Watumishi wa Mungu watoa wito mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia

NA FRESHA KINASA

VYOMBO vya habari nchini vimetajwa kuwa na umuhimu mkubwa katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hapa nchini hususani katika uibuaji wa matukio ya ukatili na utoaji wa elimu kuhusiana na madhara yake na hivyo vimeombwa kuendelea kuelimisha wananchi katika kuhakikisha jamii inakuwa na ustawi bora wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na baadhi ya viongozi wa dini mkoani Mara Novemba 27, 2021 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI BLOG kuhusiana na mchango wa vyombo vya habari na wadau mbalimbali zikiwemo Asasi za Kiraia katika kufanikisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Askofu Mkuu wa Kanisa la World Evangelism Mission (WEM) lililopo Machinjioni katika Manispaa ya Musom,a Saimon Kiange amesema kuwa, vyombo vya habari vimeendelea kufanya vyema katika utoaji wa elimu kupitia mijadala, makala na vipindi katika Radio, mitandao ya Kijamii na Televisheni kwa jamii hususani madhara ya ukatili na kuhimiza ushiriki wa kila mtu kumaliza vitendo hivyo jambo ambalo limesaidia kuongeza uelewa kwa wananchi.

"Tumeendelea kushuhudia katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mijadala mbalimbali inaendeshwa katika vyombo vya habari kuhusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia. Niseme kwamba vyombo vya habari na wanahabari wanafanya vyema katika kuelimisha umma, niombe elimu izidi kutolewa, wananchi waweze kuwafichua wanaofanya mambo ya ukatili ili Serikali iwachukulie hatua lengo ni kutokomeza ukatili wa kijinsia,"amesema Askofu Kiange.

Aidha, Askofu Kiange amesema, yapo mashirika mbalimbali na wadau nchini wanao pambana na vitendo hivyo kwa njia ya utoaji wa elimu, hifadhi kwa waathirika wa ukatili na msaada wa kisheria, amesema mambo wanayofanya yana tija kubwa kwa maendeleo ya jamii kuanzia ngazi ya familia, hadi taifa na hivyo amesisitiza mashirika hayo na wadau wote waungwe mkono na kuthaminiwa na Serikali katika harakati hizo na pia wajikite kufika maeneo ya vijijini kuendesha mijadala ya utoaji elimu kwa kuyagusa makundi yote wakishirikiana na vyombo vya habari kwa ukaribu.

"Niombe pia wahusika wanapofikishwa kwenye vyombo vya sheria wananchi au waliofanyiwa ukatili wajitokeze kutoa ushahidi kusudi watuhumiwa kutiwa hatiani na Serikali naiomba ingeweka adhabu kali kwa wanaobainika kusudi liwe fundisho kwa wengine. Jamii isichukulie jambo la ukatili kama sehemu ya maisha bali ione ni tatizo ambalo lazima lishughulikiwe liishe kabisa, mila zote mbaya zipigwe marufuku kwa nguvu zote kuanzia shuleni, nyumbani na katika Taasisi zote,"amesema Askofu Kiange.
Kwa upande Wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC) nchini ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa hilo Katika Kata ya Kigera Manispaa ya Musoma, Jacob Lutubija amesema, kwa sasa vitendo vya ukatili wa kijinsia vimeendelea kuibuliwa na vyombo vya habari katika maeneo mbalimbali nchini tofauti na miaka ya nyuma na hivyo akasema vithaminiwe na kushirikishwa kikamilifu kutokana na umuhimu wake katika nyanja mbalimbali za maendeleo nchini.

Amesema, kipindi cha nyuma vitendo hivyo vilifumbiwa macho na hamasa ya kuripoti katika vyombo vya sheria haikuwa kubwa na pia akasema Serikali na Mashirika kwa Sasa wameendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ikiwemo kutoa elimu na kuwachukulia hatua wahusika na amesisitiza mshikamano uwepo baina ya Serikali, wanasiasa, wadau na Wananchi wote huku akiomba mila zenye madhara ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake ulawiti wa watoto na matukio mengine ya kikatili kwa sasa hayana nafasi katika kujenga kizazi chenye ustawi.

