Rais Samia azindua hoteli ya kisasa ya nyota tano Arusha

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefungua Hoteli ya Gran Melia yenye hadhi ya Nyota Tano iliyopo jijini Arusha.
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha leo Novemba 22, 2021. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Uwekezaji wa AlBwarddy, Ali AlBwardy, wa pili kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Damas Ndumbaro.(Picha zote na Ikulu).

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa hoteli hiyo leo Novemba 22, 2021, Mhe. Rais Samia amemshukuru Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Hoteli hiyo, Bw. Ali Saeed Albwardy kwa uamuzi wake wa kuwekeza nchini kwa kujenga hoteli hiyo ambayo ni moja ya hoteli zenye hadhi kubwa duniani.

Mheshimiwa Rais amesema, uwekezaji huo ni ishara ya kuwepo kwa mazingira bora ya utalii nchini na kuwa uzinduzi wa hoteli hiyo utaiweka Tanzania katika ramani za Hoteli za Gran MeliĆ”, ambapo duniani zipo 350 katika nchi 40.

Ameeleza kuwa, vivutio vya watalii nchini vimekuwa vikitambuliwa kimataifa ambapo Tanzania ilitajwa na tovuti ya SafariBookings.com kuwa sehemu salama ya kufikia Afrika ambapo Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa miongoni mwa hifadhi zilizopendekezwa katika orodha ya maajabu Saba ya Afrika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akivuta kamba kuondoa kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha leo Novemba 22, 2021.

Pia, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania imetajwa na majarida ya New York Times na Lonely Planet kama sehemu bora za kutembelea na Bonde la Ngorongoro kutajwa na mtandao wa Fox News.com kama moja ya Bonde linalovutia duniani na jarida la The World Travel Award kuitaja Serengeti kama Mbuga ya Wanyama inayoongoza Afrika.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa Uchumi wa Utalii kwa nchi yetu hivyo inafanya jitihada kuimarisha mazingira ya kibiashara kwa kuendeleza na kuboresha miundombinu ikiwemo barabara, reli, anga na usafiri wa maji ili kuweka mazingira mazuri kwa utalii na kuwezesha uwekezaji.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa, kutokana na dunia kukumbwa na UVIKO 19 mwezi Desemba, 2019 nchi nyingi ikiwemo Tanzania zilichukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na ugonjwa huo lakini hata hivyo uliathiri safari za kimataifa pamoja na sekta ya utalii na uchumi.

Mhe. Rais Samia amesema katika kuhakikisha sekta ya utalii inakidhi matakwa ya kujikinga na UVIKO 19, Serikali kupitia Mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Baraza la Kusafiri na Utalii Duniani (WTTC) zilianzisha utaratibu wa viwango vya Kitaifa vya Uendeshaji ili kuzuia maambukizi ya UVIKO 19 katika shughuli zinazohusiana na utalii nchini.

Utekelezaji wa utaratibu huo uliwezesha Tanzania kutunukiwa Muhuri wa Usafiri Salama na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache ambazo zinaendelea kupokea watalii hata kipindi cha janga la UVIKO 19.

Kwa upande mwingine Mhe. Rais Samia amesema kwa kuwa Utalii una athari chanya na unagusa kila sekta ya uchumi hivyo ni matarajio yake kuwa Hoteli ya Gran Melia itakuwa na mchango katika kutokomeza umasikini kwa wakulima na wavuvi kwa kutumia bidhaa za vyakula na vinywaji vinavyozalishwa nchini Tanzania.

Mhe. Rais Samia amezitaka Hoteli zote hapa nchini kudumisha utamduni wa kitanzania kwa kuandaa vyakula vyenye asili ya kitanzania katika migahawa ya Hoteli hizo.

Post a Comment

0 Comments