Rais Dkt.Mwinyi afanya ziara ya kushtukiza vyanzo vya maji, atoa maagizo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha changamoto iliyojitokeza ya ukosefu wa maji kwa baadhi ya maeneo ya Mji wa Zanzibar inapatiwa ufumbuzi wa haraka ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo ipasavyo.

Dkt.Mwinyi ametoa agizo hilo Novemba 25, 2021 wakati alipotembelea na kukagua vyanzo vya Mradi wa Maji unaopeleka huduma hiyo Mjini Zanzibar ambapo miundombinu yake imeharibika na kusababisha kukosekana kwa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Zanzibar kwa takribani siku nne sasa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo kwa watendaji wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwa kutembelea visima vya maji safi na salama Bumbwisudi Wilaya ya Magharibi "A" Mkoa Mjini Magharibi, katikati) ni Waziri wa Maji,Nishati na Madini, Mhe.Suleiman Masoud Makame, wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi "A", Mhe.Suzan Peter Kunambi. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi amewataka watendaji wa ZAWA kuongeza kasi katika utatuzi wa changamoto za maji zinazoukabili mji, akibainisha matumaini yake baada ya baadhi ya vifaa, ikiwemo mabomba kuwasili.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutengeneza mfumo utakaowawezesha wananchi wa maeneo ya Miwani, Kizimbani na Bumbwisudi kupata huduma za maji kupitia Mradi wa Maji Safi na Salama unaopeleka huduma hiyo Mjini Zanzibar.

Amesema, kuna umuhimu wa ZAWA kuandaa mfumo maalum kutoka kisima kimoja miongoni mwa visima saba vilivyopo, ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma hiyo ya maji.
Amesema, mradi huo wakati unaanzishwa haukuzingatia mahitaji ya wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka vyanzo hivyo, na hivyo kuwafanya kukosa kabisa huduma hiyo.

Aidha, amesema Serikali hivi sasa ina mpango wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na umeme, hivyo akawahakikishia wananchi wa maeneo hayo kuwa Serikali itashughulikia chanagmoto zinazowakabili.

Dkt.Mwinyi amewataka wananchi hao kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki cha kiangazi, sambamba na kuwataka kumuomba Mwenyezi Mungu ili awaletee neema ya mvua na kuendeleza kilimo mashambani.

Vile vile, amewashukuru Mafundi wa ZAWA kwa kufanikiwa kurejesha mfumo uliosababisha kuunguka kwa mabomba na kusababisha ukosefu huo wa maji.

Mapema, Mkurugenzi wa ZAWA, Dkt. Salha Mohamed Kassim amesema, kazi kubwa zinazofanywa na mamlaka hiyo zinahitaji gharama kubwa na kubainisha mpango maalum ulioandaliwa wa kulipa madeni, ikiwemo ya walinzi wa kiraia kwenye visima vya maji.
Mlinzi katika visima vya Mamlaka ya Maji Safi na Salama (ZAWA), Bw.Hussein Ismail akitoa changamoto zinazowakabili katika kazi zao wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alipofika maeneo ya visima vya maji safi na salama vya ZAWA Bumbwisudi Wilaya ya Magharibi "A" Mkoa wa Mjini Magharibi kuangalia tatizo lililopelekea kukosekana kwa huduma hiyo. (Picha na Ikulu).

Amewahakikishia wananchi hao kuwa wale wote wanaoidai mamlaka hiyo watapatiwa haki zao hivi karibuni.

Nao, baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na vyanzo hivyo, walionyesha masikitiko yao kwa kukosa huduma za maji safi na salama kwa kipindi chote tangu mradi huo unaopeleka maji Mjini kuanzishwa, ingawa vyanzo vya huduma hiyo inapatikana katika maeneo yao.

Aidha, walilalamika kuwepo kwa barabara mbovu kuelekea katika Shehiya zao pamoja na ukosefu wa huduma za umeme changamoto ambazo Rais Dkt.Mwinyi aliwahakikishia kwamba zitapatiwa ufumbuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news