NACTE yafanya maamuzi magumu kuhusu mitihani ya utabibu

NA DOREEN ALOYCE

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limefuta matokeo ya mitihani ya nadharia kwa masomo yote ya programu ya utabibu ngazi ya tano (NTA Level 5).
Mganga, Mkuu wa serikali Dkt. Aifello Sichalwe amebainisha hayo jijini Dodoma wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kuvuja kwa mitihani ya utabibu.

Amesema, hatua imefikiwa baada ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa kuwasilisha taarifa ambayo imethibitisha kuwapo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya vyuo vilivyochunguzwa kupitia namba za simu za wanafunzi.

“Mtihani wa muhula wa pili kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ilifanyika kitaifa kuanzia tarehe 16 Agosti, 2021 hadi Septemba 30, 2021 siku ya mwisho ya ufanyaji wa mitihani ya nadharia wizara ilipokea taarifa ya kuwapo kwa viashiria vya kuvuja kwa mitihani hiyo.

“Hivyo kulazimika kuunda kamati ya uchunguzi iliyojumuisha wataalamu kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama,”amesema Dkt, Sichalwe

Amesema, kamati hiyo imefanya uchunguzi kuanzia Septemba 6, 2021 hadi Oktoba 17, 2021 ilipowasilisha taarifa ya awali katika uchunguzi huo.

“Kamati imebaini kwamba mitihani ya mwaka wa pili (NTA LEVEL 5) ya progaramu ya utabibu ilivuja, lakini mitihani ya programu zingine zote haikuvuja,”amesema.

Aidha, amesema wakati wa uchunguzi kamati ilibaini mitihani hiyo ilisambazwa kupitia mitandao ya kijamii na kuonekana kwenye baadhi ya namba za simu za wanafunzi.

Kadhalika, amesema wanafunzi hao walipohojiwa walikiri kupata mitihani hiyo kupitia makundi ya mitandao ya kijamii yaliyoanzishwa na wanafunzi hao kwa ajili ya kujadiliana.

“Kamati ya uchunguzi imewasailisha taarifa ya uchunguzi ambayo imethibitisha kuwapo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya vyuo vilivyochunguzwa kupitia namba ya simu za wanafunzi, uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watu, vyuo, taasisi zingine zilizo jihusisha na udanganyifu huo,”amesema.

Vilevile, amesema taarifa ya uchunguzi huo iliwasilishwa kwenye Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Oktoba 24, 2021 kwa ajili ya maamuzi kwani ndicho chombo cha kisheria chenye mamlaka na vyuo vya elimu ya kati nchini.

“Wizara imesikitishwa na tukio hilo na itaendelea kutoa ushirikianao kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kukamilisha uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki kufanya udanganyifu,”amesisitiza.

Dkt.Sichalwe amewataka wanafunzi wa vyuo kuzingatia masomo na kutoajihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu kwani vina madhara makubwa kwao na kwa jamii.

“Mtaalamu wa afya alijipatia sifa kwa njia ya udanganyifu ni hatari kwa afya za wananchi, tunaomba wananchi waendelee kuwa watulivu na waiamini serikali yao kuwa ipo makini na itatumia jitihada zote kulinda usalama wao,”alisisitiza Dkt, Sichalwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news