WAZIRI MKUU AZINDUA TAMASHA LA MVINYO DODOMA

>Asisitiza miche ya zabibu za matunda izalishwe kwa wingi

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua tamasha la mvinyo mkoani Dodoma na kusisitiza kuwa uzalishaji wa miche ya zabibu za matunda uongezwe ili wajasiriamali wapate bidhaa kutoka mkoa huo.

“Hizi zabibu zinazouzwa barabarani siyo za kula kama matunda, hizo ni za mvinyo. Tuweke juhudi ya kuzalisha miche ya zabibu za mezani ili wajasiriamali wanaouza zabibu kwenye stendi za mabasi wapate bidhaa kutoka hapa Dodoma,” amesema.
Ametoa wito huo leo Ijumaa, Novemba 5, 2021 wakati akizungumza na wananchi na wadau wa zao hilo waliofika kwenye uzinduzi wa tamasha la mvinyo kwenye viwanja vya Mashujaa jijini Dodoma. Tamasha hilo litaendelea hadi Jumapili, Novemba 7, mwaka huu.

“Tunataka miche ya zabibu kwa ajili ya mvinyo na ile ya kula izalishwe kwa wingi. Hivyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa itenge maeneo ya kuzalisha miche bora na kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja (Block farms) ili kuongeza uzalishaji na kurahisisha utoaji wa huduma za ugani, mitaji na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya mvinyo.

Pia amezitaka Sekretarieti ya Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zishirikiane na Wizara ya Kilimo kusimamia mikataba ya kilimo inayosainiwa baina ya wakulima, wanunuzi wa mazao na watoa huduma wengine ili kuhakikisha wakulima hawadhulumiwi.

Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo iratibu maonesho ya zabibu ili tamasha hilo liwe rasmi. “Mratibu wa tamasha hili, Bi. Atwite Makweta asaidiwe na wizara kusimamia maandalizi na kuanzia sasa haya maonesho yawe ya kudumu na yafanyike kila mwaka hapa Dodoma.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Anthony Mtaka kabla ya mwisho wa mwezi huu wakutane na wadau wa zao la zabibu wakiwemo wazalishaji, wasindikaji, wakulima na wenye viwanda na waibue mdahalo kuelekea miaka 60 ya Uhuru.

“Katika hili, mkae na muangalie kwenye zao la zabibu tumetoka wapi, tuko wapi na tunaenda wapi. Nini kifanyike ili kuimarisha zao hili, na hilo liende sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ambayo uzinduzi wake utafanyika hapa Dodoma tarehe 2 Desemba, 2021,” amesema.

Mapema, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo P. Pinda alisema anaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kulifanya zao la zabibu liwe miongoni mwa mazao nane ya kimkakati hapa nchini.

“Zao hili ni fursa kwa Dodoma na Taifa kutokana na upekee wake hapa nchini. Kwa hiyo kuna haja ya kuwaita wadau na kuwaelezea zao la mkakati maana yake ni nini na wananchi tutegemee nini katika jambo hili,” amesema.

Naye Waziri wa Kilimo, Prof. Mkenda alisema ili kuimarisha zao la zabibu, wizara hiyo imetenga sh. milioni 200 kwa ajili ya kituo cha utafiti (TARI) cha Makutupora na kati ya hizo, tayari sh. milioni 80 zimeshatolewa.

Alisema wizara hiyo pia imepanga kuboresha zao hilo kwa kuimarisha kitalu cha kuzalisha miche 300 katika shamba la umoja la Chinangali. “Miche hii itatosha kupandwa kwenye ekari 600. Pia tunafufua miundombinu ya umwagiliaji kule Chinangali ili kuhakikisha uzalishaji wa zao hili inaongezeka,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya wasindikaji wa zao hilo, Mkurugenzi wa kampuni ya Alko Vintage, Bw. Archard Kato alisema zao la zabibu lilianza kuzalishwa mwaka 1959 ambapo hadi kufikia mwaka 2005, wadau mbalimbali wakiwemo DOWICO, TAVICO, ALKO VINTAGE na CETAWICO wamekuwa wakiliendeleza kwa hatua tofauti na kufikia vijiji 93.

“Sasa hivi tumefikisha viwanda 15 kutoka viwanda saba vilivyokuwepo mwaka jana. Na hivi ni vidogo, vya kati na vikubwa. Tunakabiliwa na changamoto ya ubora wa zabibu kutokana na ukosefu wa utaalamu; nyenzo duni kwa wasindikaji na tunahitaji mafunzo zaidi kwa wakulima na wasindikaji ili kuboresha zao hili,” alisisitiza.

Naye Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Bw. Nsolo Mlozi alisema kwa miaka miwili sasa, benki hiyo imekuwa ikiwasaidia wakulima wa zabibu na wadau wa zao hilo na kwamba tangu Oktoba, 2021 benki hiyo imeshusha viwango vyake vya riba.

“Tumefanya kazi kwa karibu na wakulima, wazalishaji, wasafirishaji, wasindikaji ambao wamechukua mikopo ili kukuza zao la zabibu na kuongeza mnyororo wa thamani. Na mwezi uliopita, tumeshusha viwango vya riba na kufikia asilimia 10,” alisema na kushangiliwa na wadau waliokuwepo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news