PWANI YATENGA BILIONI 3.4/- KUWAWEZESHA WALEMAVU

NA ROTARY HAULE

MKOA wa Pwani umetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 3.4 katika bajeti yake ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya kutoa mikopo ya kuwezesha makundi ya watu mbalimbali wakiwemo walemavu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Hajjat Mwanasha Tumbo ametoa kauli hiyo wakati akifungua kongamano la viongozi na wanachama wa Chama cha Wasioona Tanzania lililofanyika Mjini Kibaha.

Hajjat Tumbo amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo bega kwa bega katika kushirikiana na Chama cha Wasioona pamoja na vyama vingine vya watu wenye ulemavu ili waweze kufikia malengo ya kimaendeleo.

Amesema kuwa,kutokana na umuhimu wa jamii ya watu wenye ulemavu Mkoa wa Pwani tayari umetenga fedha hizo na walemavu wamepangiwa asilimia mbili ya fedha hizo.

Amesema,watu wenye ulemavu wamekuwa waaminifu na waadilifu katika kurejesha mikopo na ndio maana kwa sasa hata namna ya utoaji mikopo yao imebadilika kutoka kundi la watu wengi na kufikia mtu mmoja.

"Sisi Pwani tunawapa kipaumbele kikubwa kwa watu wenye ulemavu hususani wale wasioona na tayari tumetenga bilioni 3.4 kwa mwaka wa fedha 2021/22 na Kati ya hizo walemavu wametengewa asilimia mbili kwahiyo tutashirikiana nanyi muda wowote,"amesema Hajjat Tumbo.

Aidha,Mhandisi Tumbo amewasisitiza watu wenye ulemavu wa wasioona kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuchanja chanjo ya Uviko -19 ili kujiweka sehemu salama dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa, Rais wa Awamu ya Sita anafanya kazi kubwa kwa ajili ya kuokoa wananchi wake ndio maana amepigania kupata chanjo ya Uviko -19 ,hivyo ni vyema wakamuunga mkono katika utekelezaji wake.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Tumbo amewakumbusha viongozi na wanachama hao kujitokeza katika kushiriki zoezi la sensa itakayofanyika hapo mwakani kwa lengo la kuleta maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tanzania, Omari Sultan amesema kuwa, kongamano hilo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe yatakayofanyika kitaifa Novemba 4,2021 Mjini Kibaha.

Amesema kuwa,Fimbo Nyeupe inasaidia kumtambulisha mtu asiyeona ,chombo cha kusaidia kutambua vikwazo kwa mtu asiyeona na hata alama za barabarani huku akisema anaishukuru Serikali kwa hatua kubwa ya kuwawezesha walemavu hao kwa kupata mikopo kirahisi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mhandisi Mshamu Munde amesema kuwa Halmashauri yake inaendelea kutoa kipaumbele kwa kujenga miundombinu rafiki kwa walemavu.

Munde,amesema pamoja na kujenga miundombinu hiyo lakini bado Halmashauri inahakikisha walemavu wanapata mikopo kwa wakati kwakuwa ndio watu pekee ambao wamekuwa na sifa ya kurejesha mikopo kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments