CCM yampongeza Rais Samia kwa mambo matano

NA DOREEN ALOYCE

KATIKA kusherehekea Sikukuu za Krismasi Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa uchapakazi wake,upendo, amani, utulivu na jinsi anavyoendelea kuijenga Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Dodoma Mjini, Meja Mstaafu Johnick Risasa wakati alipokuwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama ambacho ufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ya chama ikiwemo utendaji kazi.

Aidha, Meja Risasi amesema kuwa kupitia mkutano huo wajumbe wote wameridhia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amekuwa mchapakazi hodari kwa kutekeleza Ilani ya chama huku akiweka nchi katika hali ya amani,utulivu, mshikamano,upendo na kuwa nchi ya kuigwa barani Afrika na ulimwenguni kote. 

Amesema kuwa, Rais ameendelea kuifungua nchi kidplomasia na mataifa mengine hali iliyopelekea kuwepo kwa wawekezaji wengi ambao wanakuja kuwekeza na kuinua uchumi wa Taifa.

"Kwetu sisi kama Wana Dodoma tunayo sababu nyingi za kumpongeza Rais Samia kwa namna anavyoendelea kuijenga Dodoma yetu hasa miradi mikubwa ikiwemo uwanja wa ndege,ujenzi wa barabara ya mzunguko,uwanja wa Mpira wa kisasa hali ambayo imeleta maendeleo kwa jamii.

"Pia Rais wetu tunampongeza kwa kutoa fedha Bilioni 2.9 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa zaidi ya 143 na kutoa mwanya kwa wototo kupata elimu ya Sekondari bila wasiwasi hivyo tunapomaliza mwaka tumeona tumpongeze,"amesema Risasi.
Katibu wa chama hicho Wilaya ya Dodoma, Sofia Kibaba amewaeleza wajumbe kuwa ili chama kiweze kusonga mbele wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo huku wakifuata maagizo ya viongozi wao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amesema kuwa wana Dodoma wana faraja kubwa hasa maendeleo yaliyopo kutokana na Rais ambaye amekuwa akionyesha dhamira yake ya kutaka kuendeleza Makao Makuu ya nchi.

"Rais amekuwa wazi kuliunganisha Taifa letu bila kujali dini,ukabila itikadi zetu za vyama jambo ambalo limeendelea kuweka imani kubwa kwa wananchi,"amesema Mavunde.

Amesema kuwa, kwa kushirikiana na wananchi wake atahakikisha anatekeleza zile ahadi alizozitoa wakati akiomba kura kwenye kata zote ikiwemo ujenzi wa shule, barabara,umeme na maji.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wajumbe wa mkutano huo Christina Kamunya pamoja na Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboji wamesema kuwa, kwa kipindi kifupi Rais Samia ameonyesha uhodari kuleta maendeleo.

"Kitendo cha Rais kumwaga madarasa kila kona haijawahi kutokea, hali hiyo itasaidia kuongeza muamko wa elimu hapa nchini,"amesema Diwani Edward.

Post a Comment

0 Comments