Miaka 60 ya Uhuru: Haya ndiyo usiyoyajua kuhusu Ofisi ya Rais-TAMISEMI

NA ANGELA MSIMBIRA-OR TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, huduma za jamii zimeimarika na kusogezwa kwa jamii.
Akitoa taarifa kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma Novemba 30,2021 kuhusu mafanikio, changamoto na muelekeo wa Tawala za Mikoa na Serikai za Mitaa katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru,Mheshimiwa Waziri Ummy amesema katika kuimarisha ugatuaji wa madaraka kwa wananchi Serikali imekuwa ikisogeza huduma za kijamii kwa wananchi ambazo zimeimarika mara dufu.

Waziri Ummy ameendelea kufafanua kuwa katika kusogeza uhuduma karibu na wananchi, maeneo ya kiutawala yameongezeka kutoka mikoa 15 ya baada ya Uhuru kutoka kwenye majimbo nane ya mwaka 1966, ambapo sasa kuna mikoa 26 huku halmashauri zimefika 184 kutoka 45.

Amesema, wakati wa Uhuru hakukuwa na Halmashauri za Majiji lakini kwa sasa kuna Halmashauri za Majiji 6, kulikuwa na Halmashauri ya Manispaa moja ya Dar es Salaam na sasa kuna Halmashauri za Manispaa 20, Halmashauri za Miji zilikuwa 9 na sasa Halmashauri za Miji ni 21 na Halmashauri za Wilaya zilikuwa 10 na sasa zipo Halmashauri za Wilaya 137.

Waziri Ummy amesema hadi mwaka 2010 tulikuwa na kata 3,952, vijiji 10,351, mitaa 2,650, vitongoji 55,914. Hivi sasa kuna Ttrafa 570, kata 3,956, vijiji 12,318, vitongoji 64,361 na mitaa 4,263.

Kuhusu ushamirishaji wa demokrasia na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo, Waziri Ummy amesema, tangu Serikali za Mitaa zilivyorejeshwa mwaka 1982 chaguzi katika ngazi ya Kata, Vijiji na Mitaa na Vitongoji zimefanyika kwa ufanisi.

Amesema, kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuibua miradi yao na hadi kufikia June 2021, kuna maboma ya Zahanati 2,378 yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Katika Sekta ya Elimu, Waziri Ummy amesema kwenye elimu wananchi wameanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 10,300 katika halmashauri mbalimbali na kati ya hayo Serikali ikatoa fedha ya tozo ya mawasiliano shilingi bilioni 7 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 560.

Kuhusu usimamizi wa Rasilimali Fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ummy alisema katika miaka 60 ya Uhuru, Halmashauri zimepiga hatua ya ongezeko la mapato ya ndani.

Katika kipindi cha miaka kumi makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani yaliongezeka kutoka sh. 175,084,789,727 mwaka wa fedha 2010/11 hadi Sh 814,960,990,077 kwa mwaka wa fedha 2020/21, ongezeko hilo ni Sh 639,876,200,350 sawa na asilimia 365.46.

“Aidha, makusanyo ya mapato ya ndani katika kipindi hicho yaliongezeka kutoka shilingi 158,279,374,601 mwaka 2010/11 hadi shilingi 757,054,979,113 mwaka 2020/21. Ongezeko hilo ni shilingi 598,775,604,512 sawa na asilimia 378.30. Mafanikio ya makusanyo ya mapato ya ndani yametokana na Serikali kuimarisha usimamizi wa matumizi ya mifumo ya kielektroniki,”amesema.


TULIKOTOKA NA MWELEKEO KWA KINA 

Waziri Ummy Mwalimu anasema kuwa, nchi yetu ilipata Uhuru Desemba 9,1961 ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza aliunda Wizara ya Serikali za Mitaa na Kumteua Mheshimiwa Job Lusinde kuwa Waziri wa kwanza kuongoza Wizara hii.

Akifuatiwa na Mawaziri 19 ikijumuisha wanawake wanne (4) akiwemo Waziri wa sasa Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu.

Tangu mwaka 1961 hadi sasa Ofisi ya Rais –TAMISEMI imekuwa ama inajitegemea yenyewe au kuwekwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu au kwenye Ofisi ya Rais kama ilivyo sasa. Uamuzi wa wapi inawekwa umekuwa ukifanyika ili kuimarisha utendaji wa Ofisi hii.

Ofisi ya Rais TAMISEMI ni Wizara pekee ambayo Makao Makuu yake yalianzia jijini Dodoma tangu mwaka 1973 pale Serikali ilipotangaza Makao Makuu ya Serikali kuwa ni Dodoma. Uwepo wa Makao Makuu Dodoma ulikua na lengo la kutoa fursa kwa wananchi na kwa wadau wake wakuu hususan Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufika Dodoma kwa urahisi wanapofuata huduma mbalimbali.

Madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka Madaraka kwa Wananchi (D by D) ambapo chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Sura ya 8, Ibara ya 145 na 146. Lengo ni kuimarisha madaraka kwa wananchi na kuwashirikisha katika kufanya maamuzi.

Wakati Nchi yetu inapata uhuru wake kulikuwa na majimbo nane ya Utawala ambayo yaliritihiwa toka utawala wa kikoloni wa Kiingereza mwaka 1966. Majimbo haya ni Jimbo la Kati, Jimbo la Mashariki, Jimbo la Ziwa, Jimbo la Kaskazini, Jimno la Nyanda za Juu Kusini, Jimbo la Tanga, Jimbo la Magharibi na Jimbo la Ziwa Magharibi. Rais wa kwanza Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa Mamlaka aliyopewa aliunda Mikoa 15 na kuondoa utaratibu wa mgawanyo wa nchi katika Majimbo. Mikoa ya mwanzo ni Arusha, Pwani, Dodoma. Tanga, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora

Mnamo mwaka 1972 Serikali ilifuta Mamlaka hizi na kuanzisha mfumo wa Madaraka Mikoani. Mfumo huu ulizifanya Serikali za Mitaa kuitegemea Serikali Kuu kwa kila jambo kutokana na wananchi kutoshiriki katika maamuzi na pia katika shughuli za maendeleo. Kutokana na hali hii, Mamlaka za Miji zilirejeshwa mwaka 1978 na mamlaka za wilaya zilirejeshwa mwaka 1984.

