Wito wa Tanzania kwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI ya Tanzania imetoa wito kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za kusaidia upatikanaji wa chanjo ya Uviko-19 kwa Watanzania.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam. Waziri Mulamula amewasihi mabalozi hao kuendelea kuungana na Serikali katika jitihada za upatikanaji wa chanjo ya Uviko 19 ambapo amesema kuwa hadi sasa ni watanzania milioni 1.5 wamechanjwa. “Ninawaomba zaidi chanjo nyingine ili watanzania wote waweze kuchanja kwani mwamko wa kuchanja kwa sasa hapa nchini umekuwa mkubwa,” amesema Balozi Mulamula.

Pia Waziri Mulamula amewahakikishia kuwa Tanzania inazingatia masula ya demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria pamoja na kuheshimu haki za binadamu.
Kwa upande wake kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed amesema pamoja na mambo mengine, vikao hivyo vimekuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa majukumu yao hapa nchini.

Nae Waziri wa uchumi wa buluu Zanzibar Mhe. Abdalla Hussein Kombo amesema katika mkutano huo, wamejadili agenda ya uchumi wa buluu ambayo ina vipaumbele vitano ambavyo ni uvuvi na utamaduni, utalii, usafirishaji, usimamizi wa bahari pamoja na nishati.

“Tumewaeleza wenzetu mabalozi vipaumbele vyetu vya uchumi wa buluu na wameonesha nia ya kushirikiana na sisi katika kuendeleza agenda yetu ya Uchumi wa buluu,” amesema Mhe. Kombo.

“Pia tumewaeleza kuwa tumemaliza kupitia sera yetu ya uchumi wa buluu na sasa tumeshatekelez mpango wa utekelezaji na sasa tunataka tuone namna gani sisi na wao tunaweza kuanza kuitekeleza agenda yetu ya uchumi wa buluu,” ameongeza Mhe. Kombo.
Mawaziri walioshiriki katika kikao kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi na Taasisi zao hapa nchini kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi na Taasisi zao hapa nchini katika kikao cha pamoja kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Prof. Shukrani Manya pamoja na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news