Rais Dkt.Mwinyi: UWT ina mchango mkubwa kwa CCM

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), una mchango mkubwa katika kukiendeleza na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania UWT ulipofika Ikulu Jijini Zanzibar kusalimiana nae (katikati) Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa Bibi Gaudentia Kabaka na Makamu wake Thwaiba Adington Kisasi.

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Novemba 21, 2021 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) uliofika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza sambamba na kumtambulisha Katibu Mkuu mpya wa Umoja huo, Bi Phillis Nyimbi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) umekuwa ukishiriki vyema katika kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaendelea kushika hatua na kuimarika kwa lengo la kuiletea maendeleo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na watu wake.

Alisema kuwa, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), umekuwa ndio nguzo muhimu katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na imeweza kusaidia katika harakati zote ikiwa ni pamoja na kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushika madaraka katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka jana 2020, ambapo (CCM) ilishinda kwa kishindo.

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuupongeza Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), kwa kuja na wazo la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia, ni Mwenyekiti wa (CCM) Taifa Samia Suluhu Hassan kwa kuandaa mkutano mkubwa hapa Zanzibar uliofanyika jana (20 Novemba 2021) ambao ulifana.

Aliongeza kuwa, mikutano pamoja na makongamano kadhaa ambayo yamekuwa yakifanywa na Umoja huo yamekuwa yakimfariji kwa kiasi kikubwa Rais Samia na kuona kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wanachama, Jumuiya zake pamoja na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaendelea kumuunga mkono.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alimpongeza Katibu Mkuu mpya wa Umoja huo Bi Phillis Nyimbi kwa kushika wadhifa huo na kueleza kwamba anamatumaini makubwa kwamba nafasi hiyo ataifanyia kazi ipasavyo kutokana na kumfahamu utendaji wake wa kazi.

Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mama Gaudentia Kabaka alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza vyema majuku yake ya Urais ambapo amekuwa akifanya vizuri tokea kukabidhiwa wadhifa huo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akizungumza na Mwenyekiti wa wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania Taifa (UWT), Bibi Gaudentia Kabaka ulipofika Ikulu jijini Zanzibar kusalimiana nae akiwa na ujumbe aliofuatana nao (hawapo pichani).

Mama Kabaka alisema kuwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), unafarajika na juhudi kubwa anazozichukua Rais Dk. Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuendelea umoja, amani na mshikamano wa wananchi.

Katika maelezo yake, Mama Kabaka alimuahidi Rais Dk.Mwinyi kwamba Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), utaendelea kumuunga mkono pamoja na kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya chama tawala cha (CCM) katika kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua na kuendelea kupata maendeleo endelevu.

Uongozi huo pia, ulitumia fursa hiyo kumtambulisha Katibu Mkuu wake mpya Bi Phillis Nyimbi kwa Rais Dk. Mwinyi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiwa katika picha na Uongozi wa Jumuiya wa Wanawake Tanzania (UWT) baada ya kusalimiana nao walipofika Ikulu Novemba 21, 2021. (Picha na Ikulu).

Miongoni mwa viongozi wa Umoja huo waliofika Ikulu kwa ajili ya kuzungumza, kumpongeza na kumtambulisha Katibu Mkuu mpya kwa Rais Dkt. Mwinyi ni Mwenyekiti wa (UWT) Mama Gaudentia Kabaka, Makamo wa Mwenyekiti (UWT) Thuwayba Kisasi, Katibu Mkuu wa (UWT) Phillis Nyimbi pamoja na Naibu Katibu wa (UWT) Zanzibar Tunu Juma Kondo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news