2.0 MUUNDO NA MAJUKUMU YA OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

Kwa sasa Muundo na Majukumu ya Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Ofisi ya Rais - TAMISEMI) yapo kwa Hati ya Rais ya Mgawanyo wa Majukumu ya Wizara iliyotolewa tarehe 07 Mei, 2021. Ofisi hii inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Hati ya Rais ya Mgawanyo wa Majukumu ya Wizara na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Ofisi ya Rais - TAMISEMI ina Idara kumi na moja (11) na Vitengo sita (6) na inasimamia Taasisi Saba (7) ambazo ni Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Shirika la Elimu Kibaha, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, Shirika la Masoko ya Kariakoo na Tume ya Utumishi wa Walimu.

Aidha, Ofisi ya Rais-TAMISEMI inasimamia utekelezaji wa Sera mbalimbali za Kisekta na Sheria ya Tawala za Mikoa Sura 97, Sheria ya Serikali za Mitaa Mamlaka za Wilaya Sura 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa Mamlaka za Miji Sura 288. Katika kutekeleza majukumu hayo, Ofisi ya Rais - TAMISEMI ina Mpango Mkakati unaoiongoza katika kutekeleza majukumu yake. Mpango huo una Dira na Dhima zifuatazo: -

2.1 Dira

Kuwa na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zenye uwezo wa kuboresha huduma kwa wananchi.

2.2 Dhima

Kuratibu, kuwezesha na kusimamia Tawala za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi kwa kutoa Sera, Miongozo na maelekezo ili kuwepo na huduma zilizo boreshwa.

3.0 UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA OFISI YA RAIS TAMISEMI, MAFANIKIO YALIYOPATIKANA TOKA UHURU HADI SASA

Toka kuanzishwa kwake, Wizara hii inayosimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imepata mafanikio mbalimbali. Katika muktadha huu nitajikita katika maeneo makubwa matano ambayo ni:-

- Kuimarisha utawala bora na kugatua madaraka kwa wananchi

- Kuimarisha Elimu Msingi na Sekondari

- Kuboresha utoaji wa Huduma za AfyaMsingi

- Kuimarisha Miundombinu ya Barabara na;

- Kuwawezesha wananchi kiuchumi

3.1 Utawala Bora na Ugatuaji wa madaraka kwa wananchi

i. Ongezeko la maeneo ya kiutawala

Katika kuimarisha ugatuaji wa madaraka kwa wananchi Serikali imekuwa ikiongeza maeneo ya kiutawala ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Hadi Sasa Nchi yetu ina Mikoa 26 kutoka Mikoa 15 iliyokuwepo baada ya uhuru, Baada ya uhuru Halmashauri zilikuwa 45 na hadi kufikia mwaka 2009 zilikuwa Halmashauri 129 na zimeendelea kuongezeka hadi kufikia 184 mwaka 2021.

Wakati wa Uhuru hakukuwa na Halmashauri za Majiji, hivi sasa kuna Halmashauri za Majiji 6, kulikuwa na Halmashauri ya Manispaa moja ya Dares Salaam na sasa kuna Halmashauri za Manispaa 20, Halmashauri za Miji zilikuwa 9 na sasa Halmashauri za Miji ni 21 na Halmashauri za Wilaya zilikuwa 10 na sasa zipo Halmashauri za Wilaya 137.

Aidha, hadi mwaka 2010 tulikuwa na Kata 3,952, Vijiji 10,351, Mitaa 2,650, Vitongoji 55,914. Hivi sasa kuna Tarafa 570, Kata 3,956, Vijiji 12,318, Vitongoji 64,361 na Mitaa 4,263. Hatua hii inaimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kiiutawala kwa wananchi.

ii. Ushamirishaji wa Demokrasia na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo

Tangu Serikali za Mitaa zilivyorejeshwa mwaka 1982 chaguzi katika ngazi ya Kata, Vijiji na Mitaa na Vitongoji zimefanyika kuanzia mwaka 1983, 1988 na 1994. Kwa chaguzi zilizofanyika mwaka 1994, 1999, 2004, 2009, 2014, 2019 hazikujumuisha Chaguzi za Madiwani kwa kuwa kuanzia mwaka 1994 Chaguzi za Madiwani zilianza kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa sababu ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vilivyoanza mwaka 1992.

Aidha kumekuwa na Mwamko mkubwa wa Wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuibua miradi yao na hivyo wakati mwingine kuzidi kasi ya Serikali katika kukamilisha miradi katika maeneo mbalimbali. Mfano hadi kufikia June 2021, kuna maboma ya Zahanati 2,378 yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi. Kwa upande wa sekta ya Elimu wananchi wameanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 10,300 katika Halmashauri mbalimbali na kati ya hayo Serikali ikatoa fedha ya tozo ya mawasiliano sh. bilioni 7 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 560.

iii. Uimarishaji wa Serikali za Mitaa

Kwa lengo la kuziimarisha Serikali za Mitaa na kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya hatua hizi ni kuanzishwa kwa Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ulioanzishwa mwaka 1998 ambao ulilenga katika kupeleka madaraka kwa Wananchi (D by D). Sambamba na hilo, Serikali ilitoa Tamko la Kisera la Ugatuaji wa Madaraka kama njia muafaka ya kufikisha na kuharakisha maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi na kuinua utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dhana hii imejengwa kwa misingi ya kutoka kwenye mfumo wa Madaraka ya Serikali Kuu kuwa na maamuzi yote, na Serikali za Mitaa kuwa Mtekelezaji tu (yaani Mwagizaji na Mtekelezaji) kwenda katika mfumo wa Serikali za Mitaa wenye Mamlaka ya Kisheria ya kuamua mambo katika eneo lao na kuyatekeleza. Hivyo, kuwa na mfumo wa mahusiano ya majadiliano katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Ugatuaji wa Madaraka kwa wananchi unalenga kuzipatia Mamlaka za Mitaa uhuru wa kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu utoaji wa huduma kwa wananchi walio katika Mamlaka zao na kuwashirikisha katika kujiletea maendeleo na ustawi wao. Aidha, Tawala za Mikoa zimepewa mamlaka ya kusimamia na kuratibu shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora na endelevu kwa wananchi.

