Waziri Makamba aingia katika doria

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI wa Nishati, January Makamba, ameanza doria katika mito inayoingiza maji katika mabwawa ya vituo vyote vya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji.
Katika doria hiyo, Waziri Makamba aliambata na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande na viongozi waandamizi wa TANESCO. 

Doria hiyo ililenga kutathmini hali ya ukame katika mito hiyo, kiwango cha maji katika mabwawa, hali ya uzalishaji katika vituo hivyo na kutathmini hatua za kuchukua kukabiliana na hali hiyo.

Waziri Makamba alishuhudia mtiririko hafifu katika Mto Ruaha na kukauka mito midogo inayochangia katika mtiririko wa mto Ruaha na katika bwawa dogo la Kidatu. 

Hali hiyo imesababishwa na ukame mkali unaotokana na kutonyesha mvua katika maeneo yanayolisha mito hiyo na pia matumizi mabaya ya rasilimali - maji na uharibifu wa mazingira katika maeneo husika. 

Pia hali hii imesababisha upungufu wa Megawati 307 kati ya Megawati 561 zinazopaswa kuzalishwa kutokana na nguvu ya maji. 

Waziri Makamba pia alipata nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi katika vituo vya kuzalisha umeme, pamoja na wananchi na viongozi mbalimbali katika maeneo hayo.

Akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO na viongozi mbalimbali katika maeneo husika, Waziri Makamba alisema kwamba ni dhahiri kwamba kuna ukame mkubwa ambao umeathiri mtiririko wa maji na hivyo kuathiri uzalishaji wa umeme. 

Alisisitiza umuhimu wa hifadhi ya mazingira na matumizi ya rasilimali-maji yanayozingatia Sheria mbalimbali za nchi na hifadhi ya mazingira.

Alisema kwamba TANESCO na Serikali zinachukua hatua za muda mfupi, wa kati na muda mrefu kukabiliana na upungufu wa umeme. 

Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Ndugu Maharage Chande, aliongeza kwamba Shirika linachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia, kwa kuharakisha matengezo ya baadhi ya mitambo yake ya Ubungo I (MW 25), Upanuzi wa Kinyerezi I (MW 185) na Ubungo III (MW 112). 

Aidha, Shirika limelazimika kuwasha kituo cha kuzalisha umeme cha Nyakato (MW 36). Hatua hizi zitakazokamilika kwa hatua kuanzia Desemba, 2021 hadi Machi, 2022 zitasaidia kuongeza jumla ya MW 350 katika mfumo wa gridi ya Taifa. 

Shirika pia linaendelea na matengenezo na maboresho ya mfumo wa usambazaji na ugavi wa umeme ikiwemo kuharakisha maboresho ya miundombinu ya kusafrisha umeme ya 220kV Kidatu – Iringa, 220kV Kingolwira – Msamvu na vituo vya kusambazaumeme vya Msamvu, Luguruni, Kunduchi na Nyakanazi. 

Pia, TANESCO itafanya maboresho katika njia za kasambaza umeme ambazo kwa sasa ni ndefu nazinapelekea wateja kupata umeme hafifu (low voltage) na uharibifu wa mara kwa mara wa mita.

Waziri Makamba aliilekeza TANESCO kuhakikisha kwamba, pamoja na kadhia hii ya umeme, Shirika lisijiingize kwenye kukodi mitambo ya dharura kutokana na historia mbaya ya mitambo ya aina hiyo kuwa na gharama kubwa kwa Serikali na kugubikwa na utata mwingi. 

Badala yake, amelielekeza Shirika kuhakikisha kwamba linaongeza miradi mipya ya uzalishaji umeme kwa njia ya upepo na jua ambayo inaweza kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja ili mwakani katika kipindi kama hiki cha umeme taifa lisikabiliwe tena na uhaba wa umeme.

Pia ameelekeza kwamba TANESCO, kama msimamizi wa mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere kule Rufiji, ihakikishe kwamba mradi huo hauchelewi kwa kiwango kikubwa ili nao uchangie katika majawabu ya kudumu ya upatikanaji wa umeme nchini.

Waziri Makamba aliwasihi wananchi wawe na subira katika kipindi hiki kigumu wakati TANESCO ikihakikisha kwamba inadhibiti upungufu wa uzalishaji kwa njia mbalimbali. 

“Nimeingia katika nafasi hii katika siku 70 tu zilizopita, wajibu wangu ni kumsadia Rais wetu Mhe Samia Suluhu Hassan, na kuisaidia nchi yetu, kwa kuisimamia TANESCO ipasavyo ili itemize wajibu wake na tuondokane na kadhia hii haraka iwezekanavyo,"alisema Waziri Makamba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news