Tottenham Hotspurs kumtangaza mrithi wa Nuno Espirito Santo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kocha wa zamani wa Chelsea na Inter Milan, Antonio Conte huenda leo akawa mbadala wa kocha Nuno Espirito Santo ambaye ametimuliwa Tottenham Hotspurs.

Ni baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy na Mkurugenzi wa Michezo, Patricio Paratici kusisitiza wanataka kumpata mrithi wa kocha huyo haraka, pengine siku moja baada ya kufutwa kazi kwa maana ya Novemba 1, 2021.
Conte huenda akatangazwa leo kumrithi Nuno Espirito (47) ambaye alihudumu miezi minne pekee katika klabu hiyo.

Uamuzi huo ulikuja, baada ya Tottenham Hotspurs kupoteza mechi tano kati ya saba zilizopita katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ikiwemo ya Jumamosi ya Oktoba 30, 2021 ambayo ilishuhudia Manchester United ikiwacharaza bakora 3-0 kwa sufuri wakiwa nyumbani katika dimba la The Tottenham Hotspur Stadium.

Kwa sasa, Tottenham Hotspurs wanashikilia nafasi ya nane kwenye msimamo wa EPL kwa alama 15 huku pengo la alama 10 likionekana kati yao na Klabu ya Chelsea.

Nuno Epirito aliajiriwa na  Tottenham Hotspurs kwa mkataba wa miaka miwili kuanzia mwezi Juni, mwaka huu baada ya kuagana na Wolves waliojivunia maarifa yake kwa kipindi cha miaka minne.

Kocha huyo alirithi mikoba ambayo Spurs waliipoka kutoka kwa ndugu yake, Jose Mourinho ambaye kwa sasa yupo AS Roma.

Mzee Conte hajawahi kupata kikosi kipya tangu aondoke Inter Milan mnamo Mei, ikiwa ni wiki chache baada ya kuongoza wababe hao kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) chini ya miaka 11.

Kocha huyo raia wa Italia alishinda ubingwa wa EPL na Kombe la FA akihudumu kambini mwa Chelsea.

Hata hivyo, alipigwa chini Julai 2018 baada ya waajiri wake kusajili matokeo duni katika msimu wa pili chini yake.

Kiungo huyo wa zamani aliwahi pia kunoa kikosi cha Juventus kati ya 2011-14 na akanyanyua mataji matatu ya Serie A kabla ya kupewa mikoba ya timu ya taifa ya Italia kuanzia 2014 hadi 2016.

Conte alikuwa miongoni mwa wakufunzi wa kwanza waliozungumziwa na Tottenham Hotspurs kuhusu uwezekano wa kujaza pengo la Mourinho aliyetimuliwa mwezi Aprili kwa sababu ya matokeo mabaya.

Hata hivyo, walishindwa kutimiza baadhi ya masharti ya Conte ambaye pia amekuwa akihusishwa na Manchester United iwapo Ole Gunnar Solskjaer ataondoka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news