vi. Usimamizi wa Rasilimali Fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa

Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru Halmashauri zimepiga hatua ya ongezeko la mapato ya ndani. Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2010/11 makisio ya mapato ya ndani yalikuwa shilingi 175,084,789,727. Makusanyo halisi yalikuwa shilingi 158,279,374,601 sawa na asilimia 90.4. 

Katika mwaka wa fedha 2020/21 Halmashauri zilikasimiwa kukusanya shilingi 814,960,990,077 na makusanyo halisi ni shilingi 757,054,979,113 sawa na asilimia 93. 

Katika kipindi cha miaka kumi makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani yaliongezeka kutoka shilingi 175,084,789,727 mwaka wa fedha 2010/11 hadi shilingi 814,960,990,077 kwa mwaka wa fedha 2020/21. Ongezeko hilo ni Shilingi 639,876,200,350 sawa na asilimia 365.46. 

Aidha, makusanyo ya mapato ya ndani katika kipindi hicho yaliongezeka kutoka shilingi 158,279,374,601 mwaka 2010/11 hadi shilingi 757,054,979,113 mwaka 2020/21. Ongezeko hilo ni shilingi 598,775,604,512 sawa na asilimia 378.30. Mafanikio ya makusanyo ya mapato ya ndani yametokana na Serikali kuimarisha usimamizi wa matumizi ya mifumo ya kielektroniki.

3.2 Sekta ya Elimumsingi

Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kipindi cha miaka sitini iliyopita imefanya maboresho mbalimbali katika Elimumsingi. Lengo mojawapo la maboresho hayo ni kuongeza upatikanaji, ubora na usawa katika elimu.

Elimu Kabla ya Uhuru hadi 1961

Katika kipindi hiki Elimu ilitolewa kwa watu wachache kwa lengo la kupata maafisa wachache ambao wanaweza kusaidia katika shughuli mbalimbali za utawala na kuandaa watu kwa ajili ya kushika uongozi wa nchi. 

Hadi mwaka 1961, kulikuwa na Shule za Msingi 3,270 zilizokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 450,626. Shule hizo ziligawanywa kwa matabaka ya rangi ambapo kati ya Waafrika 9,869,000 wanafunzi 431,056 walipata nafasi ya kusoma katika shule 3,115 na kati ya wananchi Wasio Wafrika 150,000 wanafunzi 19,570 walipata nafasi ya kusoma katika shule 155.

Kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuiwa na Serikali kuanzia Uhuru hadi sasa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni pamoja na:-

i. Idadi ya shule za Msingi za Serikali zimeongezeka kutoka 3,270 mwaka 1961 hadi 16,656 mwaka 2021. Aidha, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 486,470 mwaka 1961 hadi 10,687,593 mwaka 2021. Walimu wameongezeka kutoka 9,885 mwaka 1961 hadi 171,993 mwaka 2021.

ii. Shule za Sekondari zimeongezeka kutoka 39 mwaka 1961 hadi 4,002 za Serikali mwaka 2021. Aidha, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 2,379,945 mwaka 2021. Walimu wameongezeka kutoka 764 mwaka 1961 hadi 87,992 mwaka 2021.

iii. Shule za Elimu Maalum zimeongezeka kutoka nne (4) za wamisionari (Tabora, Buigiri, Irente na Uhuru Mchanganyiko mwaka 1961 hadi kufikia 746 mwaka 2021. Aidha, kuna Elimu Jumuishi katika shule zote za msingi. Idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum imeongezeka kutoka 1,000 mwaka 1960 hadi 70,265 mwaka 2021.

iv. Utoaji wa Elimumsingi bila Malipo unazingatia Ibara ya 3.1.5. ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.

Kiasi cha shilingi bilioni 23.8 zinatolewa kila mwezi kuanzia mwezi Disemba, 2015 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa Mpango wa Elimumsingi bila Ada na shilingi bilioni 3.0 zinapokelewa Baraza la Taifa la Mitihani kwa ajili ya shughuli za Mitihani. Aidha, kuanzia mwezi Oktoba 2021 Serikali imepeleka Shilingi bilioni 26.00 kwa ajili ya uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari nchini.

Kuanzia Disemba, 2015 mpaka sasa Serikali imepeleka jumla ya Shilingi trilioni 1.43. kwa ajili ya kugharamia Mpango wa Elimumsingi bila Malipo. Fedha hizi zimekuwa zikipelekwa katika shule moja kwa moja na kuwafikia wanufaika.

Mpango wa Elimumsingi bila malipo umesaidia kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kutokana na kuondolewa kwa vikwazo. Katika mwaka 2016 jumla ya wananfunzi 3,335,637 waliandikishwa, kati ya hao wanafunzi 1,013,310 wa elimu ya awali, 1,896,584 wa darasa la kwanza na wanafunzi 425,743 wa kidato cha kwanza. Mwaka 2021 jumla ya wananfunzi 3,469,275 waliandikishwa, kati ya hao wanafunzi 1,198,564 wa elimu ya awali, 1,549,279 wa darasa la kwanza na wanafunzi 721,432 wa kidato cha kwanza.

3.3 Sekta ya Afya

Mwaka 1961, kulikuwa na Vituo vya kutolea huduma za Afya 1,343 vilivyokuwa na idadi ya vitanda 18,832 nchini. Serikali za Mitaa ilikuwa inamiliki Vituo vya Afya na Zahanati 737 pekee zenye vitanda 1,795. 

