Waziri atoa agizo Masasi baada ya kusuasua ujenzi wa madarasa

NA FRED KIBANO

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange ameiagiza Halmashauri ya Wilaya Masasi kuharakisha ujenzi wa madarasa katika halmashauri hiyo ili unakamilika kwa wakati.
Akiongea na watendaji wa Halmashauri za Masasi Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mbele ya Wenyeviti wa Halmashauri hizo na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Claudia Mkya, Dkt. Dugange amesema, hatakuwa tayari kuangushwa na watendaji, badala yake wafanye kazi usiku na mchana na kuhakikisha miradi ya ujenzi wa madarasa yote inakamilika ifikapo Desemba 15, 2021.

“Halmashauri ya Wilaya ya Masasi bado mnachechemea kwenye ujenzi wa madarasa kwa zaidi ya asilimia 60 hadi 70, bado mpo katika hatua ya msingi sasa hiyo siyo dalili njema, Mkurugenzi na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Masasi lazima mkajipange, muhakikishe miradi inakamilika kwa wakati, hayo ni maelekezo na hamtakiwi kujitetea na mimi sipo tayari kuangushwa,” amesema Dkt.Dugange.

Dkt.Dugange amewataka kukamilisha miradi hiyo kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha na siyo kujenga kwa haraka bila kufikia viwango vinavyokubalika. Aidha, amesema fedha zilizotolewa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya madarasa imewekwa pamoja na madawati na viti na hivyo ujenzi wa madarasa uendane sambamba na manunuzi ya samani za darasani.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Claudia Mkya amekiri kuwa halmashauri hiyo imekuwa na kasi ndogo kwenye ujenzi wa madarasa kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji na kuchelewa kupata saruji iliyoagizwa kutoka kiwanda cha Dangote na sasa changamoto hizo zimetatuliwa, hivyo basi amepokea maelekezo na atasimamia kwa kuhakikisha wanajenga usiku na mchana ili kukamilisha miradi katika muda uliopangwa.

Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bw. Apoo Tindwa amesema halmashauri yake ilipokea fedha za ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 kiasi cha shilingi Bilioni moja na milioni 960 kwa ajili ya kujenga madarasa 84 ya sekondari na madarasa 14 ya shule za msingi na kwamba yapo katika hatua mbalimbali.

“Madarasa 26 yapo kwenye hatua ya ujenzi wa maboma, madarasa manne ujenzi upo kwenye hatua ya linta na madarasa 68 ujenzi upo kwenye hatua ya msingi,”amesema.

Amezitaja changamoto zilizosababisha kuchelewa kwa ujenzi wa madarasa kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji, kutokupatikana kwa tofali za kununua kwa bei isiyozidi shilingi 1,500 kwa tofali moja na ucheleweshwaji wa saruji kutoka kiwandani.

Mapema mwaka huu Serikali ilipeleka fedha kwenye halmashauri zote kwenye nchi nzima ili kuhakikisha inapofika Januari mwaka 2022 wanafunzi wote waliofaulu na kupangiwa shule kuanza kidato cha kwanza wanaanza masomo kwa pamoja bila kuwa na chaguo la pili na la tatu.

Post a Comment

0 Comments