Serikali yaahidi kutoa usaidizi wa haraka kurejesha hoteli zilizoteketea kwa moto Zanzibar

NA MWANDISHI MAALUM

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali itatoa kila aina ya ushirikiano katika kurudisha hali za hoteli zilizoathiriwa na janga la moto.
Mheshimiwa Hemed alieleza hayo wakati alipofanya ziara ya kuzikagua hoteli nne zilizoathiriwa na janga la moto huko Jambiani Kibigija Mkoa wa Kusini Unguja pamoja na kuwafariji wawekezaji wa hoteli hizo.

Katika kufanikisha azma hiyo, Makamu wa Pili wa Rais aliziagiza mamlaka na taasisi zinazohusika na masuala ya sekta ya utalii kukaa pamoja na kuja na mapendekezo ya kuishauri serikali yatakayosaidia kurudisha hali za hoteli hizo.

Aliwataka wawekezaji hao kujenga imani kuwa serikali imeguswa na kadhia hiyo na itatoa ushirikiano wake katika kuwasaidia wawekezaji waliopatwa na athari.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwae Hemed alizitaka mamlaka zinzohusika na utoaji wa huduma kwa wawekezaji kuendelea kutoa taaluma kwa wawekezaji juu ya miundombinu bora ya kutumia katika ujenzi wa hoteli ili kuepukana na athari.

Aidha, aliupongeza uongozi wa serikali za mkoa na wilaya kwa hatua za haraka walizozichukua katika kukabiliana na janga hilo ambapo hakuna taarifa yoyote ilioripotiwa ya majeruhi wala kifo.

Akitoa taarifa kuhusiana na janga hilo la moto Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mheshimiwa Rashid Hadidi Rashid alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa, jumla ya hoteli nne zimetekea kwa janga la moto lililosababishwa na kuungua kwa sehemu ya jikoni katika hoteli ya Villa De Coco.

Mheshimiwa. Hadidi alieleza kwamba moja kati ya changamoto iliojitokeza ni kukosekana kwa miundombinu bora ya kupambamba na janga la moto na kuishauri serikali kuangalia namna nzuri ya kuimarisha miuondombini hiyo ikizingatiwa Mkoa wa kusini ni Ukanda wa uwekezaji wa hoteli za kitalii.

Alibainisha kuwa kufuatia tukio hilo la janga la moto bado thamani halisi ya athari iliopatikana hajifahamika ambapo wahusika wanaendelea na zoezi la kufanya tahhmini.

Nao, wamiliki wa hoteli hizo waliipongeza serikali kwa jitihada zake kwa kushirikiana nao katika zoezi zima la uokoaji wa wageni waliokuwepo katika eneo la tukio.

Waliiomba Serikali kungalia jinsi itakavyoweza kuwasaidia kwani athari iliowapata ni kubwa na ikizingatiwa kwa kipindi kirefu sasa hawakufanya biashara kutokana na wimbi la ugonjwa wa UVIKO-19.

Hoteli hizo zilizoathiriwa na janga la moja ni pamoja na Villa de Coco, Kobe House, Fan Beach na Spice Island na kusababisha jumla ya wafanyakazi 48 watakuwa hawana ajira kufuatia tukio hilo la hoteli kuungua moto.

Post a Comment

0 Comments