Watumishi wa kada mbalimbali za Afya walikuwa 3,172 kati yao Madaktari walikuwa 580, Madaktari wa Meno 30, Wasaidizi Madaktari wa Meno 19, Wafamasia 50,Wasaidizi Wafamasia 38, Tabibu 402, Wauguzi 1,999, Wateknolojia Maabara 3, Wasaidizi Maabara 49 na Wataalam wa Mionzi 2. Aidha mwaka 1961 watumishi waliofuzu Shahada ya Udaktari walikuwa 400 kati yao Watanzania wakiwa 20 pekeee

Mafanikio

i. Zahanati na vituo vya afya vimeongezeka kutoka 737 mwaka 1961 hadi 5,696 (Vituo vya afya 630 na zahanati 5,066) vya Serikali za Mitaa.

ii. Hospitali zinazotoa huduma zimefikia 142 mwaka 2021 wakati Serikali za Mitaa hazikuwa na hospitali mwaka 1961.

iii. Vituo vya Afya vinavyotoa huduma za upasuaji zimeongezeka kufikia 415 wakati hapakua na kituo kinachotoa huduma za upasuaji mwaka 1961.

3.4 Sekta ya Miundombinu ya Barabara

3.4.1 Miundombinu ya Barabara zinazosimamiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa

Wakati wa Uhuru mtandao wa barabara ulikuwa na jumla ya kilometa 33,600 zilizojumuisha kilometa 16,000 zilizokuwa zikitambuliwa kama Barabara Kuu za Nchi na za Kawaida (Territorial Main and Local Main Roads) na kilometa 17,600 zikiwa ni Barabara za Wilaya (District Roads).

Hata hivyo mwaka 2006, kulifanyika zoezi la kuhakiki wa hali ya barabara nchini zilizochini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Local Government Roads Inventory and Condition Survey - LG-RICS). Katika zoezi hili barabara zilizoainishwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali na kuingizwa kwenye Sheria ya Barabara namba 13 ya 2007 zilikuwa na urefu wa kilomita 56,625. Mtandao huu ulihuishwa na kufikia barabara zenye urefu wa kilomita 108,946 ambazo zilihamishiwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini (TARURA) pale ilipoanzishwa mwezi Julai, 2017.

Mwaka wa fedha 2019/20, zoezi la kuhakiki upya mtandao wa barabara zilizo chini ya TARURA lilifanyika na barabara zilizobainishwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali zina urefu wa kilomita 144,429.77 ambapo kati ya hizo barabara zenye hali nzuri na Wastani ni 53.37 na barabara zilizo katika hali mbaya ni wastani wa 46.63.
Aina na hali ya barabara zilizo chini ya TARURA; Chanzo: DROMAS data June, 2021


Mtandao wa barabara za wilaya umeongezeka kwa urefu wa kilomita 126,829.77 kutoka kilometa 17,600 zilizokuwepo mwaka 1961 hadi kufikia kilometa 144,429.77 mwaka 2021

Kulinganishwa na takwimu zilizochukuliwa 2006, mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 1,325 hadi kilomita 2,404.90 ikiwa ni ongezeko la kilometa 1,079.41 sawa na asilimia 81.47. na Mtandando wa barabara za changarawe Kumekuwepo na ongezeko la barabara za Changarawe kutoka kilometa 22,088.79 hadi kilometa 29,166.57 sawa na ongezeko la kilometa 7,077.78 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 32.04. Kuongezeka kwa urefu wa mtandao wa barabara na kuongezeka kwa barabara za lami na changarawe ni kiashiria cha maendeleo katika nchi kwani barabara ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

- Madaraja yameongezeka kutoka 2,960 mwaka 2006 hadi kufikia madaraja 3,191 na makalvati yameongezeka kutoka 67,992 hadi 69,317.

- Kumekuwepo na ongezeko la bajeti ya ujenzi na matengenezo ya barabara kutoka Shilingi bilioni 94.020 katika mwaka wa fedha 2011/12 hadi Shilingi Bilioni 966.90 katika mwaka wa fedha wa 2021/22.

- Serikali iliunda Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini – TARURA ulianzishwa na kuanza kazi rasmi tarehe 01 Julai, 2017. Maeneo mengine ni kuanzishwa kwa TARURA ambayo kazi yake mahususi ni kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara na madaraja, ambapo imejengewa uwezo kwa kupatiwa Wataalam na Vitendea Kazi ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2021/22, kila Halmashauri itakuwa na gari la usimamizi.

3.4.2 Miundombinu ya Usafiri wa Umma Mijini

Kabla ya kuwasilisha mafanikio ya sekta hii, naomba kufanya marejeo kwa ufupi sana kuhusu sekta ya usafiri wa umma mijini. Sekta hii ilianza kupewa kipaumbele hata kabla ya uhuru wetu, ambapo mwaka 1949 Serikali ya Mkoloni iliunda kampuni ya Dar es Salaam Motor Transport (DMT) kwa ajili ya kutoa usafiri wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam. Huduma hii iliendelea hivyo hata baada ya uhuru wetu wa mwaka 1961 chini ya Serikali ya Serikali yetu.

Aidha, kati ya mnamo mwaka 1967 hadi 1970, Serikali ilipanua zaidi wigo kwa kuweka kipaumbele na mpango kabambe kwa ajili ya kuboresha usafiri wa umma kwenye miji yote nchini ambapo awamu hii kampuni ya DMT iligawanywa na kuunda Kampuni mbili za Umma. 

Kwanza, ni Shrika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa jili ya usafiri wa umma Mkoani Dar es Salaam. 

Pili, ni Kampuni ya Mabasi ya Taifa (KAMATA) kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri wa umma kutoka na kuingia Mkoani Dar es Salaam kwenda na kurudi Mikoa yote ya Tanzania. Juhudi hizi za Serikali zilichangia kuhakikisha kuna uwepo wa huduma ya usafiri wa mijini. 

