Amref yawezesha asilimia 99 ya WAVIU Simiyu kutumia dawa

NA DERICK MILTON

SHIRIKA la Amref Health Africa limetajwa kuwa moja ya wadau wa Afya katika Mkoa wa Simiyu ambao wamefanikisha mkoa huo kufikia asilimia 99 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kutumia dawa za kufubaza virusi (ARVs).
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila (mwenye skafu) akipata maelezo kutoka kwa wataalamu wa Shirika la Amref Health Africa juu ya shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo mkoani humo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mratibu wa Ukimwi mkoani huo, Oscar Tenganamba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kimkoa ambayo yamefanyika mjini Bariadi.

Tenganamba amesema kuwa, kupitia mradi ambao Amref wanatekeleza mkoani humo wa Afya Kamilifu, wamekuwa wakitekeleza shughuli mbalimbali ambazo zimewezesha mapambano dhidi ya VVU kuendelea kuwa makubwa.

Amesema kuwa, mbali na hilo eneo la watu wote kupima afya zao, Mkoa wa Simiyu umefikia asilimia 89 kati ya 95 ambazo wanatakiwa kufikia ifikapo mwaka 2030, ambapo Amref wameanzisha huduma za upimaji katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya mkoani humo.

Aidha,amesema kuwa asilimia 96 ya wale ambao wanatumia dawa za ARVs kwenye mihili yao, virusi vimeanza kufubaa, ambapo lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2030.
Amesema kuwa, kupitia mradi huo, Amref wamekuwa wakiwafuatilia wale wote wanaotumia dawa na kuwapatia elimu ya kutumia dawa hizo mara kwa mara hali ambayo imewezesha wengi wao virusi kufubaa katika mihili yao.

“Amref pia wamekuwa wakitekeleza huduma za tohara kinga kwa wanaume, lakini pia kupambana katika kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto, ambapo kwa mkoa kiwango cha maambukizi hayo ni asilimia moja, ni moja ya eneo ambalo Amref wamesaidia na tukafikia hapa,” amesema Mratibu huyo.

Mratibu wa Mradi wa Afya Kamilifu mkoani humo uliopo chini ya Amref, Paschal Nyagonde alisema kuwa kupitia mradi huo zaidi ya vituo 90 vya kutolea huduma za Afya mkoa mzima vinatoa huduma za upimaji wa VVU.

Aidha, Nyagonde amesema kuwa mbali na upimaji, kupitia vituo hivyo Amref inatoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wenye VVU ili kuendelea kutumia dawa zaidi na kuwakinga wengine.

“Amref kupitia mradi wetu huu, tumeendelea kutoa elimu kwa vijana mbalimbali juu ya kujikinga na ugonjwa huu, vijana wote wa rika balee wamekuwa wakipewa elimu ya jinsia,” alisema Nyagonde.

Akifunga maonesho hayo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa David Kafulila amewapongeza wadau wote ambao wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi huku akitaka suala la ugonjwa huo kuwa ajenda katika vikao mbalimbali vya maendeleo.

Kafulila amewataka wazazi pamoja na viongozi wa Dini kuendelea kulea watoto katika tabia njema, kwani asilimia kubwa ya watu ambao wameambukizwa na ugonjwa huo ni vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.

“Suala la mapambano dhidi ya Ukimwi liwe ajenda kuu katika vikao vyote vya maendeleo kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa, mapambano lazima yazidi kuwa makubwa kuhakikisha ugonjwa huu unaisha kabisa au maambukizi kupungua,” alisema Kafulila.

Post a Comment

0 Comments