NA TITO MSELEM-WM
KATIKA kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji wote wa madini nchini kuhakikisha wanalinda afya zao kwa kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Aidha, Waziri
Biteko amewataka wachimbaji hao kuhakikisha wanatunza akiba ya kipato
wanachokipata na kutunza familia zao ikiwemo kuwekeza katika sekta
nyingine hususan katika Sekta ya Biashara na Kilimo.
“Hela
unayoipata usiidharau hata kama ni kidogo weka akiba ili ije ikusaidie
kesho ukiwa huna nguvu, leo unanguvu unaingia duarani lakini baada ya
miaka kadhaa hautaweza, utaitaji watu wa kukusaidia, nguvu ya leo uiweke
akiba kwa ajili ya kesho ili ikusaidi kuwa na kesho nzuri usije
ukawasumbua watu,” amesema Waziri Biteko.
Waziri Biteko amesema Wilaya ya Kaliua inafahamika kwa Kilimo cha
Tumbaku ambapo kwa sasa umetokea mlipuko wa Madini ya Dhahabu katika
eneo hilo na kusababisha Wilaya hiyo kuingia kwenye orodha ya Wilaya
zinazochimba Madini ambapo amewataka Wachimbaji hao kuendelea kuwa
watulivu na kufuata Sheria katika uchimbaji wao.
Pia, Waziri
Biteko amesema haki zipo nyingi kuna Haki ya Ardhi, Haki ya Anga, Haki
ya Madini na kadhalika, unaweza ukawa na shamba lakini mmiliki mkuu wa
shamba hilo ni wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenye
mamlaka ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama kwenye shamba
hilo kuna Madini hairuhusiwi yachimbwe mpaka kuwe na leseni katika eneo
hilo.
Pia, Waziri Biteko amewasisitiza wachimbaji wadogo kuachana na suala la kutorosha madini ambapo amewataka kuchimba kwa kufuata Sheria na kuhakikisha kodi ya Serikali inalipwa.
“Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anataka kuona Uchumi wa Madini unamilikiwa na Watanzania wa kawaida pia wachimbaji wote walioko sehemu mbalimbali ikiwemo Kaliua wanabadilisha maisha yao kwa rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amewabariki,” amesema Waziri Biteko.
0 Comments