viongozi kila wakati hatuna budi kuzingatia na tufahamu kwamba maslahi ya wananchi ndio jambo la msingi. Tofauti zetu, kama ndogo au kubwa,zisiwe kikwazo cha maendeleo ya wananchi na nchi yetu kwa jumla. Katiba ya Zanzibar imeeleza kwamba ‘Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe’, Bila ya shaka tumeweza kufikia hatua hiyo kwa sababu tunauelewa huo wa kikatiba”.

“Nasaha zangu kwa wananchi, ni kwamba sote tuwe kitu kimoja na tuunge mkono juhudi hizi zenye lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa”.

Mbali ya matakwa ya kisheria, umoja ni imani pia, umoja ni vitendo kama anavyoendelea kufanya Dk. Mwinyi katika kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane pamoja na kuwaongoza wananchi wake wote wa Zanzibar waliomchagua na waliokuwa hawakumchagua.
Pichani aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Pombe Magufuli (katikati) akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi (kushoto) na aliyekuwa Makamo wa Kwaza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad (kulia) walipokutana Ikulu Chato mkoani Geita mnamo Januari 14,2021.

Rais Dk. Mwinyi amekuwa akisisitiza kwamba maridhiano ya wkeli yanajengwa wka mambo makuu matatu likiwemo dhamira, ambapo pande zote mbili zilizotofautiana ni lazima kuwa na udhati katika kufanikisha na kuedneleza maelewano baina yao. Aidha, maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana na kuwa endelevu iwapo wahusika na wadau wote hawana dhamira ya kweli ya kufikia, kufanikisha na kuendeleza maridhiano hayo.

Jambo la pili ambalo Rais Dk. Mwinyi amekuwa akilisisitiza katika maridhiano ni kuvumiliana, kustahamiliana na kusahau yaliyopita ambapo jambo la tatu ni kujenga utamaduni wa kuaminiana, ambapo maridhiano yoyote hayawezi kudumu iwapo pande mbili zitakuwa haziaminiani.

Mbali na hayo, Rais Dk. Mwinyi amekuwa akiwapongeza viongozi wa dini zote hapa nchini kwa kuhubiri amani wakati wote wa uchaguzi mkuu na kupelekea zoezi hilo kwenda vizuri na hatimae kuleta mafanikio makubwa ambapo pia, utamaduni hao wamekuwa wakiuendeleza hadi hivi leo.

Amekuwa akieleza kwamba maendeleo ya nchi yoyote hayawezi kupatikana kama umoja na amani havipo na kusisitiza kwamba baada ya uchaguzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeundwa kwa lengo la kuleta umoja hasa katika kuleta maendeleo kwani kuwepo kwa maendeleo ni lazima watu wote waungane na kuwa wamoja.

Anaeleza kwamba Serikali ya Umoa wa Kitaifa imeundwa kwa lengo la kuleta umoja hasa katika kuleta maendeleo kwani kuwepo kwa maendeleo ni lazima watu wote waungane na kuwa wamoja.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi anasisitiza kwamba umefika wakati wa kujenga nchi na wananchi wote kwua kitu kimoja na kuondokana na malumbano ya kisiasa na badala yake kuendelea na kazi moja ya kuiletea nchi maendeleo endelevu.

Mnamo Juni 06,2021 Rais Dk. Miwnyi alikutana na kufanya amzungumzo na viongozi mbali mbali wa dini wakiwemo viongozi wa dini ya Kiislamu wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih pamoja na viongozi wa dini ya Kikristo wakiongozwa na Askofu Dickson Kaganga, Katibu wa Umoja wa dini mbali mbali Zanzibar na kuwapongeza kwa utayari wao wa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba viongozi wa dini pamoja na viongozi wa Serikali wanapaswa kuwa kitu kimoja katika kuendeleza na kuimarisha masuala ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.

Nao viongozi hao wa dini walieleza jinsi walivyofarajika na hatua za makusudi anazozichukua Rais Dk. Mwinyi katika kuhamasisha amani, umoja na mshikamano huku wakisisitiza haja kwa viongozi wengine wa Serikali kufuata nyayo zake.

Sambamba na hayo, viongozi hao walieleza jinsi hatua za makusudi zilizochukuliwa na Rais Dk. Miwnyi mara tu baada ya kuingia madarakani za kuhakiksiha anawaweka wananchi kuwa kitu kimoja na kuondosha ubaguzi wa aina zote.

Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania ukiongozwa na Sheikh Abdallah Ndauga mnamo Agosti 18,2021 walikutana na kufanya amzungumzo na Rais Dk. Miwnyi ambapo miongoni mwa mazungumzo yao, viongozi hao walimpongeza Rais kwa hekima yake ya kuirejesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imerejesha mshikamano, upendo na ushirikiano kwa kiwango kikubwa na hivyo kuurahisishia uongozi wake kuyafikia malengo ya kimaendeleo iliyoyaweka kwa urahisi zaidi.

“Sisi Hay-atul Ulamaa, tunaamini uamuzi wako huu uliouchukua utakubakiza katika kumbukumbu za Wazanzibari na Watanzania kiujumla hata baada ya kumalizika kwa kipindi chako cha uongozi kwa Zanzibar”,alisema sehemu ya risala ya umoja huo iliyosomwa na Sheikh Abdallah Swaleh Ndauga.

Wageni mbali mbali waliohudhuria katika Mkutano wa Pili wa Amani uliofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort mnamo Januari 16, 2021 walimpongeza Rais Dk. Mwinyi na kueleza mataraji yao ya mafanikio kwa Zanzibar kutoka na kiongozi huyo kulivalia njuga suala la umoja katika Serikali yake anayoiongoza ikiwa ni pamoja na kuiendeleza na kuisimamia Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news