Waziri Ummy atangaza neema kwa vikundi vichanga kuhusu mikopo

NA ANGELA MSIMBIRA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mhe Ummy Mwalimu amesema hatamuonea aibu Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye hatatenga na kutoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwa wanawake ndo jeshi la mabadiliko nchini
Akifungua Kongamano la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi na Kijamii Mkoa wa Iringa, Waziri Ummy amesema wananwake ndio wanaolea familia, wanasomesha watoto na kufanya shughuli za maendeleo katika nchi yetu.

Amewaelekeza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutoa mikopo yenye tija na mikopo itakayowawezesha kuanzisha viwanda,kuanzisha biashara na mikopo itakayowezesha kuongeza ajira kwa watu wengine, mambo ya kutoa mikopo kiduchu yamepitwa na wakati.

Amesema kuwa maafisa maendeleo ya jamii wanajukumu la kusimamia na kutoa ushauri kwa vikundi vya akina mama ili waweze kutumia mikopo waliyopata kwa kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo katika jamii
Amesema, wanawake na vijana wana mawazo mazuri ya kuanzisha biashara zao ila sasa wakipeleka maombi kwenye Halmashauri wanaambiwa na Halmashauri hawawezi kupatiwa mkopo hadi wawe na biashara,lakini sheria ya fedha za Serikali za mitaa na kanuni za usimamizi wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu zinaelekeza mikopo itolewe kwa madhumuni mawili; ya kuwawezesha wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kuanzisha shughuli zao au kuendeleza shughuli zao.

“Wananchi wamekuwa hawapewi mikopo kwa kigezo kuwa mikopo haitolewi kwa vikundi vinavyoanzisha biashara, hii haina maana ya utoaji wa mikopo lengo ni kutoa mikopo kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hivyo ninawaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kufuata sheria na taratibu za utoaji wa Mikopo nchini “ amesisitiza Waziri Ummy.

Amesema, watu wana mawazo mazuri ya biashara , wameandika maandiko mazuri ya biashara lakini hawana biashara wanaomba mikopo wanaambiwa lazima na biashara au sehemu za kufanyia biashara, ni kinyume na sheria na utaratibu kwa kuwa kanuni zinasema mikopo itolewe kwa ajili ya kuanzisha biashara au shughuli za ujasiriamali na kuendeleza, hivyo ni ruksa kupata mkopo.
Amewaelekeza Halmashauri kujiridhisha na maandiko ya biashara yanayoletwa na wahusika kama yanarudisha fedha zilizoombwa na kazi hiyo inatakiwa kutekelezwa na maafisa maendeleo ya jamii,

Aidha, amezisitiza Halmashauri kuacha kuweka vikwazo katika suala zima la utoaji wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kupunguza ukiritimba na kuwazungusha wakopaji kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments