Wanawake wapata mafanikio lukuki kupitia elimu ya afya ya uzazi Endasaki

NA MARY MARGWE

MWENYEKITI wa Kijiji cha Endasaki wilayani Hanang' mkoani Manyara, Hussein Qaresi ameudhihirisha usemi wake wa "Elimu ni nzuri zaidi ya kuwezeshwa pesa" ambapo umeleta matokeo lukuki na chanya kwa wanawake na wasichana wa Kata ya Endasaki waliopatiwa elimu juu ya haki ya afya ya uzazi salama, iliyotolewa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara ( MNRPC ).
Kauli ya " Elimu ni nzuri zaidi ya kuwezeshwa pesa " aliitoa wakati alipokuwa akizungumza na wanawake, wasichana walipokuwa wakipatiwa elimu juu ya haki ya afya ya uzazi salama iliyotolewa hivi karibuni na klabu hiyo huku ikihusisha zaidi ya wanawake na wasichana wapatao 60 kutoka katika Kata ya Endasaki.

Qaresi amesema kauli hiyo aliongea akijua dhahiri kuwa, mafunzo hayo yatakuja kuwabadilisha washiriki na kuwa tofauti kama walivyoingia siku ile pale ukumbini, ambapo amesema elimu hiyo imetoa matokeo chanya kwa wengi wao kwani tayari akina mama wameanza kuandaa taarifa za mirathi na wosia ili kuacha kama nyaraka mahakamani na wengine kupeleka BAKWATA kwa ajili ya kuja kuwasaidia hapo baadaye na hatimaye kuweza kuondokana na ukatili utakaoweza kujitokeza huko baadaye.

"Mimi ndio maana huwa nasemaga hivi elimu yoyote ile unapoipata itakutoa ulipo na kukupeleka sehemu nyingine tofauti na ndio maana huwa nawaambia washiriki wowote wanapopatiwa mafunzo ya elimu wewe makini sana katika kusikiliza kuliko kuwaza nitapewa shilingi ngapi, kwani pesa ukipatiwa leo hata kiasi gani itakwisha na kurudi katika hali yako ya awali. Lakini elimu ukiitumia vizuri itakupatia mafanikio makubwa,"amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Aidha, amesema licha ya kumueleza baadhi yao kuanza kuandaa taarifa ya mirathi na wosia, lakini yupo msichana aitwaye Halima aliyekwenda kwake kumueleza matatizo makubwa yanayoikabili ndoa yake na kumuelekeza aende BAKWATA ambapo ni sehemu sahihi ya kufikisha tatizo lake, jambo ambalo awali kabla ya kupatiwa elimu ya haki ya afya ya uzazi salama halikuwepo, alikuwa akiishi katika mazingira magumu na mume wake, ambapo kwa sasa baada ya kupata mwanga na ujasiri njia ameiona.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Endasaki wilayani Hanang' mkoani Manyara, Hussein Qaresi, alipokuwa akizungumza na wanawake, wasichana waliokuwa wakipata elimu juu ya haki ya afya ya uzazi salama, mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni huko Endasaki. (Picha na Mary Margwe).

"Elimu waliyoipata imewasaidia kuwafumbua macho na kuona kila baya lililokuwa likifanyika awali dhidi yao ambapo kwa sasa wameona la! kumbe nilikuwa nateseka kwa sababu ya kutokujua haki yangu, lakini kwa sasa baada ya kupatiwa elimu hii hakika wanawake na wasichana wamebadilika na kujitambua haki zao za msimgi katika familia zao wanaendelea kuishi kwa amani, maana nyumba ikikosa amani machafuko hutokea, hivyo pata kwanza amani, furaha na upendo vitafuata,"amesema Qaresi.

Akiongea kwa furaha na DIRAMAKINI BLOGA mmoja wa wanufaika wa elimu hiyo, Salome Athanas amesema kufuatia elimu hiyo wanawake wameweza kushirikiana na kuanzisha biashara ndogo za ujasiriamali na kuondokana na ukatili wa kiuchumi, ambapo kwa sasa wameweza kusaidiana kimaisha na waume zao, jambo ambalo awali wanaume walikuwa wakiwazuia kujihusisha na biashara wakisema ni uhuni, lakini baada ya kupata hiyo elimu wakaenda kuwaelimisha waume zao na sasa wanafanya biashara na maisha yanakwenda vizuri.

"Jamani kabla ya kupata hii elimu wanawake wengi walikuwa wakikaa tu nyumbani wakisubiria kila kitu kufanyiwa na mwanaume, siku ikitokea mwanaume amerudi nyumbani bila kitu basi wanalala njaa, lakini baada ya wanaume kuelimishwa na kuelewa sasa wamewakubaliana ambapo awali kwbla ya mafunzo haikuwa kazi rahisi, lakini wameelewa tunafanya biashara tunasaidiana maisha, awali walidhani kufanya biashara kufanya uhuni, tunaishukuru klabu ya waandishi wa habari mkoa wetu wa Manyara (MNRPC) kwa kutuletea mafunzo haya ambayo yametusaidia sana, sasa hivi hatunyanyasiki tena kama awali,"amesema Salome Athanas.

Naye Elizabeth January amesema, mafunzo waliyoyapata kwao ni kama taa ya kuwaonyesha walikotoka, walipo na waendapo, walikosa mwanga lakini kwa sasa baada ya elimu ya haki ya afya ya uzazi salama imewaelimisha ipasavyo.

January amesema kwanza awali akina mama walikuwa hawapendani wala hawakuwa wanasaidiana lakini chakushangaza baada ya kupatiwa mafunzo hayo wamekuwa na upendo, wanaishi kwa umoja na mshikamano, na wakati mwingine wanatembeleana na kupeana ushauri mbalimbali.

"Kama ambavyo mnajua kuna wakati sisi wanawake huwa hatupendani kabisa, mwenzio akigombana na mumewe mwingine anaona furaha yaani anafurahia mateso ya mwingine, ndio maana hata huenda kuna wakati unaweza ukafurahia kupigwa kwa mwenzio badala ya kwenda kugombezea, ndio mwanzo unaishia kuchungulia madirishani huku mwenzio anajeruhiwa vibaya pengine hata kupoteza maisha kabisa, baadaye unabakia kusema ningejua...ungejua nini wakati ulikua unafurahia," alifafanua January.

Mmoja wa wanaume Jumnne Akonaay ambaye mke wake alibahatika kupata mafunzo ya haki ya afya ya uzazi salama amesema, kila kitu bila kupatiwa elimu ya kueleweka haitamfikia mlengwa, hivyo kwakuwa ameeleweshwa vizuri ameelewa na sasa amemruhusu mkewe Amina Kassim kuanza kufanya biashara ndogo ndogo ili kusaidiana maisha na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Aidha, mafunzo hayo yalitolewa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara (MNRPC), chini ya mwenyekiti wake Zacharia Mtigandi na Mratibu wa mradi huo, Jaliwason Jason ambaye pia ni katibu wa klabu hiyo ya waandishi wa habari mkoani humo na kufadhiliwa na Women Fund Trust (WFT).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news