Wizara ya Kilimo yazidi kuimarisha uhusiano wa Kimataifa, Profesa Mkenda azifikia fursa Uganda

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amefanya ziara ya kikazi nchini Uganda na kufanya mkutano na Waziri wa Kilimo, Mifugo,Viwanda na Uvuvi, Frank Kagyigyi Tumwebaze pamoja na timu ya wataalam kutoka Tanzania na Uganda siku ya Novemba 23,2021.
Katika ziara hiyo Waziri Mkenda ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye na wataalam wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo na Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma ni mojawapo ya mikoa ya kimkakati katika uzalishaji wa zao la mchikichi.

Mkutano huo una lengo la kuimarisha uhusiano wa Uganda na Tanzania katika Sekta ya Kilimo ili kukuza tija ya uzalishaji wa mazao kwa kutumia mbinu bora za kilimo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti wa kilimo na upatikanaji wa mbegu bora.
Katika mkutano huo Waziri Mkenda ameelezea jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi kwa kuimarisha uhusiano chanya kati ya nchi jirani kama Uganda.

“Tumekuja Uganda kwa kuwa tunafahamu sisi ni ndugu na uhusiano wetu una historia ndefu, Marais wetu wote wawili, Rais Yoweri Kaguta Museveni na Rais Samia Suluhu Hassan wanafanya kazi nzuri ya kuimarisha uhusiano uliopo na kukuza uchumi wa nchi zote mbili,”amesema Waziri Mkenda.

Amesisitizia kuwa, Wizara ya Kilimo ipo katika mkakati kabambe wa kuhakikisha nchi inaondokana na changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula, na kutumia fursa ya ziara hii kujifunza namna ambavyo Uganda imepiga hatua kubwa ya kilimo cha Michikichi, itaongeza hamasa kwa uwekezaji mkubwa wa kilimo hicho nchini na ambapo kitalimwa kwa tija na kupunguza uhaba wa mafuta ya kula kwa kiwango kikubwa na kushusha bei kwa mlaji.
“Katika ziara hii nimeongozana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye, kwa kuwa Kigoma ni mkoa mmojawapo wa kimkakati kwa kilimo cha Michikichi, kuja kwake huku kutawezesha kujionea na kujifunza ili kwenda kuwahamasisha wakulima wetu kulima kwa tija,”ameongeza Profesa Mkenda.

Ziara hiyo pia imehusisha kutembelea mashamba makubwa ya Mchikichi, viwanda vya uchakataji wa mafuta ya mawese na kujifunza mfumo mzima wa ulimaji na utunzaji wa mchikichi na hadi kupata mafuta ya mawese.

Kampuni ya Wilmer yenye matawi katika nchi zaidi ya 25 ina nia ya kuongeza uzalishaji nchini Tanzania katika kuzalisha mafuta yatokanayo na michikichi, alizeti na mazao mengine.
Aidha, kampuni hiyo imejenga kiwanda cha mchele mjini Morogoro chenye uwezo wa kukoboa mpunga tani 200 kwa siku, kilichofunguliwa rasmi na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Mifugo,Viwanda na Uvuvi wa Uganda, Frank Kagyigyi Tumwebaze amemshukuru Waziri Mkenda na timu yake kwa kuamua kutembelea Uganda na kuonyesha undugu na urafiki wa nchi hizi mbili.
Ameongeza kuwa, Uganda iko tayari kuendelea kuimarisha uhusiano na Tanzania katika Sekta ya Kilimo na kutaka wataalam wa kilimo wa nchi zote mbili kuharakisha uundwaji wa Kamati ya Pamoja ya Kilimo (Joint Permanent Committee) ili kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa pamoja katika kilimo yaliyosainiwa Septemba 6, 2019 jijini Dar es Salaam.

“Tumekubaliana nchi zetu kushirikiana katika mambo mbalimbali kwenye sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa mbegu bora,masoko, utafiti na mengineyo. Tumefurahi sana kwa ujio huu wa Waziri wa Kilimo wa Tanzania kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa makabaliano hayo,”amesema Waziri Tumwebaze.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Wilmar anayesimamia Afrika, Bw. Santhosh Pilai, amesema, kampuni hiyo ipo tayari kuongeza uwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania ili kumhakikishia mkulima uhakika wa soko pamoja na kuondoa changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula nchini Tanzania.
“Tumefanya uwekezaji katika nchi zaidi ya 20 Afrika, Asia na Marekani, na kwa Tanzania tumewekeza kiwanda kikubwa pale Morogoro na tunataka kuwekeza zaidi Tanzania. Zaidi ya vijana 400 wameajiriwa katika uwekezaji huo,”amesema Pilai.

Post a Comment

0 Comments