Hata hivyo, kufuatia ongezeko la kasi la uhitaji wa huduma hii, hususani katika Mkoa wa Dar es Saalaam, hata baada ya kuishirikisha sekta binafsi katika ya kipindi cha mwaka 1983 hadi sasa, kwa kuanzia, Serikali ilianzisha Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) hapo mwaka 2007.

Mafanikio

Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka kupitia Wakala wa DART 2007 ni pamoja na:-

(i) Ujenzi wa barabara maalum kwa ajili ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kutoka kilomita sifuri (0 km) kipindi tunapata uhuru hadi kufikia kilomita 20.9 mwaka 2016 na ujenzi wa kilomita 23.6 unandelea ukiwa katika ufanisi wa asilimia 38.4 ambapo barabara hii itakamilishwa ifikapo Machi 2023. 

Aidha, ujenzi wa barabara nyingine za mradi zenye urefu wa kilomita 109.74 upo kweye hatua mbalimbali na ifikapo mwaka 2025 zitakuwa zimekalika kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyoelekeza.

(ii) Mradi umepunguza muda wa safari toka masaa matatu kabla ya kuanza mradi hadi wastni wa dakika arobaini na tano (45) kwa safari moja hivyo wananchi kuwezeshwa kuwahi katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi zinazoongeza tija kwenye Pato la Taifa.

(iii) Aidha, kumekuwepo na ongezeko la watumiaji wa usafiri wa umma kupitia mradi wa DART ikiwa ni kutoka abiria 76,000 kwa siku wakati mradi ulivyoanza kutoa huduma Mei 2016 hadi kufikia abiria 200,000 kwa siku mwaka 2018 kabla ya kupata changamoto za kiundeshaji n idadi hiyo kushuka hadi wastani wa abira 100,000 kwa siku mwaka 2020 ambapo baada ya maboresho yanayoendelea, hivi sasa wastani wa abria wapatoa 160,000 wanatumia usafiri huu kwa siku.

(iv) Mradi umechochea matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye maendeleo ya sekta ya usafiri wa umma ambapo mradi umetoa fursa kwa Wataalam wetu wa ndani kusanifu na kuujenga Mfumo wa Kieletroniki wa Usimamizi na Ukusanyaji Nauli (Automated Fare Collection System-AFCS) unaomilikiwa na Serikali na kwamba mfumo huu utafungamanishwa na Mfumo wa Kuongozea Magari (Intelligent Transport System-ITS) ikiwa ni sehemu ya maboresho endelevu ya huduma hii kwa wananchi waishio mijini.

(v) Kiasi cha Shilini milioni 127.57 kilikusanywa mwaka 2008/09 hadi kufikia kiasi cha Shilingi bilioni 4.23 mwaka 2019/20 kabla ya kushuka hadi kufikia Shilingi bilioni 3.3 mwaka 2020/21 kama mapato ya yatokanayo na tozo ya kutumia miundombinu ya DART na vyanzo vyanzo vingine. 

Aidha, tangu mwenzi Agosti 2021, mapato ya Serikali yatokanayo na tozo hiyo yameongezeka kutoka Shilingi milioni 8.1 hadi Shilingi milioni 20.04 kwa siku (ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 147.35). 

Hivyo, Serikali inategemea kukusanya Shilingi bilioni 11.2 kutokana na tozo hiyo na vyanzo vingine. Vile vile, mradi umechangia mapato mengine ya Serikali kupitia kodi ya Serikali na iyotokana na huduma inayotolewa na kutengeneza ajira ya moja kwa moja kwa watu wapatao 1,051.

(vi) Kuchangia ujenzi wa taswira nzuri ya Tanzania katika duru za Kimataifa ambapo mradi ilitambuliwa na kupata tuzo mbili za Kimataifa. Tuzo ya kwanza ni ile ya Sustainable Transport Award na tuzo ya pili ni ile ya C40 Cities Bloomberg Philanthropies Award zilizotolewa mwaka 2018.

3.4.3 Ujenzi wa Miundombinu ya utoaji huduma kwa jamii

Aidha, kupitia miradi ya kimkakati Serikali imefanikiwa kujenga Stendi 19 za mabasi za kisasa, masoko 15, machinjio 5, madampo ya kisasa 8, maeneo ya kupumzikia 4 na maegesho ya malori 4.

3.5 Kuwawezesha Wananchi kiuchumi

Kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha wananchi kiuchumi hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. 

Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani zimekuwa zikitoa mikopo kwa vikundi mbalimbali vya kiuchumi. 

Mwaka 2015/16 jumla ya shilingi bilioni 6.69 zilitolewa kwa ajili ya mikopo kwa vikundi 4,037 vyenye jumla ya watu 40,657 kati yao wanawake ni 24,094, vijana 16,547 na watu wenye ulemavu 16. Mwaka 2020, kiasi cha shilingi bilioni 56.12 zilitolewa kwa ajili ya mikopo kwa vikundi 12,962 vyenye watu 150,477 kati ya hao wanawake ni 96,774, vijana 45,356 na watu wenye ulemavu 8,347. 

Hivyo kufanya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 145.83 kutolewa kuanzia mwaka 2015 – 2020 na kunufaisha vikundi 47,309 vyenye watu 490,815 ambapo wanawake ni 318,616, vijana ni 155,781 na watu wenye ulemavu ni 16,418. 

Mikopo hiyo imechangia kukuza uwekezaji mdogo na mkubwa na kuongeza kipato cha wananchi. Aidha, kuanzia mwaka wa fedha 2019/20, mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu inatolewa bila riba.

Kwa mwaka huu wa fedha 2021/22 Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepanga kutoa jumla ya shilingi Bilioni 67.6 kama Mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.

