Mheshimiwa Dugange:TARURA imewekeza Bilioni 28/- mkoani Mbeya

NA FRED KIBANO

SERIKALI imesema zaidi ya shilingi Bilioni 28 zilitengwa kwa ajili ya kutengeneza na kukarabati barabara na miundombinu yake ili ziweze kupitika kwa muda wa mwaka mzima na kuinua shughuli za kiuchumi kwa watanzania mkoani Mbeya.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Festo Dugange ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya barabara za halmashauri ambazo zipo chini ya Wakala wa Barabara wa Mijini na Vijijini (TARURA) kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Mbeya.

Dkt. Dugange amesema, kwa mwaka 2020/2021 chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ilipeka shilingi Bilioni 17,958,599,000 ili kujenga kilomita 760.13 za viwango vya lami na changarawe mkoani Mbeya ikiwa ni pamoja na madaraja 31 na makaravati 165.

Aidha, amesema mwaka 2019/2020 jumla ya shilingi 11,412,388,842.26 kwa ajili ya matengenezo ya Barabara za Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani Mbeya ambapo fedha hizo zimetokana na Ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fedha za maendeleo na Bajeti ya kawaida ya Serikali.
Aidha, Dkt. Dugange amesema, mwaka 2019/2020 jumla ya barabara zinazofanyiwa matengenezo kwa viwango mbalimbali vya lami na changarawe ni kilomita 553.31, ikijumuisha makalavati 106 na madaraja19 ambapo njia hizo zinasaidia barabara kuu zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi kuhakikisha shughuli za kiuchumi kama usafirishaji wa mazao na huduma za kijamii hazikwami katika kipindi chote cha majira ya mwaka.

Amesema, kiasi cha fedha na umbali wa kilomita kwenye Mamalaka za Serikali za Mitaa mwaka 2019/2020 ni kuwa Halmashauri ya Busokelo ilipata kilomita 44.2, zenye thamani ya shilingi 1,615,846,290.61, Halmashauri ya Chunya kilomita 56.8, zenye thamani ya shilingi 1,370,511,290.61, Halmashauri ya Kyela kilomita 104.03, zenye thamani ya shilingi 1,139,445,220.61, Halmashauri ya Mbarali kilomita 71.25, zenye thamani ya shilingi 550,380,290.61, Jiji la Mbeya kilomita 93.41, zenye thamani ya shilingi 3,063,028,980.95,Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kilomita 44.6, zenye thamani ya shilingi 1,423,792,478.26, na Halmashauri ya Rungwe kilomita 139.02 na zina thamani ya shilingi 1,249,384,290.61
Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini ndio watekelezaji wa miradi ya barabara kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na husimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa.

Post a Comment

0 Comments