Serikali:Wala rushwa, watumia lugha chafu Kituo cha Afya Sinza wachukuliwe hatua

NA FRED KIBANO

SERIKALI imeuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam kuwachukulia hatua watumishi wasio waadilifu mara moja na kuwasilisha taarifa yao Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kabla ya Desemba 30, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Afya Sinza mkoani Dar es Salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote ambaye anatumia lugha chafu kwa wagonjwa, kula rushwa na kujihusisha na vitendo vya aina hiyo.

Dkt. Dugange amesema, Kituo cha Afya cha Sinza kimekuwa kikilalamikiwa kwa vitendo vya rushwa vilivyokithiri, lakini pia kushindwa kutoa dawa kwa asilimia 95 wakati makusanyo ya fedha ni makubwa.

“Kituo cha Afya Sinza eneo la kwanza ni ukosefu au upungufu wa dawa, eneo la pili linalolalamikiwa ni kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu, lakini pia matumizi ya lugha chafu kwa wagonjwa,” amesema Dkt. Dugange.

Dkt.Dugange ameagiza kuwekwa mfumo madhubuti wa ununuzi na udhibiti wa dawa baada ya kubaini baadhi ya taarifa zinazokinzana bila ya kutolewa kwa maelezo ya msingi na hivyo kuagiza pia kuongeza mapato ya kituo hicho cha afya hadi kufikia milioni 150 kwa mwezi ifikapo Desemba 30, 2021.

Aidha, amewataka kuongeza kiwango cha upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 80 hadi 85 hadi kufikia asilimia 95 na asilimia 100 kwa dawa zote muhimu. 
 
Ametaka kushirikishwa kwa timu ya ununuzi wa dawa kukaa kwa pamoja na kununua dawa zitakazokuwa na tija kwa wananchi.

Ameagiza vituo vya afya vyote nchini kuhakikisha upatikanaji wa dawa zote muhimu kufikia asilimia 100 na pia kuongeza usimamizi na ufanisi katika kutoa huduma huduma bora kwa watanzania.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, Bi. Beatrice Dominic ameahidi kutoa taarifa ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi wasio waadilifu kabla ya tarehe 30 Desemba, 2021 lakini pia kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa zaidi ya asilimia tisini na tano na kurudisha hali ya uwajibikaji ikiwa ni pamoja na watumishi kuacha kutoa lugha chafu kwa wagonjwa.

Awali akitoa maelezo kwa Naibu Waziri, OR-TAMISEMI Dkt. Festo Dugange, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sinza, Dkt. Leonard Mwamkoa amesema, jumla ya watumishi watano ambao wametuhumiwa na wagonjwa kujihusisha na vitendo vya rushwa wamekwishachukuliwa hatua za kinidhamu na mashauri yao yapo katika hatua mbalimbali.

Dkt. Leonard amesema, pia baadhi ya madaktari wamekuwa na tabia ya kuwaandikia wagonjwa dawa ambazo hazipo hospitalini hapo ili wakanunue kwenye maduka ambayo wanamaslahi nayo wakati dawa mbadala zipo kwenye kituo cha afya na kwamba suala hilo pia linafanyiwa kazi kwa madaktari wenye tabia hiyo.

Post a Comment

0 Comments