Washirikiana kudhibiti mmoja wa majambazi yaliyopora milioni 30/- kituo cha mafuta

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MENEJA wa Kituo cha kuuza mafuta cha Hike kilichopo mjini Isongole wilayani Ileje mkoani Songwe amevamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za moto huku wakimpora fedha shilingi milioni 30.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Amewaeleza waandishi wa habari ofisini kwake kuwa,kufuatia tukio hilo la juzi Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi walianzisha msako mkali na kufanikiwa kumkamata na kumuua mmoja kati ya majambazi waliohusika katika uporaji huo.

Alimtaja mtu huyo ambaye anahisiwa kuwa ni jambazi ambaye aliuawa kuwa ni Emili Yeka Mwakayamba (39) baada ya kukamatwa na wananchi katika Kijiji cha Sange, wilayani humo na kumjeruhi kwa kipigo kilichosababisha kifo chake.

Kamanda Magomi amesema kuwa mtuhumiwa huyo aliomba lifti katika gari aina ya fuso na kutokana wananchi na Jeshi la Polisi kujipanga na kuweka vizuizi katika njia mbalimbali za kuingia na kutoka Ileje baada ya kulisimamisha gari hilo dereva aliwaeleza viongozi wa kata kuwa kuna mtu wamempakia na wanamtilia mashaka ndani ya gari lao.

Amesema, baadaye mtu huyo alitolewa katika gari hilo na kumpeleka katika ofisi ya Mtendaji wa kijiji kwa ajili ya kumuhoji na kumfanyia upekuzi ambapo jambazi huyo alidai alitoka kwa mganga na alipoulizwa ni kijiji gani alitoka alishindwa kukitaja na kuwaomba atoe vielelezo vyake ndani ya begi lake.

Amesema walipomruhusu ghafla mtu huyo alitoa bunduki ya kivita aina ya Ak 47 na kuwaelekezea mtendaji na mgambo waliokuwa wanamuhoji, lakini bahati nzuri mmoja kati ya mgambo hao aliweza kumrukia na kuishika bunduki hiyo na katika purukushani risasi mbili zilifyatuliwa humo ndani ofisi.

Amesema baada ya kurukushani wananchi wakazi wa kijiji cha Sange walisogea eneo la tukio na kuanza kumshambulia jambazi hadi kupelekea kifo chake.

Pia amesema kuwa, walipopekuliwa katika begi lake alikutwa na pesa kiasi cha shilingi milioni 1,200,000 na silaha nyingine aina ya bastola iliokuwa na risasi tano kati ya nane zilizostahili kuwepo ndani ya silaha na haijajulikana risasi tatu zingine zilitumika wapi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news