Rais Samia atoa maagizo Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amezindua Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kuhusu matumizi ya barabara na madaraja pamoja na kuvuka katika maeneo hayo kutoka kwa watoto wa shule mbalimbali mkoani Arusha alipotembelea mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika Novemba 23, 2021 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, wa pili kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro.

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo Novemba 23, 2021 huku akisisitiza kuwa, jukumu la usalama barabarani sio la askari wa barabarani peke yao bali ni la kila mwananchi katika jamii na hivyo kumtaka kila mwananchi kuwa makini na kuhakikisha matumizi sahihi ya barabara.

Aidha, Mheshimiwa Rais Samia amesema suala la usalama barabarani lipewe uzito wa kuwa ajenda ya kitaifa katika majukwaa pamoja na kuwahusisha kikamilifu washirika wa maendeleo hasa wale ambao wamepiga hatua kubwa katika maendeleo ya nyanja ya usalama barabarani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyoanza Novemba 23, 2021 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Mhe. Rais Samia amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa ajali za barabarani bado zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania wengi mbali na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwekeza kwenye miundombinu bora ya barabara. 

Pia Rais amesema vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya taifa wamekuwa wahanga wakubwa wa ajali za barabarani ambapo asilimia kubwa za ajali hizo husababishwa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizunguza na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. George Simbachawene (kushoto), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Khamis Hamza Chillo na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro baada ya kufungua maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika Novemba 23, 2021 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. 

Rais Samia amesema, takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano jumla ya wapanda pikipiki 2,220 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na kusababisha majeruhi 4,202.  

Aidha, Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuwa na msaada kwa wananchi na sio kero kwao ili kujenga mahusiano mazuri katika jamii hali itakayopelekea kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali kwa wakati.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akikabidhi jumla ya pikipiki 26 kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwa ajili ya kuongeza kasi ya kufanya doria kwa jeshi hilo, kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama yalioanza Novemba 23, 2021 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Khamis Hamza Chillo.

Ametaja baadhi ya kero zinazofanywa na askari wa usalama barabarani kuwa ni pamoja na kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu, kulazimisha madereva kulipa faini za papo kwa papo kinyume na ilivyo Sheria ya Usalama Barabarani, hivyo kuwataka wahusika kubadilika mara moja. 

Wakati huo huo, Rais Samia ameliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikianana na vyuo vikuu, vyuo vya ufundi na Chuo cha Usafirishaji (NIT) kuwekeza katika utafiti wa suala la usalama barabarani ili kupata suluhu ya kisayansi na kimfumo ya namna ya kupunguza ajali za barabarani.
Viongozi pamoja na wananchi mbalimbali wa mkoa wa Arusha wakiwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuhudhuria Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani iliyoanza Novemba 23,2021. 

Aidha, Rais Samia amelitaka Baraza la Usalama Barabarani kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu ya usalama barabarani kwasababu kwa hivi sasa dunia ni ya kidijitali na taarifa nyingi zipo kiganjani ambapo vijana wengi hutumia mitandao hiyo.

Pia, Mhe. Rais Samia ameelekeza kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa magari kabla ya kutoa stika za usalama barabarani na kutaka Taasisi zinazohusika kukaa na wadau na Sekta binafsi kujadiliana jinsi ya kuendesha zoezi hilo kwa pamoja kwa kutumia vifaa vya kisasa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akisisitiza jambo kwa makamanda wa Jeshi la Polisi alipotembelea mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyoanza leo tarehe Novemba 23, 2021 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene. (PICHA ZOTE NA IKULU).

Katika Maadhimisho hayo ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, Mhe. Rais Samia amekabidhi vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani vilivyotolewa na wadau mbalimbali. Pia, Mhe. Rais alitembelea mabanda mbalimbali pamoja na kupata maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na wadau mbalimbali kuhusu usalama barabarani.

Post a Comment

0 Comments