Pia, Askofu Lutubija ameomba viongozi wa dini kuendelea kuhimiza amani na kukemea maovu yakiwemo matukio ya kikatili kwa njia ya mafundisho ya neno la Mungu huku akitoa msisitizo kuwa ukatili ni kinyume na agizo la Mungu kwani Mungu ameagiza watu wote kupendana, kujaliana, kuthaminiana na kushirikiana kwa mema hivyo mtu akifanya Ukatili lazima atambue amefanya dhambi mbele za Mungu na hivyo sheria inapaswa kuchukua mkondo wake.
Naye Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Life in Christ Prayers Ministry lenye makao makuu yake Kata ya Bweri ambaye pia ni Afisa Mratibu wa Shirika linalojishughulisha na kusaidia Watoto wanaoishi Mazingira magumu la New Trust Help Foundation Tanzania, Mchungaji Daud Japhet amesema kuwa, vyombo vya habari vinalo jukumu la kuifanya ajenda ya mapambano ya ukatili wa kijinsia iwe endelevu hasa kutoa elimu kupitia vipindi, na makala badala ya kusubiri pale tukio linapojitokeza ama katika maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili ambayo hufanyika kila mwaka Novemba 25 hadi Desemba 10.

"Vyombo vya habari na wanahabari niwapongeze, wanaendelea kuripoti matukio ya ukatili na kuifanya serikali na wadau waongeze nguvu ya mapambano. Niiombe serikikali na mashirika yanayopambana na ukatili wawe na mfuko maalumu kuwawezesha Wanahabari kufanya ufuatiliaji wa kuripoti matukio hayo vijijini huko wanawake wanapigwa hawana mtu wa kuwasemea ila wanahabari wana uwezo wa kufichua na kutoa elimu na pia kila mtu akishiriki vyema kuanzia ngazi ya familia, shuleni, vyuoni, hakika Ukatili utapungua kwa kiwango kikubwa kama sio kuisha kabisa."amesema Mch. Japhet.

"Nilipongeze Jeshi la Polisi nchini chini ya IGP Sirro wameendelea na mkazo wa kuhimiza Wwnanchi kuwafichua wahusika na hatua wamekuwa wakichukua ikiwemo kuwafikisha wahusika mahakamani na kutoa elimu kupitia Dawati la Jinsia lazima tutambue kuwa kupiga wanawake ni kosa, kubaka ni kosa, kulawiti ni kosa kukeketa mabinti ni kosa na ukatili mwingine wa kiuchumi na kisaikolojia Kama matusi hayafai hivyo ni vyema kila mtu akaonesha ushiriki wake kuzingatia haki za binadamu kwa ufanisi bila kuwaachia jukumu hilo Polisi, Serikali ama Asasi za Kiraia,"amesema.

Naye Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God Jimbo la Mara (PAGT) lililopo Kata ya Kamunyonge Manispaa ya Musoma, Mchungaji Deus Kijeti amewaomba wananchi kufuata mafundisho sahihi ya Neno la Mungu na kujiepusha kutenda dhambi huku akisistiza kuwa upendo ndio Msingi wa yote na kumtii Mungu na kwamba mtu akimpenda ndugu yake hata mfanyia ukatili wowote ule na kwamb atasimama katika misingi na maagizo ya Mungu.

"Kuna watoto pia wanafanya ukatili kwa mfano wazazi wanamhudumia kila kitu na kumsomesha shule nzuri, lakini anakuwa na makundi yasiyofaa akionywa anakimbia nyumbani kwenda kuishi mitaani na kusema amefukuzwa kumbe yeye ndiye mkosaji. Niombe kila mmoja ahusike kuepusha mazingira ya ukatili kutokea kwenye familia na jamii baba atimize wajibu, mama pia na mtoto ili jambo hili liende sawia,"amesema Mchungaji Kijeti.

Post a Comment

0 Comments