Mama Tunu Pinda:Wajane msikate tamaa mnapoondokewa na wenza wenu

NA MWANDISHI MAALUM

MKE wa Waziri Mkuu Mstaafu, Mama Tunu Pinda amewataka wajane wasikate tamaa ya maisha au kujiona wanyonge pale wanapoondokewa na wenza wao.

Ametoa wito huo mwishoni kwa wiki wakati akizungumza na waumini na watu mbalimbali walioshiriki hafla ya chakula cha mchana cha Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Upendo Revival Christian Center (TAG) jijini Dodoma.
Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Mama Tunu Pinda akihutubia waumini wa Kanisa la Upendo Revival Christian Center Area D Dodoma, kabla ya kutoa zawadi kwa wajane na yatima na wahitaji wengine zilizotolewa na kanisa hilo ikiwa ni zawadi kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi. Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki.
Wajane kutoka Veyula wakimsikiliza kwa makini Mama Tunu Pinda alipokuwa akiwahutubia, kabla ya kukabidhiwa zawadi zao kwenye hafla ya chakula cha mchana cha Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Upendo Revival Christian Center Area D Dodoma. 

“Leo nimejifunza jambo kubwa sana hapa kanisani, kanisa limeonesha upendo wa hali ya juu sana kwa kuweza kukusanya idadi ya watu 500 na kula nao chakula,” alisema kabla ya kutoa zawadi kwa wahitaji waliojumuisha wajane, watoto yatima na watoto wa mitaani.

“Natamani hata mimi kufanya jambo kama hili kwani ni upendo wa aina yake, napenda kusema hili ni tukio kubwa na la kuigwa na watu wote,” alisema.

Mama Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo alisema: “Pamoja na kanisa kuhubiri neno la Mungu, pia limeweza kuwajali watu kimwili kwa kushiriki nao chakula pamoja na mahitaji mbalimbali na kuwafanya wafarijike badala ya kujiona wanyonge kwenye sikukuu hii muhimu.”
Mama Tunu Pinda akimkabidhi vifaa vya shule mwanafunzi yatima anayelelewa na kanisa hilo kwenye hafla ya chakula cha mchana cha Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Upendo Revival Christian Center Area D Dodoma.
Mama Tunu Pinda, akimkabidhi begi mwanafunzi yatima anayelelewa na kanisa hilo kwenye hafla ya chakula cha mchana cha Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Upendo Revival Christian Center Area D Dodoma. 

Kanisa hilo lina utaratibu wa kila mwaka kushiriki chakula na watu wenye uhitaji na mwaka huu Kamati ya Dorcas ya Kanisa hilo iliwakusanya wajane 150 kutoka Veyula, watoto yatima 250 kutoka vituo vya Safina (eneo la Ntyuka) na Shukrani (eneo la Kigwe) na watoto waishio katika mazingira magumu wapatao 100 kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Dorcas iliyopo katika kanisa hilo, Bi. Annie Maugo, alisema matatizo makubwa ya kuwepo kwa watoto wa mitaani yanasababishwa na vurugu na migogoro ya kifamilia.

Bi. Maugo alisema kanisa hilo limekuwa na utaratibu kula chakula na kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto waliopo mashuleni na kutoa misaada mbalimbali kwa makundi hayo zenye thamani ya sh. milioni 25.
Mama Tunu Pinda akizungumza na Mama Mchungaji wa Kanisa hilo baada ya kumaliza kutoa zawadi kwenye hafla ya chakula cha mchana cha Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Upendo Revival Christian Center Area D Dodoma.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Upendo Revival Christian Center (T.A.G) lililoko Area D Dodoma, Dkt. Vangast Salum, akimshukuru Mama Tunu Pinda baada ya kumaliza kutoa zawadi kwenye hafla ya chakula cha mchana cha Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa hilo.
Mama Tunu Pinda, akikata keki kwa ajili ya waumini wa kanisa hilo.

“Tumetoa vifaa mbalimbali vya masomo kwa wanafunzi wanaoingia shuleni Januari mwakani na pia tumetoa chakula, sukari, sabuni, mafuta ya kula, miswaki, dawa za meno, vitenge pamoja na mafuta ya kujipaka,” alisema na kuongeza kuwa: “Zawadi nyingine ni mabegi ya shule, madaftari, ream za karatasi, rula, penseli na kalamu za wino.”

Amesema lengo kubwa ni kuyafanya makundi hayo yajisikie kuwa ni sehemu ya jamii kwa kujumuika na wenzao ili nao wawe na furaha kama zilivyo familia nyingine.

Naye, Mdala Yulia ambaye ni miongoni mwa wajane walioshiriki chakula cha pamoja kanisani hapo amelishukuru kanisa kwa upendo ambao wameuonesha. “Napenda kulishukuru kanisa kwa kuwa na maono ya kutujali sisi wajane na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na zaidi ni pale ambapo wanatuwezesha kupata mahitaji.
Mama Tunu Pinda, akimlisha keki mmoja wa wajane wa kanisa hilo.
Wanakwaya wa Kanisa hilo wakitoa burudani kwa waumini wa kanisa hilo. (Picha na Deus Mhagale).

“Pamoja na hayo, wamekuwa wakiwasaidia watoto wetu katika kuwawezesha vifaa vya shule jambo ambalo linatutia moyo kwani tunajengwa kiroho, kimwili na kiakili,” alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news