Mtandao wa barabara waboresha maisha ya wananchi Singida

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

UWEPO wa mitandao ya barabara kuu na za viunganishi mkoani Singida zimeongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi na kukuza uchumi wa mtu mmoja moja kutokana na biashara zinazofanyika baina ya wilaya na halmashauri mbalimbali.
Mkoa huo umetajwa kuwa na mtandao wa barabara wenye urefu wa jumla ya kilomita 1,716.12 ambapo lami ni kilomita 488.73 na changarawe ni kilomita 1,227.39.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Binilith Mahenge alipokuwa akifungua kikao kazi cha 44 kilichohusu Bodi ya Barabara ya Mkoa ambacho kimefanyika Desemba 3, 2021 katika ukumbi wa mkoa huo na kuhusisha Wakala wa Barabara (TANROADS), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wabunge wa mkoa huo, viongozi wa CCM mkoa, wenyeviti wa halmashauri, wakurungezi watendaji na wataalamu mbalimbali wa Serikali.
Akiongea katika kikao hicho, RC Mahenge amesema, mifumo ya barabara iliyopo katika mkoa huo umefungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa imeendelea kuunganisha mkoa na mikoa mingine, miji na maeneo ya kitalii pamoja na migodi ya madini.

“Mifumo ya barabara imekuwa kama mishipa ya damu ambayo ikisimama kila kitu kina simama, nawashukuru sana TANROADS na TARURA kwa kusaidia kuboresha barabara za lami na zile zenye kiwango cha changarawe,”amesema RC Mahenge.

Aidha, amewaomba viongozi waliohudhuria kikao hicho kuhakikisha wanasaidia kusimamia ujenzi wa barabara zote zinazoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapo kwa kuwa fedha nyingi za barabara zinaendelea kuja.

Aidha, Mkuu wa Mkoa akaendelea kuwakumbusha wakandarasi wote wanaoshughulika ujenzi wa barabara kuhakikisha wanatekeleza kazi zao kwa muda walipewa kwa kuwa hatapenda kusikia sababu zozote zitakazosimamisha ujenzi huo.

Akiwakilisha taarifa yake Meneja wa TANROADS Mkoa, Mhandshi Erick Ng’walali amesema, hali ya barabara katika Mkoa wa Singida inaridhisha kwa kuwa asilimia 63.1 ni barabara zenye hali nzuri, asilimia 27.6 ni hali ya wastani wakati asilimia 9.3 tu zina hali mbaya.

Aidha, Mhandisi Erick akafafanua kwamba bado wameendelea kufanya matengenezo katika baadhi ya barabara mkoani hapo ambapo asilimia 32.7 zimekamilika na asilimia 14.4 za fedha zimekwishatumika.

Hata hivyo, Mhandisi Erick amezitaja baadhi ya changamoto zikiwemo wizi wa vyuma na alama za barabarani ambapo amesema elimu na uhamasishaji vinahitajika katika maeneo mbalimbali ili kutunza alama hizo ambazo ni muhimu kwa watumiaji wa barabara.
Aidha, akatumia muda huo kuwaonya baadhi ya watu wanaotumia vibaya hifadhi ya barabara ikiwemo kupasua mifereji ya maji, kujenga na kupitisha mifugo katika sehemu ambazo hazistahili.

Akitoa maazimio ya kikao hicho Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko amesema ahadi zote zilizotolewa na viongozi wa juu kuhusiana na ukarabati na utengenezwaji wa barabara utaingizwa kwenye mpango na kuhakikisha unatekelezwa na wananchi wanafaidika.
Aidha, amewataka TANROADS na TARURA kuboresha barabara na madaraja yote yenye uhitaji huo ndani ya mkoa mzima ili kuondoa athari zinazoweza kutokea wakati wa mvua.

Post a Comment

0 Comments