3.6 Miundombinu ya TEHAMA

Kuanzia mwaka 1961 mpaka 1999, hakukuwa na matumizi ya mifumo ndani ya Ofisi hii. Maboresho makubwa ya kimiundombinu yalifanyika na kuweza kuunganisha Mikoa yote 26 na Halmashauri zote 184 zilizokuwepo wakati huo kuja sehemu moja (kompyuta kuu). 

Maboresho haya ya miundombinu yaliongeza ufanisi wa kazi haswa katika mawasiliano na kupunguza gharama hasa za uwasilishajiwa taarifa

i. Kuanzishwa kwa mifumo ya TEHAMA, ambayo imeongeza udhibiti, usimamizi na ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za kisekta.

ii. Kupunguza gharama za uendeshaji na muda wa kazi husika.

iii. Kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani

iv. Kuongeza ufanisi katika mipango na bajeti za serikali.

4.0 CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA

Pamoja na mafanikio makubwa, zipo changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo:-

4.1 Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi

i. Wananchi katika maeneo mengi kuhitaji kuongeza maeneo ya Utawala. Mfano uanzishwaji wa Vijiji, Kata, Mitaa na Halmashauri mpya, Wilaya na Mikoa

ii. Kufanyika kwa chaguzi kwa wakati tofauti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Madiwani, Vijiji, Mitaa na Vitongoji.

iii. Mamlaka za Serikali za Mitaa kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu kwa zaidi ya wastani wa asilimia 88; na

iv. Ushirikwaji mdogo wa wananchi katika kupanga vipaumbele vyao vya , maendeleo.

v. Uwezo mdogo wa baadhi ya Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato

vi. Baadhi ya halmashauri kushindwa kuandaa maandiko ya miradi( mfano miradi ya kimkakati)

vii. Kuendelea kuajiri wataalam wa fani mbalimbali katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuwajengea uwezo wataalam waliopo.

viii. Kuimarisha Tawala za Mikoa ili ziweze kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake

ix. Kukamilisha miundombinu ya maeneo mapya ya utawala.

x. Halmashauri kuhakikisha zinakusanya mapato ya kutosha ili ziweze kujitegemea

xi. Halmashauri zinazokusanya mapato ya ndani yasiyolindwa zaidi ya Shilingi bilioni 5 zihakikishe zinachangia asilimia 10 ya mapato hayo kwa ajili ya miundombinu ya barabara.

xii. Halmashauri zinazokusanya mapato ya ndani yasiyolindwa pungufu ya Shilingi bilioni 1 zihakikishe zinaongeza vyanzo vipya vya mapato ili kupunguza utegemezi na

xiii. Kuendelea kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza udhibiti wa matumizi na kuhakikisha matumizi yanafanywa kwenye shughuli zenye tija kwa wananchi

Mwelekeo

i. Serikali kuangalia uwezekano wa kufanya chaguzi wa Serikali za Mitaa kufanyika kwa wakati mmoja. Mwezi huu Novemba 2021 Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na TAMISEMI walikutana kujadili namna bora ya kufanya ucjhaguzi huu kwa wakati mmoja.

ii. Serikali kuendelea kuratibu uanzishaji wa maeneo ya Utawala ili kufikia lengo la kusogeza huduma kwa Wananchi ikiwemo kufungua miundombinu ya barabara, umeme, maji na huduma nyignine;

iii. Kuimarisha ukusanyaji wa Mapato katika mamlaka za Serikali za Mitaa na kudhibiti Matumizi ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato. Aidha, Halmashauri zinasaidiwa na kujengewa uwezo ili kuongeza wigo na kubuni vyanzo vipya vya mapato; na

iv. Kuhakikisha Halmashauri ambazo zinakusanya zaidi ya bilioni 5 kwa mwaka wajitegemea katika kutoa huduma za jamii badala ya kusubiri Ruzuku ya Serikali kuu. 

Aidha kwa Halmashauri ambazo zinakusanya juu ya bilioni 1 na chini ya bilioni 4 zikusanye lengo la bilioni 4 na kuendelea ili kuweza kutoa huduma za bora kwa wananchi. Vilevile Halmashauri zinazokusanya chini ya bilioni 1 kuongeza jitiahada ili kukusanya bilioni 1 hadi bilioni 4.

v. Serikali kuendelea kuunga mkono jitihada za wananchi katika miradi waliyoiibua. Mfano mwaka wa fedha 2020/21 tumetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 50 kwa kila Zahanati iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ambapo jumla ya 566 zinaendele kujengwa.

vi. Serikali imeandaa Miongozo ya Mfumo wa Fursa na Vikwazo ulioboreshwa ili kuwasaidia Wananchi kupanga na kuwa na vipaumbele vinavyotekelezeka pamoja na kupata rasilimali kutoka kwa wadau mbalimbali zilizo juu ya uwezo wao.

4.2 Elimu Msingi

i. Upungufu wa miundombinu katika baadhi ya shule za msingi na sekondari kutokana na ongezeko kubwa la uandikishwaji wa wanafunzi wa elimu ya awali,msingi na sekondari.

ii. Upungufu wa walimu wa elimu ya awali, maalum,msingi na sekondari hasa katika masomo ya sayansi, tehama na English

iii. Mtawanyo wa makazi ya wananchi unaosababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu

iv. Upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

v. Kuibuka kwa tabia kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari kulazimisha wanafunzi kuendelea na masomo ya muda wa ziada ikiwemo wakati wa likizo

Mwelekeo

i. Kujenga na kukarabati miundombinu ya shule kongwe za msingi na sekondari. Kipaumbele kitakuwa ni kuboresha miundombinu ya shule kongwe za Msingi zilizoazishwa kabla ya Uhuru.

ii. Kujenga shule mpya 1,000 za sekondari katika kata zisizokuwa na shule na ambazo zina msongamano mkubwa wa wanafunzi. 

Na katika hatua hii wiki iliyopita tumepeka kiasi cha shilingi bilioni 109.9 kujenga shule 234 za Kata katika Majimbo yote 214 na shule 20 kwenye Halmashauri ambazo zina shule zenye uwiano mkubwa wa wanafunzi darasani. 

