Serikali yaanza mchakato wa kujenga Barabara ya Same-Mkomanzi ya kilomita 96.46 kwa kiwango cha lami

NA MWANDISHI MAALUM

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Same - Kisiwani-Mkomazi yenye urefu wa (KM 96.46).
Muonekano wa barabara ya Same-Kisiwani-Mkomazi yenye urefu wa (KM 96.46), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akikagua maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo, Mhandisi Kasekenya amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo itahusisha KM 11.9 ambapo ujenzi utaanzia sehemu ya Mroyo - Ndungu hadi Kihurio.
Muonekano wa madaraja ya Mamba na Yongoma ambayo ujenzi wake umekamilika, madaraja hayo ni miongoni mwa madaraja zaidi ya sita yanayojengwa katika barabara ya Mwembe-Myamba-Ndungu yenye urefu wa KM 90.19.

Barabara hiyo ambayo inapita pembezoni mwa hifadhi ya taifa ya Mkomazi itachochea na kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi, kilimo, utalii na biashara kwa wakazi wa tarafa za Gonja, Ndungu, Kihurio, Bendera na Mkomazi wilayani Same na hivyo kukuza uchumi wa wakazi hao.

“Tumejipanga kuijenga barabara hii kwa lami na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa,”amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

Aidha amekagua ujenzi wa madaraja ya Mamba na Yongoma ambayo ujenzi wake umekamilika katika barabara ya Mwembe-Myamba-Ndungu na kuzungumzia umuhimu wa wananchi kulinda miundombinu hiyo ili itumike wakati wote wa mwaka.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando (wa pili kulia), akionesha na kufafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokagua maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Same-Kisiwani-Mkomazi yenye urefu wa (KM 96.46), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando amesema ujenzi wa madaraja na makalvati katika barabara ya Mwembe hadi Ndungu ni zoezi endelevu hivyo kuwataka wananchi kuepuka kulima karibu na hifadhi ya barabara ili kuepuka mmomonyoko wa udongo.
Naye Mbunge wa Same Mashariki,Mhe. Anne Kilango Malechela amesema ujenzi wa barabara ya Same-Kisiwani-Mkomazi (KM 96.46), na Mwembe-Myamba-Ndungu (KM 90.19), ukikamilika utafungua uchumi wa wakazi wa wilaya ya Same ambao kwa kiasi kikubwa unategemea shughuli za kilimo cha mazao ya tangawizi na ndizi na kuhuisha utalii katika hifadhi ya taifa ya Mkomazi.
Mbunge wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malechela akitoa shukrani zake kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (kushoto) na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando (kulia), mara baada ya kukagua ujenzi wa madarara ya Mamba na Yongoma ambayo ujenzi wake umekamilika katika barabara ya Mwembe-Myamba-Ndungu yenye urefu wa (KM 90.19). (Picha zote na WUU).

Post a Comment

0 Comments