SABABU ZA KUDHIBITI MIONZI KWENYE MNYORORO WA BIDHAA ZABAINISHWA

NA MWANDISHI MAALUM

MKUU wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Peter Ngamilo amesema, kuna sababu nyingi na faida za kudhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kwa kuwa matumizi ya bidhaa zenye viasili vya mionzi ni hatari kwa afya.
Ameyasema hayo akiwa katika Tamasha la Mawasiliano, Utalii, Utamaduni na Maonesho ya Biashara yanayofanyika kwenye viwanja vya Malamala Igoma Jijini Mwanza wakati akielezea sababu za kudhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa.

Ngamilo amesema, TAEC wamejizatiti katika udhibiti wa matumizi salama ya mionzi na uhamasishaji wa uendelezaji wa teknolojia ya nyuklia hapa nchini.

"Hapa tunatoa elimu hiyo,kwa sababu wananchi walio wengi wamekuwa na shauku ya kujua kwa nini tunadhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa,"amesema.
Amesema, mionzi ina faida nyingii kwani inachangia mambo makubwa katika ustawi wa jamii ambapo utumika katika sekta mbalimbali kama vile Sekta ya Afya.

Amesema, katika sekta hiyo huwa inatumika katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali, kwenye Sekta ya Kilimo mionzi huwa inatumika katika kutafuta au upatikanaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali na kwenye Sekta ya Mifugo utumika kutokomeza wadudu waharibifu kama mbungo kule Zanzibar na kwa sasa hakuna tena.

Pia amesema, mionzi utumika kwenye sekta za ujenzi kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa reli, ujenzi wa mindombinu ya bomba la mafuta na katika suala zima la utafiti kwenye vyuo vikuu na maeneo mengine yanayofanya utafiti.
Amesema, kuna sababu nyingi za kudhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa na sababu hizo ni kama usafirishaji holela wa vyanzo vya mionzi.

Bw. Ngamilo amesema kuwa, endapo itatokea vyanzo hivyo vikaingia kwenye mnyororo wa bidhaa italeta shida kwani endapo wananchi wakizitumia bidhaa ambazo zina viasili vya mionzi matokeo ni magonjwa ya saratani na kuharibu mfumo wa DNA na kupelekea mama kujifungua mtoto ambaye ana mapungufu.

"Hivyo kama taasisi yenye jukumu la kudhibiti matumizi ya mionzi lazima tuhakikishe wananchi,mazingira, wafanyakazi wote wanakuwa salama dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza kupitia mionzi.

"Sababu nyingine ya uwepo wa mionzi ya asili kwenye udongo na mazingira yetu kwa sababu nchi yetu katika maeneo mengi ina madini ya urani, hivyo ni jukumu letu kama taasisi iliyopewa mamlaka ya udhibiti kuweza kuchukua sampuli mbalimbali za kimazingira na kuweza kuangalia viasili vya mionzi vilivyomo, hii yote ni katika kuhakikisha tunawalinda watanzania dhidi ya madhara ya mionzi,"amesema.
Ametaja sababu nyingine kuwa, ni wajibu wa Serikali kulinda wananchi dhidi ya uchafuzi wa mnyororo wa bidhaa.

Bw.Ngamilo amesema kutokana na majukumu hayo, wana ofisi zaidi ya 29 nchi nzima zikiwemo ofisi ndogondogo lengo ni kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya mazara ya mionzi lakini pia na kurahisisha biashara kwa wafanyabiashara wote.

Sababu nyingine, Bw.Ngamilo amesema kuwa, ni kuhakikisha wanalinda soko la bidhaa nje ya nchi kwani kwa sasa kuna vita kubwa vya kiuchumi ambapo kipindi cha nyuma shehena kubwa ya mizigo kutoka Tanzania ilizuiliwa kwa madai ina sumu kuvu jambo ambalo sio kweli, kwani yale mahindi hayakutokea Tanzania ndiyo maana Serikali iliamua kuanzisha taasisi hiyo katika kulinda bidhaa za Tanzania nje ya nchi.

"Leo hii tukipoteza soko nje ya nchi kwa kusingiziwa kwamba linaweza likawa bidhaa zako kuwa na viasili vya mionzi inaweza kutuchukua muda mwingi sana na gharama kurudisha hilo soko,"amesema.
Pia amesema kuwa,sababu nyingine ni kutimiza matakwa ya kisheria, Sheria namba 7 ya Nguvu za Atomiki ambayo inawataka kudhibiti, Sheria za kimataifa kama Sheria ya Shirika la Afya Duniani (WHO),Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani ambapo kama Tanzania ni wanachama.

"Kwa hiyo hizo ni baadhi ya sababu za msingi zinazotufanya sisi kama Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania tuweze kudhibiti mionzi katika mnyororo wa bidhaa,"amesema Ngamilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news