Kila shule itagharimu shilingi milioni 600, ambapo awamu wa kwanza tumeleka shilingi milioni 470 kwa kila shule. Nitumie fursa kueleza kuwa fedha hizi zitumike kuanza ujenzio wa madarasa 8, vyumba vya maabara ya masomo ya sayansi 3 na matundu ya vyoo.

iii. Kujenga shule mpya 26 za wasichana kwa ajili ya masomo ya sayansi. Shule 1 katika kila Mkoa. Na katika hatua hii wiki iliyopita tumepeleka kiasi cha shilingi bilioni 30 kuanza kujenga shule 10 za wasichana za masomo ya sayansi katika mikoa 10 ya Dar es salaam, Kagera, Lindi, pwani, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Songwe, Tanga na Mwanza ambapo kila shule itagharimu shilingi milioni 600 , Ninaelekeza Wakuu wa Mikoa kuanza michakato ya ujenzi wa shule mara moja na kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizotolewa.

iv. Kuajiri Walimu wa elimu ya awali, msingi na sekondari ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

v. Kujenga shule mpya za msingi ili kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye shule zenye wanafunzi Zaidi ya 2000 ili kuwa na wastani wa wanafunzi wasiozidi 1000 katika kila shule ya msingi.

vi. Kuboresha miundombinu ya madarasa ya elimu ya awali

vii. Kujenga mabweni katika shule za msingi na sekondari ili kuwahudumia wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu na hatarishi na wenye mahitaji maalum.

viii. Kuratibu utendaji wa Walimu na kuhimiza mahudhurio ya wanafunzi ili kuweza kukamilisha Kalenda ya masomo kwaa mwaka.

4.3 Huduma za Afya ya Msingi

Pamoja kazi kubwa iliyofanyika ya kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za Afya ya Msingi, bado OR-TAMISEMI inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

i. Kuwepo kwa Vituo vya Afya na Zahanati zenye miundombinu chakavu ya majengo.

ii. Uchache wa Zahanati na Vituo vya Afya katika Halmashauri mbalimbali.Kwa mfano kuna Zahanati 5,066 dhidi ya Vijiji 12,319 vilivyopo. Kwa upande wa vituo vya afya vilivyopo ni 630 dhidi ya kata 3,956 zilizopo

iii. Upungufu wa watumishi wa kada za afya kwa ngazi zote za Afya ya Msingi ambao unaathiri utoaji wa huduma bora za Afya kwa Wananchi.

iv. Uhaba wa nyumba za watumishi na miundombinu ya nishati na maji safi katika Vituo vya kutolea huduma za Afya.

v. Uhaba wa vifaa na vifaa tiba

Mwelekeo

i. Ujenzi na ukamilishaji wa zahanati kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma za afya. Na katika hili tutazingatia vigezo vinne ambayo ni Idadi ya watu, Jografia ya eneo husika, umbali kutoka kituo jirani na makao makuu ya halmshauri na mzigo wa magonjwa. 

Ujenzi wa vituo vya 481 unaendelea ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya 221 vilivyoanza kujengwa katika Tarafa na kata za kimkakati kwa kutumia fedha za miamala ya simu kiasi cha shilingi bilioni 55.2 zimeshapeleka katika Kata husika ambapo kila Kituo kimepelekewa milioni 250.

ii. Kuendelea kuboresha Miundombinu chakavu katika Vituo vya kutolea huduma za afya vya zamani.

iii. Ujenzi na ukamilishaji wa Hospitali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

iv. Kujenga nyumba za watumishi.

v. Serikali kuendelea kuajiri watumishi na kushirikiana na wadau katika kutoa ajira za Mikataba kwenye maeneo mahsusi ili kusaidia utoaji wa huduma za Afya

vi. Kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba bora kwenye Vituo vyote vya kutolea huduma za Afya-

4.4 Miundombinu ya barabara

Changamoto

- Mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 112,858.3 sawa na asilimia 78.14 ni barabara za udongo hivyo zinaharibika mara kwa mara hususan kipindi cha mvua

Mwelekeo

- Kuongeza mtandao wa barabara za udongo kuwa za changarawe. Serikali kwa kipindi cha 2021/22 hadi 2025/26 imepanga kuongeza barabara za changarawe kutoka kilometa 29,116.57 hadi kufikia kilometa 102,358.1. 

Mpango huu unakadiriwa kutumia shilingi trillion 2.974 kwa kipindi cha miaka 5, na katika hatua hii tunamshukur Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya Tarura kutoka shilingi bilioni 271 mwaka wa fehda 2020/21 hadi kufikia bilioni 966.9 mwaka wa fedha 2021/22.

Aidha Serikali kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26 imepanga kuongeza madaraja toka 2,812 hadi 6,620 sawa 135% ambapo fedha zitakazotumika kwenye mpango huu zinakadiriwa kuwa Shilingi trilioni 2.974.

Changamoto na Fursa Kuhusu Usafiri wa Umma Mijini

(i) Kukosekana kwa mfumo thabiti wa kitaasisi wenye mamlaka ya kisheria ya kupanga, kusimamia, kuendesha, kuratibu, kutekeleza na kufuatilia usafiri wa umma mijini.

(ii) Kuchelewa kwa upatikanaji wa watoa huduma kamili kwenye mfumo wa DART awamu ya kwanza.

(iii) Kuchukua muda mrefu kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya barabara ya mabasi yaendayo haraka.

(iv) Fursa ya uwepo wa ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma bora ya usafiri wa umma kwa Mkoa wa Dar es Salaam na hata miji mingine ya Tanzania, mfano mahitaji ya usafiri wa umma na miundombinu bora ya watembea kwa miguu ni asilimia 84 (Dar es Salaam), asilimia 80 (Dodoma), asilimia 90 (Mwanza), asilimia 70 (Arusha), asilimia 87 (Tanga), na asilimia 70 kwa Mkoa wa Mbeya. Pia, kuna fursa ya uhitaji wa maeneo nadhifu kwa ajili ya shuguli za biashara na huduma za jamii.

