Rais Samia arejea nchini, afanya ziara eneo la Coco Beach

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 04 Novemba, 2021 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea Glasgow, Scotland alipokuwa akihudhuria Mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo tarehe 04 Novemba 2021 alipokua akitokea nchini Glasgow, Scotland alikohudhuria mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa uliojadili kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi Duniani.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Aidha, Mhe. Rais Samia amefanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Tanzanite linalojengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amepokea maelezo ya ujenzi wa daraja hilo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Mhandisi Rogatius Mativilla ambaye amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 70.

Mhandisi Mativila amesema daraja hilo litakapokamilika litapunguza msongamano wa magari, ajali bararani, litaboresha hali ya maisha Jijini Dar es Salaam pamoja na kupendezesha jiji la Dar es Salaam na kuwa sehemu moja wapo ya kivutio cha utalii katika fukwe zilizopo karibu na daraja hilo.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amefanya ziara katika eneo la Coco Beach ili kuona agizo lake la kutaka wafanyabiashara wadogowadogo kupangwa vizuri katika mazingira bora ya kufanya biashara linavyoendelea kutekelezwa. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo tarehe 04 Novemba 2021 alipokua akitokea nchini Glasgow, Scotland alikohudhuria mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa uliojadili kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi Duniani.

Aidha, Mhe. Rais amesema ziara hiyo pia imemuwezesha kuona hali halisi ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za Coco beach na kusema kuwa Serikali itaangalia upya namna ya kuzuia athari hizo.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa Serikali itaendelea kuwajali wafanyabiashara wadogo wadogo na kutolea mfano eneo hilo ambalo wafanyabiashara wakubwa walilitaka lakini Serikali ilikataa kwa kujali maslahi ya wafanyabiashara wadogo ili waendelee kukuwa na kujipatia kipato.

Pia, Mhe. Rais amesema Serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 5 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo ambao itabidi kuzirejesha ili kuwezesha wengine kupata mikopo hiyo na kuendeleza biashara zao.

Mhe. Rais Samia amesema zoezi la lengo la kuwapanga wafanyabiashara wadogo wadogo mijini ni zuri ambalo limelenga kuwaboreshea mazingira yao ya biashara, kuweka miji katika hali ya usafi pamoja na kuimarisha usalama.

Vilevile Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango Pamoja na TAMISEMI kuanza mara moja ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo kwasababu tayari Serikali imepata fedha kiasi cha zaidi ya Sh. Bilioni 34 ambapo ujenzi huo utahusisha soko la zamani na kujenga mengine mawili mapya ya kisasa mkabala na soko la zamani la Kariakoo na kujenga soko jingine jipya katika eneo la Jangwani Jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news