Rais Samia ataja sababu za Serikali kuruhusu wanafunzi wote walioacha shule kuendelea

NA MWANDISHI MAALUM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeamua kuruhusu wanafunzi wote walioacha shule kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, sababu za kisheria au walioshindwa kufaulu darasa la saba kupewa nafasi nyingine ya kuendelea na masomo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakikagua baadhi ya majengo ya shule hiyo ya Awali na Msingi iliyojengwa kwa msaada wa Rais Yoweri Museveni Chato mkoani Geita mara baada ya kuizindua rasmi shule hiyo Novemba 29, 2021. (Picha na Ikulu).

Amesema, lengo la maamuzi hayo ya Serikali ni kutoa fursa pana kwa watoto wa kitanzania kuweza kuendelea na elimu ili iweze kuwasaidia katika maisha.

Mhe. Rais Samia amesema hayo Novemba 29, 2021 katika hafla ya makabidhiano ya Shule ya Awali na Msingi Museveni iliyokabidhiwa kwakwe na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, katika kijiji cha Nyabilezi, Chato mkoani Geita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kwa pamoja wakikata utepe kuzindua rasmi Shule ya Awali na Msingi Museveni Pre & Primary School iliyojengwa kwa msaada wa Rais Yoweri Museveni Wilayani Chato mkoani Geita.(Picha na Ikulu).

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kwa wanafunzi watakaoshindwa kuendelea na mfumo wa masomo wa kawaida wanaweza kujiunga na Elimu Mbadala ambayo itawezesha kujitegemea kimaisha kwa kuwa inatoa stadi mbalimbali za maisha kama ilivyo katika baadhi ya nchi.
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni akimkabidhi mfano wa funguo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kama ishara ya makabidhiano ya Shule hiyo ya Awali mara baada ya uzinduzi uliofanyika katika Shule hiyo ya Museveni Pre & Primary School Chato mkoani Geita. (Picha na Ikulu).

Pia, Mhe. Rais Samia amesema makabidhiano ya Shule hiyo iliyogharimu jumla ya Dola za Marekani Milioni 1.67, yamefanyika wakati muafaka ambapo itaongeza fursa kwa wanafunzi wote kupata elimu hata kwa wale wenye mahitaji maalum.

Mhe. Rais Samia amemshukuru Rais Museveni kwa wema na utu wake na kujitoa kuhakikisha kuwa elimu bora sio suala la mipaka ila ni jukumu la viongozi wote wa Afrika katika kusaidia bara letu kutoa elimu bora na yenye viwango ili kuweza kukidhi soko la ajira.
Mhe. Rais Samia ameongeza kuwa jukumu hilo kwa viongozi wa Afrika litasaidia bara letu kutoa elimu bora na yenye viwango ili kuweza kukidhi soko la ajira.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema majengo ya shule hiyo yatabaki kama alama ya kipekee katika kumbukumbu za watanzania na wanachato kwa ujumla na ndio maana Serikali ikaamua kuisajili shule hiyo kwa jina la Mhe. Rais Museveni na itajulikana kama Shule ya Msingi Museveni na itafundisha kwa mtaala wa Kingereza.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amewataka wanafunzi watakaopata nafasi ya kujiunga na Shule hiyo kutumia fursa wanayoipata kujifunza kwa bidii ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao na elimu watakayoipata iweze kuwasaidia katika maisha yao ya baadae.

Katika kuenzi mchango wa Rais Museveni na Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuweka historia ya Marais hao kwenye Maktaba yake ili kusaidia wanafunzi watakaosoma shuleni hapo kujifunza uzalendo, umajumui na falsafa za Marais hao ili kuhakikisha waafrika wanajitegemea kwenye sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni amesema, uamuzi wa kujenga Shule hiyo sio kwasababu Serikali ya Tanzania haina fedha bali ni kutokana na udugu, uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Uganda.

Serikali ya Tanzania imetoa Shilingi milioni 705,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa samani na ukamilishaji wa kazi za nje ambazo hazikuwa sehemu ya mkataba wa ujenzi wa Shule hiyo na inatarajiwa kuchukua wanafunzi 630 wa Bweni itakapokamilika.

Shule hiyo ya Awali na Msingi ina vyumba vya madarasa ya Shule ya Msingi 17, Maktaba 1, vyumba vya madarasa ya Elimu ya Awali 3, Jengo la Utawala 1, Ofisi kwa ajili ya Elimu ya Awali 2, Matundu ya vyoo 37 na Nyumba ya Walimu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika Uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita, baada ya Rais Museveni kukamilisha ziara yake ya Kitaifa ya Kiserikali hapa nchini. (Picha na Ikulu).

Mhe. Rais Museveni amemaliza ziara yake ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini ambapo ameagwa rasmi na Mhe. Rais Samia katika Uwanja wa Ndege wa Geita uliopo wilayani Chato mkoani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news