MIAKA 60 YA UHURU: KIJUWE CHUO KIKUU HURIA NA MCHANGO WAKE KWA NCHI YETU YA TANZANIA


1. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu kimejipambanua kwa kuwapelekea wananchi Elimu ya juu katika maeneo wanayoishi mijini na vijijini. 

Kupitia Programu ya Foundation chuo kimeweza kuwawezesha watu wengi waliopungukiwa sifa kidogo za kuendelea na elimu ya juu kupata sifa na kujiendeleza mpaka ngazi za juu as elimu.

2. CKHT kilianza rasmi mwaka 1992, kupitia Sheria ya Bunge Na. 12. Utaratibu wa kujifunza na kufundishia unaotumiwa na Chuo, ulianza kutumika Tanzania Bara, kuanzia mwaka 1924.

3. Utaratibu huo wa Elimu kwa Njia ya Posta (Correspondence Education) ulishika kasi kubwa miongoni mwa wenyeji baada ya Vita Kuu ya Dunia ya Pili. Wasomi na hivi Wataalamu wengi wenyeji baada ya Uhuru mwaka 1961, walikuwa wamepata elimu kwa njia hii ya correspondence education. Itoshe tu kumtaja mmoja. Kamishna wa kwanza mwenyeji wa Jeshi la Magereza na Mtaalamu wa Kilimo na Ufugaji, Marehemu Obadiah Rugimbana.

4. Baada ya Uhuru, juhudi za makusudi zilifanywa na Serikali kuunda Taasisi za Kitaifa kuwaendeleza Wananchi kwa njia hii ya correspondence education. Hizi ni pamoja na Idara ya Masomo ya Jioni, Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Chuo cha Ushirika Moshi. Hadi mwaka 1992, Taasisi zote hizi zilikuwa zimechangia kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya rasilimali watu. Haishangazi kwamba toka mwaka 1980 ilikwishajitosheleza kwa mahitaji ya Wataalamu wa fani mbalimbali za msingi. 

5. Kukidhi mahitaji ya elimu endelezi (continuing education) kwani elimu haina mwisho (life long learning) na upatikanaji wa elimu kwa kila mtu (education as a basic human right), jitihada za kuanzisha Chuo Kikuu Huria, zilianza rasmi kutokea mwaka 1979 na kufikia kilele chake mwaka 1992, Chuo kilipoanza. 

6. Chuo kimetoa mchango gani kwa maendeleo ya elimu na rasilimali watu kwa takriban miaka 30 iliyopita? Tuangalie maeneo matatu tu; udahili, kuimarisha mfumo wa elimu na upekee wa Wahitimu.

(i) CKHT kimeweza kudahili Wanafunzi wengi zaidi kuliko Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Bweni kwa pamoja. Hii imesaidia sana kiwango cha Gross Tertiary Enrolment Rate cha Tanzania kupanda kwa haraka zaidi. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, kipimo hiki kinaakisi pia kiwango cha Uchumi wa Taifa husika. Kwa hivi, kuwapatia Watu fursa ya kujiendeleza kielimu na hususan kwa njia ya Elimu Huria huchangia sana kuinua kiwango cha Uchumi wa Nchi.

(ii) Idadi kubwa ya Wahitimu wa CKHT ni wa Programu za Vyeti na Diploma. Kwa hivi, pamoja na kuimarisha Elimu ya Msingi, Chuo kimetoa mchango mkubwa katika kuwajengea weledi wahitimu hao kuendelea na Programu za Shahada za kwanza. Tukiendelea kukiimarisha Chuo hiki, kila Mtanzania ana uhakika wa kusoma vizuri kuanzia Chekechea hadi Chuo Kikuu.

(iii) Chuo kimefanikiwa kutoa Wahitimu wa mfano. Tutoe mifano michache. Muhitimu wa kwanza wa Shahada ya BSc (Mathematics), mwaka 2000, alikuwa mfanya biashara mdogo (machinga) wa mitumba, Manzese, Dar es Salaam. Aliendelea na masomo ya Uzamili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye China na akafanikiwa kuhitimu katika fani ya Computer Science. Muhitimu wa kwanza Mama wa Shahada ya BSc (Education) alikuwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari. Aliendelea na masomo ya Uzamili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hatimaye akamalizia Shahada ya Uzamivu, CKHT. Hivi sasa ni Mkuu wa Idara ya Sayansi, CKHT. Yupo Muhitimu aliyeweka Rekodi ya Dunia kwa kusoma na kuhitimu Shahada ya BA (Education) kwa miaka miwili badala ya miaka 3 - 6). Baba wa Taifa alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Usomi (Doctor of Letters (Honoris Causa) na CKHT kwenye Mahafali yake ya kwanza Machi 5, 1999. Hiyo ilikuwa ni Shahada yake ya heshima ya mwisho, kwani alifariki Oktoba 14, 1999. Hata hivyo, ilikuwa ni Shahada pekee miongoni mwa Shahada zake za heshima zaidi ya 12, kutoka Chuo Kikuu Huria. Mwenyewe alisema "naona fahari kuwa Chuo Kikuu Huria hicho ni cha Tanzania".

Mfululizo wa Insha za Elimu na Maendeleo kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Mwandishi

Dkt. Nevile Ruben

Mhadhiri Msitaafu

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania 

18/12/2021

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news