Waziri apiga marufuku uuzaji wa shaba nje, atoa tamko kuhusu bei za vifaa vya ujenzi

NA DOREEN ALOYCE

SERIKALI imepiga marufuku wafanyabiashara uuzaji nje ya nchi Shaba Chakavu (copper Scraps) na za Ingots shaba ambazo hutumika katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za vyuma  hapa nchini.

Kauli hiyo imeitolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa kuhusu tathimini ya mwenendo wa uzalishaji , usambazaji na bei za vifaa vya ujenzi nchini kwa kipindi cha Septemba mpaka Novemba  mwaka huu.

Amesema kuwa, kutokana na nchi ya Tanzania kuwa na bidhaa zinazotokana na Shaba hasa mabati ambapo kwa hapa nchini kuna viwanda viwili, bidhaa hizo zimeonyesha kupanda bei kutokana na kwamba wazalishaji wanategemea nchi ya China kutafuta malighafi za kutengenezea bidhaa hizo ambazo zimekuwa adimu nchini China.

"Viwanda viwili vya kuzalisha mabati vina uwezo wa kuzalisha kwa mwaka mabati 14,949,703 sawa na tani 200,000) kwa mabati ya geji 28 ambayo utumika zaidi, hivyo kwa Mkoa wa Mwanza imepanda kutoka shilingi 31,700 kwa mwezi Septemba mwaka huu hadi shilingi 33,400 mwezi Novemba mwaka huu," amesema.

Amesema kuwa,kwa upande wa saruji  hapa nchini kuna viwanda tisa vyenye uwezo wa kuzalisha tani 9,080,000 kwa mwaka na kwamba bei za saruji zimepanda kwa wastani wa shilingi 1,000 kwenye mikoa ya Mwanza ,Dar es Salaam,huku Mkoa wa Ruvuma bei ikishuka kwa asilimia  15 kutokana na kuwa karibu na kiwanda cha Dangote.

"Pia tuna viwanda 16 vya nondo vyenye uwezo wa kuzalisha tani 1,082,788 za ukubwa mbalimbali na kwa mwaka vinaweza kuzalisha wastani watani 750,000 za nondo,hivyo kama Serikali hatuna budi kuzuia bidhaa ambazo zinatokana na haya malighafi kutokwenda nje ya nchi kwani hazitoshelezi, "ameongeza.

Amesema kuwa, kutokana na hali hiyo Serikali inachukua hatua kudhibiti ongezeko lisilohalali la bei za bidhaa muhimu nchini ikiwa ni kuhakikisha wizara husika kutoa taarifa ya mwenendo wa wastani wa bei za bidhaa muhimu kila mwezi kwa mikoa yote ambapo itawapa wahusika uelewa wa kutosha kuhusu uhalisia wa bei za bidhaa.

"Nawahimiza Tume ya Ushindani kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upangaji wa bei nchini na kuwachukulia hatua stahiki za kisheria wafanyabiashara ambao wanakiuka sheria ya ushindani nchini.
"Jambo lingine Serikali Katika mpango wa muda mrefu itatekeleza miradi kielelezo itakayotuwezesha kuzalisha chuma kingi hapa nchini kwa ajili ya viwanda vya ndani na  kuuza nje ya nchi sambamba na kurekebisha sheria na kanuni ili kuruhusu kuingizwa kwa urahisi malighafi zinazohitajika Katika uzalishaji wa bidhaa za vyuma, "amesema Profesa Mkumbo. 

Mwakilishi kutoka Tume ya Ushindani, Allan Mlulla ambaye amehudhuria kikao hicho alisema wamechukua maelekezo yaliyotolewa na Waziri huku wakiahidi kuyafanyia kazi na kuchunguza huku atakayebainika kuchukuliwa hatua.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi Shirikisho la Viwanda, Akida Mnyenyelwa amesema kuwa kupitia kauli hiyo italeta tija kwa wafanyabiashara hapa nchini na wenye viwanda wataenda kuwekeza bila wasiwasi .

"Tumeongea na wazalishaji na wameshangaa kuona baadhi ya  vyombo vya habari  vimeandika kwamba wazalishaji wa bidhaa viwandani wameongeza bei kubwa .

 "Kama Waziri alivyoeleza hapo awali sababu za kuongezeka kidogo gharama na ni kutokana kwamba kuna  ongezeko kidogo kwa ajili ya usambazaji  ambalo sio la kuleta taharuki kwenye jamii,"amesema Mnyenyelwa.

Post a Comment

0 Comments