Mwelekeo

(i) Kutunga Sheria mahususi ya kuboresha usafiri wa umma kwenye miji yote ya Tanzania kupitia miundombinu na huduma zilizoratibiwa, na kufungamanishwa ili kuhakikisha kuwa miundombinu na huduma hizo ni zenye ufanisi na endelevu kwenye nyanja za kiuchumi, kijamii, na afya ya watu na mazingira.

(ii) Kuanzisha utaratibu wa kukuza na kutekeleza uratibu na ufungamanishi wa huduma bora ya usafiri wa umma mijini ikiwa ni pamona na kutenga na kueneleza maeneo maalum kwa ajiri ya wafanyabiashara, wakiwemo wafanyabishara wadogo, na maeneo ya wazi ya umma (public spaces).

(iii) Kuongeza mabasi idadi ya mbasi kwa awamu ya kwanza kutoka 210 yaliyopo sasa hadi 305 ifikapo Julai 2022 kwa awamu ya kwanza, na kuleta mabasi yapatayo 755 kwa ajili ya kutoa huduma kwenye awamu ya pili ifikapo Machi 2023. 

Aidha, kuanza maadalizi ya kuongeza mabasi kwenye awamu nyingine hadi kufikia kiasi cha mabasi yapatayo 3,650 yanayohitaji kwa awamu zote ifikapo mwaka 2025.

(iv) Kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya mradi yenye jumla ya kilometa 109.74 ifikapo mwaka 2025, hii ikiwa ni kwa awamu zote sita kwa Mkoa wa Dar es Salaam sambamba kuanza kwenda kwenye miji mara baada ya maboresho ya kufanyika kwa sheria.

(v) Kukamilisha ujenzi na usimikaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Nauli ulifungamanishwa na Mfumo wa Kuongoza Magari (ITS) ifikapo Julai 2022, ikiwa ni sehemu endelevu ya maboresho ya huduma ya usafiri wa umma mijini.

(vi) Kuongeza wigo wa vyanzo wa mapato yasiyotokana na nauli kwa kuwekeza kwenye fursa fungamanishi na huduma za usafiri wa umma kwa lengo kuwa na huduma endelevu ya usafiri wa umma mijini.

4.5 Uwezeshaji wananchi kiuchumi

i. Baadhi ya vikundi kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati

ii. Uhitaji wa mikopo kutolewa katika vikundi vya kuanzia watu 5.

iii. Baadhi ya Halmashauri kushindwa kutenga fedha zinazotosheleza mahitaji ya mikopo ya vikundi

Mwelekeo

i. Kuweka utaratibu mzuri wa utakaowezesha vikundi vilivyokopeshwa kurejesha fedha kwa wakati.

ii. Kusimamia kanuni ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ili kuruhusu hata mlemavu mmoja mmoja kupata mkopo.

iii. Kuweka utaratibu utakaowezesha idad ya wanakikundi kupungua kutoka watu watano hadi watatu, na kwa upande wa watu wenye ulemavu kuhakikisha mikopo inatolewa kwa mtu mmoja mmoja.

iv. Kuweka mifumo thabiti ya kuimarisha ukusanyaji na utoaji wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake,vijana na watu wenye ulemava

4.6 Tehama

- Uchakavu na upungufu wa miundombinu ya TEHAMA katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

- Upungufu wa Wataalam na vitendea kazi vya TEHAMA

- Baadhi ya Halmashauri kutokuwa na mtandao imara wa intaneti

Mwelekeo

i. Kuendelea kuajiri na kuwajengea uwezo watumishi waliopo katika fani za TEHAMA

ii. Ununuzi wa vifaa na vitendea kazi vya TEHAMA

iii. Kuhimiza na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA

5.0 HITIMISHO

Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kutekeleza Sera na Mikakati ya kuwapatia huduma bora wananchi kupitia Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo 2021/22-2025/26 pamoja na kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020.

"Mafanikio ya utekelezaji yametokana na kazi kubwa inayofanywa na viongozi wenzangu wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI ambao ni mheshimiwa David Silinde (Mb) Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI na Festo Dugange (Mb) Naibu Waziri anayeshughulikia Afya. 

"Napenda kutambua kazi kubwa inayofanywa na Katibu Mkuu Prof Riziki Shemdoe akisaidiwa na Naibu Makatibu Wakuu Gerald Mweli anayeshughulikia Elimu na Dkt. Grace Magembe anayeshughulikia Afya.

Vilevile, nawashukuru Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Wakurugenzi wa Halmashauri na watumishi wote kwa namna walivyotimiza wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha, Ofisi ya Rais TAMISEMI inawashukuru wadau wanaowezesha utekelezaji wa miradi na program mbalimbali za maendeleo wakiwemo sekta binafsi, mashirika ya dini, wadau wa maendeleo na wananchi waliochangia nguvu kazi katika utekelezaji wa miradi.

Katika kipindi hiki Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, Wizara ya Kisekta Binafsi, mashirika ya dini na wananchi wote katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Napenda kusisitiza viongozi na watendaji kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ifikapo mwaka 2025,"amebainisha kwa kila Waziri wa OR-TAMISEMI, Ummy Mwalimu.

Mwelekeo

i. Halmashauri zinazokusanya mapato ya ndani yasiyolindwa Zaidi ya shilingi bilioni 5 kutenga asilimia 10 kwa ajili ya miundombinu ya barabara. 

Aidha serikali itaendelea kutafuta vyanzo vingine vya mapato kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara

ii. Kuendelea kuajiri wahandisi wa miundombinu ya barabara

iii. Upungufu wa wataalam katika fani mbalimbali

iv. Kuwepo kwa maombi mengi ya uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala bila kukidhi vigezo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news